JAMES MSUVA AKIWA MAZOEZINI SIMBA. |
Baada ya kumkosa kiungo mshambuliaji wa Yanga,
Simon Msuva, Klabu ya Simba imehamia kwa mdogo wake, James Msuva katika usajili
wa dirisha dogo linalofunguliwa leo.
Simba kwa kupitia Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya timu hiyo, Zacharia Hans Pope, ilitangaza kutoa kiasi chochote cha
fedha kwa ajili ya kumsajili kiungo huyo mwenye kasi katika kikosi hicho.
Usajili wa dirisha dogo unatarajiwa
kufunguliwa leo Jumamosi na kufungwa Desemba 15, mwaka huu ukishirikisha klabu
mbalimbali za ligi kuu.
Kwa mujibu wa chanzo cha habari kutoka ndani
ya uongozi wa timu hiyo, wamefikia hatua ya kumsajili kiungo huyo baada ya
benchi la ufundi la timu hiyo ambalo lipo chini ya Mzambia, Patrick Phiri na
Selemani Matola kuridhishwa na kiwango chake.
Chanzo hicho kilisema, Phiri ameridhishwa na
kiwango kikubwa cha kiungo huyo mwenye kasi anayecheza namba saba kama
anayocheza kaka yake Simon baada ya kumuona kwenye mazoezi ya timu ya vijana ya
U-20.
“Uongozi umepanga kukutana na mdogo wake Msuva
(James) kwa ajili ya kuanza mazungumzo ya timu hiyo kwa ajili ya kumsajili
katika usajili wa dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa kesho (leo).
“James yupo anaichezea timu yetu ya vijana ya
U-20, akiwa hana mkataba wa kuichezea Simba, hivyo tumefikia hatua ya kumsajili
kwa mkataba na kumpandisha kwenye timu ya wakubwa, hivyo ni baada ya
kuridhishwa na kiwango chake ndani ya uwanja.
“Kocha mwenyewe leo (jana) amemuona akiwa anacheza
katika kikosi cha vijana cha U-20, amevutiwa naye kutokana na uwezo mkubwa aliokuwa
anauonyesha, hivyo upo uwezekano mkubwa wa kumsajili,” kilisema chanzo hicho.
Alipoulizwa Phiri kuhusiana na kiwango cha
James, alisema: “Ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa wa kucheza, ukiangalia
anaweza kukaba, kontroo yake nzuri na anapiga krosi safi, kuhusu kumsajili siwezi
kuzungumza hivi sasa.”
0 COMMENTS:
Post a Comment