November 5, 2014


Na Saleh Ally
MSHAMBULIAJI wa Mtibwa Sugar, Mussa Hassan Mgosi, amesema uoga na kutokuwa na uzoefu ndicho kilisababisha kipa Peter Manyika kufanya makosa na kumpa nafasi, yeye kufunga bao la kusawazisha.


Katika mechi ya Ligi Kuu Bara wikiendi iliyopita kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, Mtibwa Sugar, ilitoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba na kuipa sare ya sita mfululizo timu hiyo yenye makao makuu yake mtaa wa Msimbazi.

Mgosi ndiye alifunga bao hilo la kusawazisha baada ya kipa kinda, Manyika kuukosa mpira wakati akiuwania huku akizongwa na mshambuliaji huyo.

Mgosi anasema baada ya mpira kutangulizwa, wakati anaukimbilia alijua lazima kipa yule angefanya makosa kutokana na sababu mbili kubwa.

“Kwanza nilijua Manyika hana uzoefu, ndiyo mechi ya tatu tu ya ligi anadaka, hivyo kwenda kasi kungemtisha na ingekuwa rahisi sana kutoa nafasi ya kutengeneza kosa.

“Pili nilijua atakuwa ameingia uoga, kama unakumbuka mwanzo tuligongana na akaumia. Hivyo alijua nitamgonga tena, Manyika alikwenda akiwa na mawazo mawili, kwanza kuudaka mpira haraka na kuondoka njiani ili nisimgonge, akaukosa, nikafunga kirahisi,” anasema Mgosi.

“Mshambuliaji unatakiwa kuwa unatisha, unatakiwa kuogopwa na mabeki na kipa, hivyo nilitumia nafasi ya uzoefu wangu na Manyika kutokuwa na uzoefu kufunga bao lile.”

Mgosi alikuwa mshambuliaji tegemeo wa Simba, alitokea Mtibwa Sugar na kujiunga na timu hiyo ya Msimbazi kabla ya kurejea tena Mtibwa Sugar.
Simba:
Kuna tofauti kubwa sana kati ya Simba na Mtibwa Sugar. Hapa ninacheza kwa kujiamini na watu wanaelewa maana ya neno kukosea.

Ukikosea unaelekezwa, unakubali na mnaendelea. Tofauti na Simba kila ukikosea unaambiwa umehujumu.

Kama unakumbuka, Simba ikifungwa nilikuwa natajwa, ikishinda halikadhalika. Naweza kusema nina furaha zaidi hapa Mtibwa Sugar.
Familia:
Familia yangu imebaki Dar es Salaam, iko mbali na wakati mwingine nalazimika kurejea na kukaa nao kwa siku chache kwa kuwa nilizoea kuishi nao.

Wakati mwingine wanakuja Morogoro, mfano katika mechi dhidi ya Simba mke na watoto wangu walikuwa uwanjani.

Baada ya mechi walikuja kuniunga mkono pia kwa furaha ya kufunga bao. Mwanangu Hassan (11), alinifuata moja kwa moja na kunieleza kwamba nilifunga bao zuri lakini akasema lilitokana na dua zao kwa kuwa pale jukwaani walikuwa wananiombea nifanye vizuri.

Simba&Yanga:

Kweli msimu huu nimefunga mabao katika mechi zote mbili za Yanga halafu Simba. Lengo langu si kufunga kwenye mechi hizo, nataka kufunga kila mechi.

Ninapoingia uwanjani nataka kufunga, nikishindwa nataka kusaidia kutoa pasi ya bao au kuisaidia timu kushinda. Kuzifunga timu hizo kwangu lilikuwa ni jambo zuri zaidi na ningependa kuzifunga tena tukikutana lakini napenda kuifunga kila timu tutakayocheza nayo.

Kustaafu:

Siwezi kuzungumzia kustaafu, bado nina nguvu na uwezo wa kucheza upo hivyo bado nina nafasi ya kucheza.

Ninaamini nitacheza miaka minane ijayo au zaidi. Bado nina nafasi kubwa ya kutamba katika soka la Kibongo maana nina uzoefu nalo na ninaliweza.

Mimi ni mzoefu na soka la Bongo, napenda mazoezi na ninaipenda kazi yangu. Hivyo nina uhakika wa kuendelea kufanya vizuri.

Mashabiki:

Mashabiki wa Dar es Salaam nawakumbuka sana, walikuwa wananipenda na wana ushirikiano. Lakini bado ninashukuru, hadi leo nikipita huku na kule bado wanaonyesha ushirikiano, hivyo naamini bado niko nao na wanaukubali mchango wangu.






0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic