Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ anatarajiwa
kuikosa mechi yenye upinzani mkubwa ya Ligi Kuu Bara dhidi ya Azam FC.
Mechi hiyo ni muhimu kwa beki huyo kucheza kutokana na aina ya
washambuliaji wa Azam FC. Mtanange huo utapigwa Desemba 28, mwaka huu kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Cannavaro ataikosa mechi hiyo kutokana na kadi nyekundu ya moja
kwa moja aliyopewa kwenye mechi ya ligi kuu dhidi ya Kagera Sugar iliyopigwa
kwenye Uwanja wa Kaitaba juzi. Kagera ilishinda 1-0.
Beki huyo, alipewa kadi hiyo baada ya kumpiga kichwa mshambuliaji
wa Kagera Sugar, Rashidi Matalanda.
Kwa mujibu wa kanuni za soka, beki huyo anatarajiwa kukosa mechi
mbili za ligi kuu ambazo ni dhidi ya Mgambo JKT itakayochezwa Jumamosi ijayo na
Azam FC, zote zitachezwa Uwanja wa Taifa, Dar.
Adhabu hiyo, pia itampata kocha msaidizi wa timu hiyo Mbrazili,
Leonardo Neiva ambaye alitolewa kwa kadi nyekundu ya moja kwa moja kwenye
benchi baada ya kuingia uwanjani dakika chache Cannavaro alipopewa kadi.
Beki na kocha huyo wanatarajiwa kurejea uwanjani katika mchezo
dhidi ya Mbeya City utakaopigwa kwenye Uwanja wa Sokoine Januari 3, mwaka huu.
0 COMMENTS:
Post a Comment