MALINZI |
Na Saleh Ally
MARA nyingi ukitoa hoja za msingi na mtu
anayetakiwa kukujibu akawa ameishiwa, basi hufanya mambo mawili. Kwanza ni
kulazimisha watu wakupuuze au kuanza kukuporomoshea matusi na kashfa.
Ukikutana na watu wa namna hiyo hupaswi
kuwaogopa, hupaswi kuwahofia kabisa. Badala yake shikilia msimamo na mwisho
ukweli huwa haushindwi hata kama kutakuwa na juhudi ya kuuchelewesha kufanya
kazi yake.
Mdau mmoja wa soka alihoji, kwa nini Dk Damas
Ndumbaro ndiye autangaze ubadhilifu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) huku
akisema rais wake, Jamal Malinzi amechota mamilioni ya fedha kutoka TBL nje ya
mkataba wao.
Nikamkubusha kauli ya Dk Ndumbaro kuwa,
anamtuhumu Malinzi kwamba ametumia vibaya fedha za mkataba kati ya TFF na TBL,
ndiyo maana anataka kupewa fedha za klabu, kama unakumbuka aliagiza asilimia
tano za udhamini wa klabu 14 kutoka Vodacom na Azam TV zikatwe na kwenda kwenye
maendeleo ya soka.
Hii ni ajabu, inashangaza kuona watu wanakaa
kimya na linaonekana ni jambo dogo kabisa! Kama kweli TFF imetumia fedha
vibaya, tena mamilioni ya fedha ambayo yamepotea kutoka kwenye mkataba wa
TFF-TBL, vipi leo wanataka kuzinyonya klabu?
Nilianza kusimamia hili, wako wapambe wachache
ambao naamini watakuwa wanafaidika na ubadhirifu huo wa fedha ndani ya TFF,
wamekuwa wakiandika meseji za matusi kwangu na kashfa nyingi. Miaka 15 sasa
naelea kwenye mfumo huo wa watu waoga wasiotaka kujibu hoja, wanaangukia kwenye
vitisho.
Iko haja ya kujibu hoja za Dk Ndumbaro ambaye
amezieleza, si kama ambavyo TFF ilizijibu kirahisi ikitaka mwanasheria huyo
apuuzwe. Sasa ripoti iko mikononi mwa Championi na majina ya wahusika na
matumizi mabovu ya fedha yalivyokuwa, yako wazi.
Ripoti hiyo ya ukaguzi iliyofanywa na kampuni
mahiri ya kazi hiyo ambayo ililipwa na TBL inaonyesa madudu makubwa ambayo
yanapaswa kuwekwa hadharani na ikiwezekana Watanzania wengi waipate na kuona
fedha za soka zinavyochezewa na wajanja wachache, wapambe wao huku wakitaka
kujionyesha ni wasafi kwa jamii, kumbe sivyo.
Ukiachana na fedha dola 10,000 (Sh milioni 17)
alizochukua Malinzi, Desemba 24, 2013 ambazo kampuni hiyo ya ukaguzi imeonyesha
hazina maelezo, Malinzi alichukua fedha nyingine tena dola 15,934 (Sh milioni
27).
Kama hiyo haitoshi, Malinzi akalipwa tena dola
69,471 (Sh milioni 118) na dola 63,735 (Sh milioni 108) ndani ya mwezi mmoja
tu, maana yake amechota zaidi ya Sh milioni 270 kwa mujibu wa ripoti hiyo ya
ukaguzi iliyotolewa na Dk Ndumbaro.
Ripoti inaonyesha Malinzi aliikopesha TFF,
lakini haionyeshi lini, wapi aliikopesha au fedha alizokopesha ziliingia kwenye
akaunti moja ya TFF au zilitumika vipi. Ndiyo maana kampuni hiyo ya ukaguzi,
ikaziita unsupported document (nyaraka zisizo na vielelezo).
Achana na hivyo, ndani ya ripoti hiyo kuna
madudu lukuki, mfano ni manunuzi ya magari aina ya Toyota Hiace na ukaguzi
unaonyesha hazipo na hata wakaguzi wa mahesabu hawakuweza kuziona.
Hiace zote mbili zimenunuliwa kwa dola 34,177
(Sh milioni 58), ajabu moja ikalipiwa ushuru wa dola 20,000 (Sh milioni 34),
kitu ambacho kamwe hakiwezi kutokea. Lakini ajabu moja ya gari hizo zinatumia
jina la Juma Sharrif hadi leo, hii ni baada ya wakaguzi kuishia kuonyeshwa kadi
za usajili tu wa magari, lakini zenyewe hawakuziona ng’o.
Ukaguzi huo wa mahesabu ya TFF kwenye mkataba
wa TBL yaliyoisha Mei 8, 2014 yameanika madudu mengi tu yakiwemo yale ya malipo
ya mamilioni ya Kocha Kim Poulsen wakati anavunja mkataba na inaonyesha ni
aghalabu kulipwa dola 90,000 (Sh milioni 153) eti kisa kavunja mkataba!
Au kumfukuza kwake ilikuwa ni sehemu ya
kujitafutia maslahi? Je, TFF inaweza kuuweka mkataba wake hadharani na kusema
kweli ililipa kiasi hicho? Ndiyo, ifanye hivyo.
TFF wasipaniki, huu ndiyo wakati mzuri wa
kujibu hoja ya jambo hili. Sasa kwa wadau wa soka tunaweza tusijali sana
aliyeanzisha au kuyavumbua madudu hayo ni Dk Ndumbaro, badala yake majibu
sahihi kuhusiana na kinachoendelea.
TFF sasa haipaswi kuhama kwenye hoja na kuanza
kudai inachafuliwa au fulani hampendi fulani, badala yake iingie kwenye data na
kueleza wazi kwamba fedha hizo utaratibu wake ukoje na ilikuwa vipi.
Nawakumbusha TFF, najua kuwa watafanya kila
wanaloweza kupambana na kila anayewakosea. Najua haitawasaidia, najua mwisho
watakwama kwa kuwa watapita njia ambazo si sahihi. Lakini mwisho ukweli utapaa
na kuwashinda nguvu.
Hivyo kama wana jibu sahihi kupitia hoja hizo,
basi waweke mambo wazi ili wadau wa soka, Watanzania ambao ndiyo wamiliki wa
TFF wajue. Kumbukeni wote mnaochukia TFF kukosolewa, shirikisho hilo si la
Malinzi au rafiki zake, ni la Watanzania. Walio hapo, wengi wamechaguliwa na
walioajiriwa, pia wanafanya kazi kwa dhamana ya Watanzania.
Hivyo, Watanzania wana haki ya kujua na
niwaahidi, uchunguzi kuhusiana na suala hili, kuendelea kuchimbua na kujua
litaendelea. Hivyo majibu au ufafanuzi kutoka TFF, litakuwa jambo zuri kwa
faida ya soka yetu ambayo tunapigania ikue, wengine wanataka iendeshe maisha
yao na kuwanenepesha.
Kamwe nguvu ya hisia haijawahi kuishinda hoja
kwa kuwa haitoki inabaki kichwani na mwisho inaitwa mawazo lakini anayezungumza
mawazo yake akichanganya uhusiano wa ubongo wake na mdomo vikishirikiana na
macho, anaweza kujenga jambo sahihi linaloeleweka.
Basi TFF, watu wetu, rafiki zetu, kaka na ndugu
zetu, hebu mjibuni Dk Ndumbaro tung’amue ukweli kwa faida ya sisi Watanzania
walalahoi tunaoupenda mpira.
0 COMMENTS:
Post a Comment