KILA unapokatiza kwenye mitaa habari ni juu ya sakata la fedha za
Escrow, kila mtu anazungumza lake, lakini hiki kilichosemwa na straika wa
Yanga, Jerryson Tegete, mmmh!
Tegete amesema kuwa wahusika wote walioiba mabilioni ya fedha za
mradi wa umeme, wanatakiwa kunyongwa kwa sababu imekuwa mazoea yao kuiba fedha
za wananchi.
Sakata hilo limekolea hasa baada ya juzi Kamati ya Hesabu za
Serikali na Mashirika ya Umma (Pac) chini ya mwenyekiti wake, Zitto Kabwe,
kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, mawaziri na viongozi wengine kuwajibika
kutokana na kashfa hiyo.
“Hali inayoendelea sasa katika nchi yetu inasikitisha kwa sababu
bado Watanzania wengi wanaishi katika maisha magumu kutokana na kodi kuwa
kubwa, uchumi wenyewe unazidi kudidimia kila kukicha lakini cha kushangaza,
viongozi ambao tunawategemea ndiyo wamegeuka kuwa wezi wa mabilioni ya fedha.
“Fedha hizo zingeweza kusaidia wananchi kupata huduma muhimu kama
elimu, maji na umeme.
“Nadhani hatua nzuri ambayo inapaswa kuchukuliwa kwa sababu imekuwa
kawaida kwa viongozi kufanya mambo kama hayo ni kunyongwa kwani itasaidia
kuwafanya wengine waogope kufanya kama hivyo kwani mambo hayo yanaturudisha
nyuma katika maendeleo ya nchi,” alisema Tegete.
Alipoulizwa Rais wa Simba, Evans Aveva juu ya suala hilo alifunguka:
“Hayo mambo ni makubwa mno kwani hadi waziri mkuu yumo, mpira na siasa ni vitu
viwili tofauti, hivyo siwezi kusema chochote. Nina imani sheria itafuata
mkondo.”
Upande wa Katibu Mkuu wa Klabu ya Yanga, Beno Njovu, alishikwa na
kigugumizi na kusema: “Mimi naangalia familia yangu jamani, watoto bado wadogo
sana na wananihitaji. Sitaki kuzungumzia hizo habari. Escrow ina mambo mengi
sana.”
0 COMMENTS:
Post a Comment