Baba wa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Simon Msuva ambaye ni Happygod
Msuva ameeleza kushangazwa na taarifa kuwa Simba inataka kumsajili mtoto wake.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakari Hans Poppe,
alinukuliwa akisema kuwa, baada ya kumsainisha mkataba mpya kiungo wao, Jonas
Mkude, sasa wanamhitaji Msuva.
Hans Poppe alisema kuwa, dau la kuanzia kumsajili Msuva walilotenga
ni shilingi laki tano, hivyo wanajipanga kutuma maombi Yanga.
Happygod amesema aliwahi kumpeleka
mwanaye kwenye timu hiyo lakini walimwekea pozi.
“Unakumbuka kipindi kile Simon alikuwa akizomewa mara kwa mara na
mashabiki wa Yanga? Basi nikaamua kwenda kuzungumza na aliyekuwa Mwenyekiti wa
Simba, Ismail Rage na makamu wake, Geofrey Nyange ‘Kaburu’, walitoa majibu ya
dharau kila nilipowapigia simu.
“Yanga imechangia kumlea Simon mpaka hapo alipo baada ya kuanzia
katika Academy ya Azam FC, nilipoona hakuna maendeleo wakati akiwa chini ya Idd
Cheche na Kali Ongala, nikampeleka Moro United ndipo Seif Magari akamchukua na
kumpeleka Yanga.
“Hivyo kama Simba wanamtaka, wawafuate Yanga kwa kuwa bado ana
mkataba, lakini ukweli ni kuwa ninawashangaa hao Simba wanamtaka Simon kwa
kipi!” alisema Happygod.
0 COMMENTS:
Post a Comment