Na Saleh Ally
SIMBA imembakiza kiungo wake Jonas Mkude
ambaye imelazimika kumpa kitita cha Sh milioni 60 ili asaini mkataba mpya wa
miaka miwili baada ya ule wa kwanza kuwa umemalizika.
Mkude ni kati ya viungo hodari wanaochipukia
kwa kasi, hakuna ubishi licha ya kuwa ni faida kubwa kwa Simba lakini ni faida
kubwa kwa taifa letu kama ataendelea kuhifadhi kiwango chake na kukiendeleza.
Usajili wa zaidi ya Sh milioni 50, mara nyingi
umekuwa ukifanyika kwa wachezaji wa kigeni, tena kutokea nchi za jirani kama
Kenya, Uganda au Rwanda.
Wachezaji wa nyumbani wengi wao wanaonekana
hawana kiwango cha fedha hizo, lakini hata wa kigeni wanakuwa wanatokea katika
ligi ambazo hazina tofauti au ziko chini ukilinganisha ubora na ule wa Tanzania
Bara!
Fedha ambazo Simba wamelipa kwa Mkude,
zinaweza kuwa somo kubwa kwa wale wanaotaka kujifunza au kuona mbali kwa kuwa ni
mwanzo wa mapinduzi wa kuwaamini wachezaji waliotunzwa, kusimamiwa na
kuendelezwa kwenye klabu za nyumbani.
Kumlipa fedha kama hizo Haruna Niyonzima
(Rwanda), Paul Kiongera (Kenya), Joseph Owingo (Uganda) ilikuwa inaonekana ni
kawaida.
Lakini si kijana kama Mkude na hiyo ilikuwa
imani potofu kwa kuwa mazingira ya kuwakuza vijana wetu yamekuwa mabovu na
hawapewi dira kuwa kujituma, kujitunza na mazingira mazuri ya malezi yanaweza
kuwapa faida kubwa baadaye.
Kwa Sh milioni 60 alizopata Mkude ni hamasa
kubwa katika maisha yake ndani na nje ya soka. Kama atafungua biashara na
atataka iendelee basi lazima atajituma kazini na hapo ndipo atakapofanikiwa.
Naamini hawezi kuwa ‘kilaza’ akabweteka na kupotea kwa kuwa amejitahidi kupanda
daraja hadi kufikia alipo.
Tuwapongeze Simba, wamemlea kama alivyosema
Mkude mwenyewe, lakini mwisho wamempa thamani na yeye anaingia kwenye changamoto
ya deni la kupambana kwa ajili ya klabu na yeye pia.
Faida
kwa taifa:
Simba wapewe pongezi tena kwa kuendelea
kutengeneza watu ambao ni faida kwa taifa letu kwa kuwa kila anavyoimarika,
Mkude atakuwa tegemeo la taifa na akifanya vizuri zaidi na kusonga mbele
kimataifa, ataingiza fedha nyingi zaidi na kuwa mfano kwa vijana wengine
wanaohitaji hamasa ya kuamini mambo yanawezekana, nao wakajituma.
Wapo vijana ambao hawaamini kuwa Mtanzania
anaweza kufanya vizuri nje, kwa mwendo wa Mkude akiendelea kujituma na kuwa na
malengo, ana kila sababu ya kufanikiwa na kucheza nje ya Tanzania, hata Ulaya.
Hiyo itakuwa ni changamoto kwa vijana na njia sahihi ya kuamini kuwa
inawezekana.
Fedha
nyumbani:
Unaweza kusema ubaguzi lakini hakika ni furaha
kumuona Mtanzania mwenzako anachukua mamilioni kutoka kwenye taasisi ya
nyumbani na hasa kutokana na ubora wa kazi yake.
Bora apewe Mkude kuliko angepewa mwingine
yeyote wa taifa la jirani. Tunapigania vijana wenzetu, wadogo zetu wapate
ajira. Mtanzania anastahili kupata fedha za Tanzania, ndiyo maana unaweza
kusema fedha alizopewa kiungo huyo, zimebaki nyumbani.
Kwa malipo ya Sh milioni 60 kwa Mkude, tayari
ni changamoto kwa vijana wengi wanaocheza kwenye timu za vijana kama wakijituma
na kukubali kuumia sasa, basi mafanikio hayapo mbali nao.
Hisia
za kusonga:
Vijana hao wana kila sababu sasa ya kuamini
kwamba wana uwezo wa kusonga lakini haiwezi kuwa rahisi. Hata Mkude alipofikia
hapo haiwezekani alikuwa akilala na kuzembea mazoezi halafu akapata alichopata
kutoka Simba.
Angalia kiungo Pierre Kwizera, leo hata kuna
watu wameanza kuamini Mrundi huyo hana lolote, lakini ukweli kijana huyo ni
kati ya viungo bora kabisa katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, siku
itafika hilo litadhihirika.
Kutokana na umahiri wa Mkude, watu wameanza
kuamini hafai. Vizuri kujifunza kwamba Mtanzania anaweza kuwa changamoto kwa
mgeni na ikiwezekana aanze yeye na mgeni afuatie.
Kuwahofia Wakenya, Waganda, Wanyarwanda si
sahihi. Tujiulize wanatokea kwenye ligi za namna gani, huko kwao wana nini
kipya hasa? Wanachoweza na tusichoweza wakati hatuna tofauti ni nini?
Deni alilonalo Mkude kwa Simba ni kuonyesha
walichofanya kwake ni sahihi, awaonyeshe Watanzania thamani aliyopewa Msimbazi
hawakukosea lakini atoe somo kwa wadogo zaidi yake kuwa hata wao wanaweza kwa
kuwa yeye amefanya hivyo. Akiboronga, basi atavunja kila kitu kuwa kumbe
Watanzania hawastahili kulipwa fedha nyingi na watoto hawana sababu ya
kujituma, maana hata wafanyeje, watafeli tu!
0 COMMENTS:
Post a Comment