Na Saleh Ally
MIAKA mitano iliyopita, nilifanya mahojiano ya ana kwa
ana na kiungo Gnegneri Yaya Toure akaniambia jambo ambalo naweza kusema
limetokea.
Tukiwa Lilongwe nchini Malawi, Yaya aliniambia anataka
kucheza mechi zaidi ya 100 katika kikosi chake cha taifa cha Ivory Coast.
Lengo lake ni kuwa mmoja wa wachezaji wenye mafanikio
zaidi Ivory Coast na baadaye Afrika. Sasa yote ameyapata na bado anaendelea
kupambana.
Wakati anajibu, niliona ni tofauti kwa kuwa kwanza
nilidhani atazungumzia Barcelona aliyokuwa anaichezea wakati huo. Yaya alikuwa
na malengo timu ya taifa, nilipotaka kujua kwa nini ilikuwa ni timu ya taifa na
si Barca, jibu lilikuwa hivi:
“Hauwezi kupata mafanikio katika timu ya taifa kama
haujaanzia katika klabu. Najua nitapambana na kufanikiwa, iwe Barcelona au la,
lakini timu ya taifa ni kipimo cha juu cha ubora, pia ni raha kwa kuwa
unakitumikia kitu kilicho ndani ya moyo na maisha yako.”
Timu ya taifa ni maisha yako, hiki ndicho anachoamini Yaya.
Kilichonikumbusha kuandika makala haya ni baada ya kuona amefanikiwa kuichezea
Ivory Coast ‘The Elephants’ mechi 100.
Ameichezea mechi ya 100 huku mambo muhimu mawili
yakitokea. Kwanza alikuwa ndiye nahodha, pili Ivory Coast ndiyo ilikuwa inafuzu
kucheza fainali za Kombe la Mataifa Afrika, usisahau, Yaya ndiye mchezaji bora
Afrika na mchezaji anayeonekana kuwa na mafanikio makubwa zaidi.
Rekodi zinaweza kuwa mwongozo wa mafanikio katika soka,
kama umefunga mabao mangapi, umecheza mechi ngapi au umezisaidia timu kubeba
makombe mangapi?
Yaya anaamini timu ya taifa ndiyo inayotoa majibu ya
mafanikio yako. Kunaweza kukawa na upungufu kidogo katika hilo lakini hakuna
ubishi tena kwamba mafanikio ya timu ya taifa ni kutoka moyoni.
Hivyo utakuwa unajituma kwa nguvu kwenye klabu ili
uteuliwe kwenye kikosi cha timu ya taifa. Ukipata nafasi utaongeza juhudi ili
ulete mafanikio. Sasa jiulize, mchezaji kama Yaya, atafeli vipi?
Nyumbani tuna wachezaji bora kutokana na uwezo wao. Wapo
walioichezea Taifa Stars kwa miaka kadhaa sasa. Je, wanawaza kama Yaya?
Ungeweza kusema Wayne Rooney amefikisha mechi 100 na
England akiwa na miaka 29, tofauti na Yaya mwenye 31, halafu ukatumia kigezo
cha ubora wa mazingira ya Ulaya.
Toure katokea Afrika, kwenye mazingira ambayo huenda ni
magumu kuliko Tanzania. Hivyo hakuna cha kukwepa na ndiyo maana najiuliza
wachezaji wakongwe kama Amri Kiemba, Mrisho Ngassa au makinda kama Shomari
Kapombe, Simon Msuva wamewahi kuwaza kuhusiana na suala la moyo wa uzalendo
kama anavyofikiria Yaya kupitia timu ya taifa?
Wachezaji wengine wote wa hapa nyumbani Tanzania wanajua
timu ya taifa ni sehemu kubwa ya mafanikio na ndiyo kipimo cha mafanikio kama
anavyofikiria Toure ambaye sasa amekuwa mchezaji bora Afrika, pia ameisaidia
timu yake kushiriki Kombe la Mataifa Afrika na Kombe la Dunia!
Hata nikiuliza hizo rekodi za wamecheza mechi ngapi
wakiwa na timu ya taifa, itakuwa kazi kubwa kwa wachezaji wetu wa Shirikisho la
Soka Tanzania (TFF) wanaotakiwa kuhifadhi rekodi hizo.
Tusiache mambo haya ya kina Yaya yakapita tu kama
kimbunga, tujifunze kwa kuwa hakuna cha kukwepa kwa kuwa wamezaliwa na kukulia
Afrika. Hakuna ujanja, lazima mkubali, mna kitu cha kufanya.
0 COMMENTS:
Post a Comment