Na Saleh Ally
KWA matokeo ya mechi za Jumamosi,
maana yake Ligi Kuu Bara sasa haitabiriki na huenda inakwenda kwenye viwango
sahihi vinavyoweza kuitwa ni vya ushindani.
Mechi nne tu za Jumamosi zinaweza kuwa
uthibitisho kwamba ligi hiyo sasa ni ngumu kweli na haitabiriki.
Muonekano ulikuwa ni timu fulani ina
nafasi ya kushinda kutokana na kuwa imara au kwa kuwa ile nyingine inaonekana
kibonde kwa kupoteza mechi moja au zaidi kabla.
Timu moja ilikuwa na sare nyingi,
nyingine ina ushindi mfululizo, lakini mechi zote nne zikawa na matokeo ambayo
hayakutarajiwa.
Kuwa na mechi ambazo si rahisi
kubashiri au kutabiri mshindi ni sehemu ya kuonyesha ugumu wake.
Kwa matokeo hayo ya juzi, sasa inaonyesha
haina mwenyewe na yeyote anaweza kufungwa wakati wowote na timu yoyote.
Mtibwa Sugar
1-1 Simba:
Simba ilikuwa inapambana kupata
ushindi wa kwanza na kuepuka sare, Mtibwa Sugar ambayo pia haijafungwa lakini
iko moto maana yake katika mechi tano ilikuwa imeshinda nne, sare moja na iko
kileleni ikiwa na pointi 13.
Simba ikaanza kufunga lakini Mtibwa
ikasawazisha kwa bao la Mussa Hassan Mgosi baada ya kipa kinda Peter Manyika
kuukosa mpira wakati akijaribu kuudaka.
Ugumu hapa utauona, ni timu yenye sare
tano ambayo ilionekana wazi haina kitu lakini iliyokuwa ikipewa nafasi ndiyo
imelazimika kusawazisha na sare yakawa matokeo bora lakini yasiyotegemewa kila
upande.
Kagera 1-0
Yanga:
Ilikuwa mechi nzuri, ushindani wa juu,
lakini Yanga ilikwenda Bukoba ikijua Kagera ni wagumu wakiwa kwao Kaitaba. Hata
hivyo, baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Stand mjini Shinyanga, Yanga
ilionekana iko tayari kwa lolote.
Kagera haikuwa inaaminika sana,
ilishayumba, nani tena anaiamini? Lakini kwenye uwanja wake wenye kiwango
kibaya wa Kaitaba ikaichapa Yanga kwa bao bora la Paul Ngwai ikaizamisha Yanga
iliyoaminika imeanza kazi!
Ndanda FC
1-0 Azam FC:
Mabingwa watetezi Azam FC walikuwa
wametoka kupoteza mechi dhidi ya JKT Ruvu wakiwa nyumbani Azam Complex. Safari
yao kwenda Nangwanda Sijaona mjini Mtwara ilionekana hawana kazi ngumu.
Sababu mbili tu, kwanza walikuwa
wanakutana na Ndanda ambayo imefungwa ugenini, imefungwa mara mbili nyumbani,
hivyo imepoteza mwelekeo. Kwa mabingwa hao watetezi wenye kikosi imara,
wasingekubali kupoteza tena mfululizo.
Wapi bana! Azam FC wakalowa bao moja
bila majibu. Hakuna aliyetarajia kuanzia ndani ya kikosi hicho cha Chamazi na
wadau wengine wote kwamba Ndanda itaamka siku inapokutana na Azam FC!
JKT Ruvu 1-2
Polisi:
JKT Ruvu waligoma kufungwa Mbeya kwa
kuichapa Prisons, usisahau kabla waliikamata Mbeya City kwa sare ya bila mabao.
Walipotua Chamazi wakaitungua Azam FC na safari hii wakawa wanakutana na Polisi
Morogoro.
Wakati wameanza kufunga bao, wengi
waliamini mvua ya mabao ilikuwa inafuatia kwa Polisi Morogoro. Wapi,
mshambuliaji mkongwe, Danny Mrwanda akafunga mabao mawili na kuizima timu hiyo
ya jeshi chini ya beki wa zamani wa Yanga, Fred Felix Minziro.
Kwa mechi hizo, tayari zinaonyesha
hakuna urahisi tena na ndiyo wakati wa soka ya Tanzania kupanda kimaendeleo
kama katikati suala la rushwa au uchezeshaji mbovu wa marefa havitaingia.
Pamoja na ugumu kuanza kuonekana, pia
kuna kitu cha kujifunza kwamba viwanja vya mikoani ni tatizo kwa maana ya
kiwango.
Ukiwa ulibahatika kuangalia kwenye
Azam TV, itakuwa nafasi nzuri ya kung’amua asilimia 90 ya viwanja vya mikoani
ni tatizo kubwa kwa soka ya nchi yetu.
Uwanja pekee wa mkoani ambao
unaonekana na kiwango bora kuchezewa soka ni Kambarage mjini Shinyanga.
Vilivyobaki, yaani Sokoine Mbeya, Kaitaba, Bukoba, Jamhuri, Morogoro na
Mabatini, Mlandini ni tatizo.
Hivyo inawezekana ugumu wa mechi za
mikoani kwa timu za Dar es Salaam ukawa si viwango na badala yake ubovu wa
viwanja.
Hivyo ni tathmini inayoweza kugeuzwa
juu na chini kuwa ligi ni ngumu sababu ya uwezo wa timu za mikoani kubadilika
kwa kiwango lakini bado inaweza kubaki kuwa hivi; viwanja navyo vinaongeza
ugumu wa ligi hiyo.
0 COMMENTS:
Post a Comment