Na Saleh Ally
MMOJA wa makocha ambao
hawatapotea katika historia ya Klabu ya Simba kwa kipindi kirefu ni Milovan
Cirkovic.
Milovan, raia wa Serbia,
amekuwa mmoja wa makocha waliopendwa zaidi katika klabu ya Simba na amewahi
kuifundisha kwa vipindi viwili tofauti.
Kocha huyo mtaratibu katika
mazungumzo, ndiye aliiongoza Simba katika msimu mmoja kuifunga Yanga mabao 5-0,
pia kubeba ubingwa wa Tanzania Bara.
Milovan aliiongoza Simba
kuwa na kikosi kinachocheza soka la uhakika na hata mabingwa wa sasa wa Afrika,
Setif ya Algeria, walitua jijini Dar es Salaam na kulambwa mabao 3-1 na baadaye
kutolewa kabisa kwenye michuano hiyo.
Hakuna ubishi, kikosi cha
Simba wakati huo kilikuwa moja ya vikosi bora vilivyowahi kutokea katika klabu
hiyo.
Mei 6, 2012, Simba ilitoa
kipigo hicho cha mabao 5-0 kwa Yanga katika mechi ya kumalizia Ligi Kuu Bara.
Hiyo ni sehemu ya kumbukumbu ya kocha huyo ambaye sasa ni Kocha Msaidizi wa
timu ya taifa ya Myanmar.
Mechi hiyo ni gumzo zaidi
kwa mashabiki wa Yanga na Simba. Haijasahaulika na huenda ikachukua muda kutoka
midomoni na masikioni mwa mashabiki wa soka.
Wakati Milovan anaondoka
nchini, Simba ikiwa chini ya Ismail Aden Rage, aliwaambia mashabiki wa soka
nchini kwamba ushindi kama huo kwa Simba au Yanga, utatokea baada ya miaka
mingine mingi au utatokea si kwa kutarajia, hivyo Yanga hawana sababu ya
kupambana kutaka kulipa katika mechi wanayocheza.
Milovan anaendelea na kazi
yake vizuri katika nchi hiyo ndogo ya Bara la Asia na sasa yuko nchini
Singapore ambako kuna michuano ya Suzuki Cup.
Michuano hiyo inashirikisha
timu nane zilizo katika makundi mawili na inachezwa katika nchi mbili za
Singapore na Vietnam.
Akihojiwa na SALEHJEMBE kutoka Singapore, Milovan
anasema ameendelea kuwa mpenzi mkubwa wa Simba na kamwe hajawahi kuusahau
ushindi wa mabao matano dhidi ya Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment