Siku mbili tu baada ya kujiunga na kuanza mazoezi na kikosi cha Azam FC, aliyekuwa kiungo mshambuliaji wa Simba, Amri Kiemba,
amesema amejiunga na timu hiyo kwa ajili ya kucheza mashindano ya kimataifa.
Azam FC itaiwakilisha Tanzania Bara
katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoanza kutimua vumbi mwakani
baada ya kupata tiketi hiyo kutokana na kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu
uliopita.
Kiemba
amesema kuwa tangu aliposhiriki mashindano hayo miaka mitatu iliyopita akiwa na
Simba na kufanikiwa kufanya vizuri, alikuwa na hamu kubwa ya kuendelea kufanya
hivyo lakini ndoto hizo zilikwama.
Alisema hali hiyo ilikuwa ikimkosesha amani, lakini baada ya kutua
Azam FC, amepata matumaini mapya, hivyo Mungu akimjalia uzima atatimiza ndoto
yake.
“Lakini pia nitakuwa nafanikiwa
kuandika rekodi ya kuwa miongoni mwa wachezaji wachache wa hapa nchini waliowahi
kushiriki mashindano hayo wakiwa na klabu tatu tofauti.
“Kwa mara ya kwanza nilishiriki mashindano
hayo nikiwa na Klabu ya Yanga, baadaye Simba na sasa Mungu akipenda nitashiriki
nikiwa na Azam, hakika nina furaha sana na ninaamini kuwa nitafanya vizuri,”
alisema Kiemba.
Kiemba amejiunga na Azam FC kwa mkopo
wa miezi sita ikiwa ni baada ya uongozi wa Simba kumsimamisha pamoja na
wachezaji wenzake, Haruna Chanongo na Shabani Kisiga kwa madai ya utovu wa
nidhamu.
0 COMMENTS:
Post a Comment