SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limeanza mchakato wa
kutafuta jezi mpya ya timu ya taifa, Taifa Stars.
TFF imeanza mchakato huo mara tu baada ya kuanza
kushindwa ule wa kutaka kubadilisha jina la timu ya taifa na wadau wakawa wakali
kweli.
Katika mchakato wa kutafuta jezi hizo mpya za timu ya
taifa, TFF ilianza kutangaza wabunifu wajitokeze, wachore kitaalamu ili
kuwasilisha michoro ya jezi hizo.
Hilo likafanyika na kwa mujibu wa TFF, Watanzania 86
walijitokeza katika ubunifu huo kwa kupendekeza aina ya jezi walizoona ni
sahihi.
Jezi 11 za nyumbani, bukta nane za nyumbani, jezi nane
za ugenini na bukta tano za ugenini. Maana yake kweli katika kipindi kifupi,
watu wamejitokeza.
Hilo ni jambo la kujivunia hasa kama kweli wabunifu hao
waliofanya ubunifu ni Watanzania kweli. Kimwenendo, inaonekana wazi TFF hawana
mtaalamu wa kuwashauri vizuri kuhusiana na suala hilo.
Kwani wameamua kufanya michakato ya aina mbili. Kwanza
wameiweka michoro ya jezi hizo kwenye mtandao wao. Mchakato wa pili ni watu
waanze kupiga kura kwa kubofya kwenye picha za michoro na mwisho kura zitaamua
zipi ziwe jezi za nyumbani na ugenini za Taifa Stars.
Mimi naona hicho ni kichekesho, ndiyo maana nasisitiza,
TFF hawana utaalamu wa masuala hayo na hilo halina ubishi. Hivyo walipaswa
kuwapa nafasi watu wanaoweza kuifanya kazi hiyo, nitaukosoa kwa hoja mchakato
huo.
Kwanza:
Kuweka kwenye mtandao watu wapige kura kuna uwezekano
mkubwa wa mbunifu mmoja ambaye jezi zake zinaweza zisiwe na mvuto zaidi, lakini
akawa mjanja katika ushiriki wa kubofya mara nyingi kwa kutumia watu
mbalimbali, mwisho akashinda wakati hakustahili.
Pili:
Kama kweli lengo la TFF ni kuhakikisha Watanzania wote
wanashiriki, inajua Watanzania wangapi wanaoingia kwenye mtandao huo wa TFF?
Jiulize watu wa Makete, Iringa au Kyaka, Kagera au Dihimba, Mtwara na
kwingineko, wana nafasi ya kuingia kwenye mtandao?
Wote hao ni Watanzania, unapoweka hadharani, maana yake
unazungumzia usawa. Sasa utapatikana vipi kama kura zitapigwa na watu wa mijini
tu, tena wale wanaotumia mitandao tu? Na nani kawaambia TFF mitandao inatosha
kufikisha kura?
Tatu:
Tayari TFF imezianika jezi hizo hadharani, inatambua
jezi kwenye klabu au timu ya taifa ni biashara. Angalau ungekuwa mchakato wa
siri hadi siku jezi inatangazwa, wabunifu wangeweza kupeleka kazi zao
kimyakimya, nitakupa sababu.
Kitaalamu katika ulimwengu wa sasa, feki ndiyo gumzo.
Kabla hata TFF haijachapisha jezi hizo, zinaweza kuingia mitaani na kuuzwa,
tayari ni hasara kubwa.
Hata siku moja hauwezi kusikia Adidas wanatangaza aina
fulani ya jezi zao kabla ya kuzitengeneza. Zikiwa tayari na zimeingia mtaani,
ndiyo wanatangaza, huo ni mfumo wa kibiashara kote duniani.
Bado utajiuliza, TFF kama inataka kuanika hadharani ‘dizaini’
ya jezi zake, zitatengenezwa na kampuni ipi ambayo itakubali kuchukua kitu
kilichosambaa kila sehemu hata kabla ya kukabidhiwa?
Dunia nzima, kwa sasa kila mmoja anaficha ubunifu wa
kitu chake. Iwe kuimba, kuchora au vinginevyo hadi unapofikia wakati wa kukitoa
kitu husika. Vipi TFF haioni hilo?
Kingine, TFF lazima wakubali kazi yao ni mpira, hivyo
wana kila sababu ya kufanya mgawanyo wa kazi. Wawaachie wataalamu kwenye sekta
nyingine wafanye kazi ili kufanya mambo yasonge. Kung’ang’ania kila kitu ni
kutanguliza siasa kwenye soka.
Pia kama mchakato utaendelea kwa njia hii, inaweza
kuiingiza TFF kwenye shimo la kashfa kwamba ilipanga mapema. Maana hata wapiga
kura, watakuwa wachache na hawana haki ya kuwawakilisha Watanzania wote wapenda
mpira.
Hapa kuna kaescrowwwwwww fulani either kwa tff or sj!
ReplyDelete