TULLY (KULIA) AKIZUNGUMZA NA KOCHA MKUU WA ORLANDO PIRATES WAKATI SIMBA ILIPOKUWA IMEWEKA KAMBI NCHINI AFRIKA KUSINI. |
MOJA ya mafunzo niliyopata ni kuhusiana na
suala la kuripoti mechi moja kwa moja wakati ikiendelea. Si kwa kuzungumza,
badala yake ni kwa kuandika.
Mafunzo hayo niliyopata kutoka kwa wataalamu wa
Shirika la Habari la Ufaransa (AFP), yalisaidia kubadilisha mwelekeo na hisia,
au mazoea ya kile ambacho nilijifunza awali na haraka nikang’amua kuwa dunia
inakwenda kwa kasi kubwa, ndiyo maana natamani kujifunza zaidi.
Moja ya malalamiko makubwa yaliyowahi kutolewa
na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakati wa uongozi wa Leodegar Tenga ni
kwamba wasemaji wamekuwa hawazungumzi mambo sahihi wanayotakiwa kuzungumza.
Kwamba utakuta msemaji wa timu anazungumza kama
mwalimu wa timu. Si ajabu ukamsikia anasema watacheza 4-4-2 kwa kuwa wameamua
kuweka washambuliaji mbele, na blah blah au vinginevyo.
Pia unaweza kumsikia msemaji akitumia muda
mwingi akizungumzia mwalimu au mwamuzi wa mechi fulani akionyesha kutovutiwa na
kilichotokea katika mchezo. Uongozi wa Tenga, ukasema haikuwa sahihi.
Inawezekana itakuwa vigumu kuamini kwa kuwa
tunahitaji kujifunza zaidi, ndiyo kabla sijapata mafunzo ya AFP, kuna mambo
niliyachukulia tofauti hadi nilipojifunza na kugundua nilikuwa nyuma ya wakati.
Huenda ni wakati mwingine wa wasemaji kuendelea
kujifunza ingawa nimekuwa nikishangazwa na kufurahishwa na mmoja wa Mjumbe wa
Kamati ya Utendaji ya Simba, Said Tully.
Nafahamiana na Tully takribani miaka kumi
iliyopita, wakati akiwa mchezaji, alipoondoka nchini na baadaye kurejea. Tumekutana
mara kadhaa na kuzungumza mambo ya kawaida au ya mpira.
Kinachonivutia ni namna ambavyo amekuwa
akizungumza kwenye vyombo vya habari, anavyojibu na hasa mpangilio wa majibu
kutokana na swali na kamwe hauwezi kusikia kaingia idara si yake.
Tully amekuwa mwepesi kung’amua wapi muuliza
maswali anampeleka, kipi sahihi katika wakati mwafaka na upi mpaka wake wa
kujibu maswali. Yeye si msemaji wa Simba.
Unakumbuka wakati fulani uongozi wa Simba
ulisema umewasimamisha viongozi kuzungumza, lakini ilionekana hakuwa Tully kwa
kuwa kabla hakuwa amemshambulia au kusema maneno yasiyofaa kwa mchezaji.
Inawezekana kabisa Tully akawa hajasomea
masuala ya uzungumzaji, yaani si mwandishi wa habari. Lakini utulivu wake,
wepesi wa kugundua mipango yake mwisho ni wapi inamsaidia kuweza kuzungumza
sahihi na kutoa ufafanuzi sahihi kulingana na swali.
Kila mmoja anaweza kuwa na mtazamo wake,
nimetumia zaidi ya wiki tatu kumfuatilia Tully nikitaka kujua anakopita kwa
majibu kwa kila swali analoulizwa. Waingereza wanasema ‘perfect’. Yaani anapita
katika mistari sahihi na hakuna maswali.
Huenda siku moja akakosea kwa kuwa naye ni
binadamu lakini ukweli anachokifanya sasa kinaweza kuwa mfano kwa wasemaji
wengine ambao sisemi wanafanya vibaya ila wanaweza kujinoa kupitia kwake baadhi
ya mambo kwa nia ya kujiimarisha zaidi kuwa wapite njia ipi iliyo sahihi.
Tully kamwe hajawahi kuchanganywa na maswali ya
jamaa hapo chini (Maulid Kitenge) wala mwenzake. Hajawahi kujibu kwa
kushambulia chombo cha habari, mchezaji au mtu fulani, badala yake anakwenda
kwenye hoja.
Si wasemaji wa timu tu wanaweza kujifunza. Hata
watu wazima, viongozi wa Yanga, Simba pia nao wanaweza kujifunza kupitia Tully
kwamba anazungumza kwa kujibu hoja kutokana na anachokielewa, si kutunga
hadithi na swali linajibiwa kwa lawama au kushambulia tu. Ili mradi mahojiano
yanakamilishwa na lawama au mashambulizi.
Tully hawezi kujua kila kitu kama mimi na wewe,
lakini ameonyesha kwamba bado kuzungumza kwa kufuata weledi kunaweza kufanikiwa
kwa umakini tu wa mtu. Hivyo msikilizeni, ubora wake uwe fundisho, machache
anayokosea, pia yatumike kama mafunzo.
0 COMMENTS:
Post a Comment