November 28, 2014


Kocha Jose Mourinho ndiye anayetajwa kuwa ghali zaidi barani Ulaya kwa upande wa klabu kutokana na kitita cha pauni milioni 17 (Sh bilioni 37) anazochota kwa mwaka.


Mourinho aliyerejea Chelsea ya England akitokea Real Madrid ya Hispania, angeweza kufanya kazi nchini kwa mkataba mnono kama huo kwa miaka nane, iwapo angelipwa kitita cha Sh bilioni 306 zinazoelezwa kuchotwa kwenye akaunti ya Tegeta Escrow.

Wizi wa fedha hizo ndiyo gumzo nchini, sakata lake limeendelea kufukuta bungeni hadi jana usiku, lakini kama zingetolewa kwa ajili ya kuendeleza soka, akachaguliwa kocha wa kuinoa Taifa Stars awe Mourinho, angelipwa mshahara safi kwa miaka nane, bila ya hofu yoyote.

Kwa fedha hizo, Taifa Stars ingeweza kufundishwa na kocha yeyote wa daraja la juu duniani kuanzia miaka nane hadi 15 na angekula ‘bata’ anavyotaka bila kucheleweshewa mshahara.

Makocha wengine wa daraja hilo ambao wangeweza kulipwa bila shida kwa ‘mafedha’ hayo ya Escrow yaliyochotwa kwa maboksi na mifuko ya sandarusi ni Pep Guardiola wa Bayern Munich na Carlo Ancelotti wa Real Madrid ambao wanavuta kwa mwaka euro milioni 14 (Sh bilioni 30).

Kwa kitita anacholamba Mourinho kwa mwaka kutoka Chelsea, maana yake angeweza kuishi nchini kwa miaka nane, mfano hivi; akiinoa Taifa Stars.

Kwani ukipiga hesabu ya Sh bilioni 37 na ushee mara nane, unapata jumla ya Sh bilioni 300 na ushee ambazo ndizo zinazoelezwa kuchotwa kwenye akaunti hiyo.

Ukitaka makocha wa daraja la kati, mambo yangekuwa tofauti. Mfano uwachukue makocha wanaolipwa hadi bilioni 10 kwa mwaka kama Andre Villa Boas (AVB) aliyewahi kuzinoa Chelsea na Tottenham Hotspur wanaoweza kulipwa hadi Sh bilioni 15 kwa mwaka, wao wangeweza kukaa hadi miaka 16 hapa nchini wakifanya kazi kwa malipo ya fedha za akaunti ya Tegeta Escrow.

Fedha hizo pia kama zingeingizwa kwenye michezo kupitia viwanja vyenye uwezo wa kuingiza watu 30,000 ambazo kwa mujibu wa kampuni moja ya ujenzi nchini, vinaweza kugharimu hadi Sh bilioni 32, basi Simba, Yanga na klabu nyingine nane za Ligi Kuu Bara, zingepata viwanja vyake, saafi.

Sakata hilo bado linaendelea na kumekuwa na shinikizo Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, naibu wake, Steven Massele, katibu wake, Eliakimu Maswi na Mwanasheria Mkuu, Fredirick Werema wanatakiwa kuachia ngazi kwa madai wamehusika kwa kiasi kikubwa.


Kweli kama fedha hizo zingechotwa, halafu zikatupiwa kwenye michezo, basi mara moja Tanzania ingeanza kuwa gumzo dunia nzima.

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic