MGANDA, Emmanuel Okwi
aliwatoa machozi ya furaha mashabiki wa Simba, wakati akiikomboa timu yake
kuondoa ‘gundu’ la sare lililowaganda tangu kufunguliwa kwa msimu huu, wakati
akiipatia ushindi wa kwanza katika mchezo wa saba wa Ligi Kuu Bara dhidi ya
Ruvu Shooting.
Licha ya kuonekana ulikuwa ni
ushindi kiduchu, lakini ilikuwa ni neema kubwa kwa mashabiki, wachezaji,
viongozi na benchi la ufundi la timu hiyo, kutokana na presha kubwa waliokuwa
nayo kufuatia kuwa na mwenendo mbovu katika ligi hiyo.
Kwa kifupi, gundu la sare
lilimchanganya kila mmoja ndani na nje ya klabu hiyo, huku wakijiuliza chanzo
cha tatizo hilo. Si mchezaji, kocha wala bosi ambaye angekupa majibu sahihi
kuhusu mzimu wa sare. Ni kitendawili kigumu sana.
Simba imekwenda katika
mapumziko mafupi ikiwa katika nafasi ya saba na pointi tisa, ikiwa na mabao ya
kufunga saba, ya kufungwa sita! Kinachouma zaidi katika sare zote sita, achilia
mechi dhidi ya Yanga ambayo zilitoka suluhu, Simba ndiyo ilikuwa ikianza
kufunga, kisha wapinzani wanasawazisha. Lakini pamoja na gundu la sare, inabaki
kuwa timu ambayo mpaka sasa haijapoteza mchezo, ikiungana na vinara wa ligi
hiyo, Mtibwa Sugar.
Mahasimu wao Yanga wamekula
kichapo mara mbili, mabingwa watetezi, Azam nao wameonjeshwa shuburi mara mbili.
Kocha mkuu wa timu hiyo, Mzambia, Patrick Phiri kutaka kujua
kiufundi sababu za kushindwa kulinda ushindi wake, mikakati yake kuelekea mechi zijazo, na kubainisha tetesi
zinazovuma kuhusu ‘ugali wake kuingiwa mchanga’ pale Msimbazi.
Mechi saba zimempa mwanga
gani?
“Yaah! Naweza kusema mechi
saba zimenipa mwanga fulani, kikosi chetu kilikuwa kimeanza kucheza vizuri na
kuwa kikosi cha ushindani baada ya kutatua matatizo ya hapa na pale ya
kiufundi.
Lakini changamoto kubwa ilikuwa
ni kushindwa kufunga mabao mengi, wastani tulifanikisha kufunga bao moja kila
mechi, huu siyo ushindi kwa timu kubwa kama Simba, timu kubwa inahitaji kufunga
walau kuanzia mabao matatu ukiwa nyumbani na ugenini kwa ushindi wa bao moja
unatosha.
“Lakini kilichotuumiza
zaidi sote ni kwamba kila mchezo tulikuwa wa kwanza kupata bao, lakini
tunashindwa kuulinda. Ni matatizo
ambayo tunatakiwa kuyapatia utatuzi kipindi hiki (usajili, dirisha
dogo).
Tatizo nini hasa kushindwa
kulinda ushindi?
“Kimsingi ni matokeo ya
timu kucheza ikiwa na presha, utaona mechi mbili za mwanzo kikosi kilicheza
vizuri lakini baadaye kilianza kucheza kikiwa na presha kutokana na matokeo ya
sare za awali, lakini baada ya kuwahimiza, utaona katika mechi mbili za mwisho
walicheza vizuri sana na kupata ushindi mchezo wa mwisho. Ninafikiri ulikuwa ni mwanzo wa ushindi na sasa
Simba imekuwa ya kiushindani na itashinda zaidi.
Makocha wengine wamekwenda
likizo, je, nini mipango yako?
“Yaah! Hata mimi niko
njiani kuondoka, nafikiri wiki ijayo kama nitakuwa nimemaliza ‘ishu’
zinazonikabili, basi nitakwenda. Siwezi kuondoka na kuacha lundo la matatizo,
maana utakuwa ni mzigo wangu hata nikirejea, ikizingatiwa ni kipindi
ambacho tutakuwa kwenye maandalizi
ya mchezo dhidi ya Yanga (mechi ya Mtani Jembe).
Ni safu gani ambayo
inahitaji kurekebishwa?
“Ni safu ya mbele, maana
kama nilivyokwambia kuwa kiwastani tumekuwa tukipata mabao kidogo sana, nadhani
kama kuna haja ya ‘kui-shape’.
“Siwezi kusema ni nani anatufaa
au hafai, hilo naomba libaki kwenye ripoti yangu ambayo nimewakabidhi mabosi wangu.
Tetesi za kutemwa kwa
Kiemba, Chanongo, unadhani Simba itadhurika kiasi gani?
“Binafsi naweza kusema ni
moja ya pengo ndani ya Simba, maana wachezaji wote wamekuwa wakipata nafasi.
Sijawahi kuingia katika matatizo na mmoja wao hata ungewauliza, kifupi ninaweza
kusema suala lao libaki kiuongozi zaidi, ila siyo kwangu.
Mkude, Okwi ndiyo wanaweza ligi ya kimataifa
Phiri ni miongoni mwa
makocha ‘profeshino’, akiwa na rekodi ya kutwaa ubingwa pasipo kupoteza mchezo
wowote, msimu wa 2009/10 na kutwaa tuzo ya kocha bora wa Ligi Kuu Bara (VPL)
mara mbili, anasema Jonas Mkude na Emmanuel Okwi ndio amewaona wanaweza kucheza
soka la nje mpaka sasa.
“Kweli tayari nimeona kuna
wachezaji wanaoweza kucheza soka la kimataifa, Mkude ni mmoja wa wachezaji
hatari katika safu ya kiungo kwa sasa. Sioni kama anaweza kushindwa kucheza
ligi ya nje.
Changamoto pekee anatakiwa
kucheza mechi nyingi ndani na nje ya ligi ya nyumbani, ili aweze kutathiminiwa
zaidi, lakini kwa ‘passion’ aliyonayo anafaa kucheza nje. Pia Okwi anafaa na
ndiyo maana amecheza sehemu mbalimbali.
Tetesi ya kuachwa na Simba
“Binafsi suala la
kuachishwa kibarua ni jambo la kawaida kwa kocha yeyote, kwenye soka kuna msemo
kuwa ‘kocha anaajiriwa ili afukuzwe’. Ni kawaida, lakini siwezi kuweka mawazo
hayo kwa sasa, maana bado nimepewa kazi ya kupanga mikakati ya timu katika
mechi zijazo.
“Hata kama itatokea,
yatakuwa ni maamuzi ya mabosi ambao watakuwa wameona timu yao haifanyi vema na
tatizo ni kocha, hivyo wana ruhusa ya kumbadilisha.
Je, iwapo Simba
watakuhitaji, utarejea?
“Siwezi kujitabiria mbaya,
maana bado niko Simba na kama tetesi za kuachishwa kazi zipo, basi zikitokea
ndipo ninaweza kuongelea msimamo wangu, lakini kwa sasa ni kama najitabiria
mabaya.
Vipi Yanga wakikuhitaji,
upo tayari kwenda?
(Anacheka)… “Mhh! Ni ngumu sana
kujiunga na timu kama Yanga, ujue nina mapenzi makubwa na Simba na marafiki
zangu wote wapo Simba. Halafu hizi ni timu kubwa zenye presha, kwa hiyo
unapokuwa upande mmoja unatakiwa kuwa makini na sehemu hiyo. Unatakiwa uende
sehemu ambayo unaamini utapata amani muda wote.
Sisemi Yanga wana presha,
hapana, asili ya mpira wa Tanzania ulivyo, ni presha tu, mfano kama mimi
nitakapokuwa Yanga wakati Simba ni kama nyumbani unafikiri ni nini kitatokea.
Presha tupu mwishowe unajikuta unaharibu kazi.
Akunwa na Cannavaro, Msuva,
Yondani
“Yanga ni timu kubwa ina wachezaji wazuri na
kuna baadhi ya wachezaji wao kweli nimevutiwa nao. Kuna Yondani (Kelvin),
Cannavaro (Nadir) Msuva (Simon) na hata Ngassa (Mrisho) kiukweli ni wachezaji
wazuri. Pia wale Wabrazili kwangu nilipendezewa nao.
Kaseja unadhani bado ana nafasi Simba ya sasa?
“Yaah.. hakuna kipa bora
kama Kaseja (Juma), lakini sijajua nini kilichomuondoa Simba na kwenda kujiunga Yanga.
“Kaseja naweza kusema bado
ana nafasi hata ya kuwa namba moja. Ni kipa mzuri sana na mzoefu kwenye soka la Tanzania, cha msingi ni
changamoto ya kuwania nafasi mbele ya makipa waliopo, Ivo Mapunda, Hussein
Shariff ‘Casillas’ na Peter Manyika.
SOURCE: CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment