November 22, 2014

PANTILIMON 

Na Saleh Ally
UNAWEZA ukashangazwa na mambo mengi sana ya Ligi Kuu England ambayo ndiyo ligi maarufu zaidi ya soka duniani.


Ligi hiyo ndiyo inaongoza kwa kuwa na watu warefu zaidi duniani, kwa kuwa wachezaji wengi wana maumbo makubwa.

Usisahau, pamoja na kwamba ndiyo ligi yenye kasi zaidi, bado inaongoza kwa kuwa na wachezaji wenye kilo nyingi zaidi ukilinganisha na ligi nyingine.

Unaweza kujiuliza vipi Ligi Kuu Bara isiwe na kasi zaidi kwa kuwa wachezaji wake si wenye maumbo makubwa, maana yake walipaswa kuwa na kasi ya uhakika ukilinganisha na England.
 
GERRARD
Wachezaji kama Mrisho Ngassa wa Yanga au Ramadhani Singano wa Simba, vipi wasikimbie kwa kasi zaidi ya Eden Hazard wa Chelsea au Antonio Valencia wa Manchester United na Theo Walcott wa Arsenal?

Mazoezi makali ya kutosha, vifaa vizuri vya kujiandaa na kufuata utaratibu wa weledi wa mchezo husika vinachangia ongezeko la kasi.

Usijidanganye, eti mtu mzito hawezi kufunga, inategemea timu yake inamtumia vipi. Mfano Romelu Lukaku ana kilo 97, ndiye mshambuliaji mzito kuliko wote England, lakini anakibizana na mabeki na kufunga mabao kwa Everton.
 
LUKAKU
Kiungo mzito kuliko wote England ni Yaya Toure wa Man City. Mtu mzima ana kilo 90, si mchezo lakini umewahi kumuona akiwa kwenye mwendo?

Ila kwa England, makipa ndiyo wanaotia fora zaidi kwa uzito, maana kipa Costel Pantilimon anayecheza kwa mkopo Sunderland akitokea Man City ana kilo 100.

Makipa hawalazimiki kukimbia sana, wengi wao wana maumbo makubwa zaidi na Pantilimon raia wa Romania ndiye mchezaji mrefu zaidi England kwa kuwa ana urefu wa futi 6 na inchi 8.

Wastani unaonyesha makipa wengi ndiyo watu wazito zaidi England. Hata ukiangalia tano bora kwenye listi iliyo kwenye ukurasa huu, wao ndiyo wazito zaidi.

Washambuliaji wanaingia kwenye namba mbili ya uzito kwa kuwa wengi wanaanzia kilo 75 hadi 90 na kitu. Wastani wa uzito wa mabeki hasa wa kati, hauna tofauti sana na washambuliaji.

Viungo ndiyo viumbe wepesi zaidi Premier League kwa kuwa ndiyo wanaocheza zaidi uwanjani. Mpira huchezwa zaidi katikati wakati mabeki na viungo kati yao ni kuokoa na kufunga.

Sayansi inaonyesha, wenye maumbo makubwa kama wakifanya mazoezi ya kutosha, kwa sayansi ya uhakika, wanaweza kuwa na kasi kuliko mtu mfupi lakini kwa mwendo mfupi.

MAKIPA:
1. Costel Pantilimon (Sunderland) Kg 100
2. Mark Schwarz (Chelsea) Kg 94
3. Fraser Forster (Southampton) Kg 93
4. Simon Mignolet (Liverpool) Kg 92
5. Peter Cech (Chelsea) Kg 92

MABEKI:
1. Richard Dunne (QPR) Kg 95
2. John Terry (Chelsea) Kg 90
3. Chris Smalling (Man Utd) Kg 90

VIUNGO:
1. Yaya Toure (Man City) Kg 90
2. Kevin Nolan (West Ham) Kg 89
3. Steven Gerrard (Liverpool) Kg 83

STRAIKA:
1. Romelu Lukalu (Everton) Kg 97
2. Chris Wood (Leicester) Kg 94
3. Didier Drogba (Chelsea) Kg 91


0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic