BAADA ya kucheza mechi sita, ikatoka sare
sita, ikafunga mabao sita na kufunga sita, Simba imebadili gia katika mechi ya
saba.
Simba imeshinda mechi yake ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa kuwatwanga Ruvu Shooting kwa kuichapa bao 1-0.
Bao pekee la Simba jana limefungwa na
Emmanuel Okwi ambalo ni la tatu kwake msimu huu. Mabao mawili aliyofunga
mwanzo, yote yalirejeshwa. Jana, likang’ang’ania.
Ushindi wa Simba unaweza kuwa hatua mpya ya
kuwabadilisha wapenda soka ambao walianza kuamini eti ushirikina au ‘laana’
inaweza kufanya kazi timu ikashindwa kufunga mabao.
Taarifa zilizokuwa zinasambazwa na kupewa
nguvu eti kwa kuwa uongozi wa Simba ulikuwa umewasimamisha wanachama
waliokwenda mahakamani, basi ndiyo maana ilicheza mechi sita na zote ikatoka
sare.
Tena ikaelezwa kwamba Ukawa wamesema Simba
itacheza hadi mechi saba zote itatoka sare na mambo yanaweza kubadilika pale
uongozi utakapokubali kukaa mezani na Ukawa na kumalizana nao.
Haya ni kati ya mambo ya ajabu kabisa ambayo
hayapaswi hata kutamkwa kwenye mchezo wa soka na watu wanaoamini vitu kama
hivyo wanapaswa kusaidiwa.
Mchezo wa soka unapendwa na wengi kutokana
na kuwa na burudani za kila aina. Sare za Simba zilikuwa ni sehemu ya burudani
lakini kiufundi, kikosi cha Msimbazi hakikuwa kimekaa sawa.
Pamoja na ushindi wa kwanza, ukiangalia bado
kuna marekebisho yanatakiwa kufanyika na si suala la Ukawa wala laana.
Mashabiki na wadau wa soka hasa kwa wale
waliokuwa wanaamini, wanapaswa kubadilika kuanzia sasa na kuamini soka ni
maandalizi ya kutosha, benchi bora la ufundi na ushirikiano kwa pamoja.
Sidhani pia kama ni sahihi kuwatisha
viongozi wanaoona kuna matatizo kuwa wasiyafanyie kazi. Wale wanachama
walikwenda mahakamani, wanajua katika soka hilo ni tatizo, kuwachukulia hatua
watukutu ni sahihi na inapendeza wao wakiomba msamaha na si uongozi eti
uwafuate.
Taarifa imeelezwa kuna wazee wa Simba hawana
furaha, ndiyo maana pia Simba ilikuwa haishindi. Haya ni maneno ya kwenye chai
pia, hayapaswi kupewa nafasi hata kidogo kwa watu wanaokwenda kwenye dunia ya
sayansi na teknolojia.
Kama kuna tatizo, basi wazee walishughulikie
kiutu uzima na si kuizuia Simba kushinda, kama ingekuwa kweli. Ukawa haikuwa na
uwezo wa kuizuia Simba kushinda.
Uongozi wa Evans Aveva hauwezi ukawa
umepatia kila jambo hadi sasa. Lakini unaweza kupongezwa kwa mazuri uliyofanya,
mojawapo ni hili la kugoma kukutana na Ukawa na kuelekeza nguvu nyingi katika
kutatua matatizo ya timu, hilo ndiyo ya msingi na sasa ukweli umethibitika.
Kuna swali lilikuwa linaulizwa na baadhi ya
mashabiki wa soka, kwamba “Ukawa wanacheza namba ngapi uwanjani?”
Jibu sahihi limepatikana na wale waliotaka
kutumia sare za Simba kama sehemu ya kujinufaisha, sasa biashara imekwisha,
turuki kwenye ukweli na kuuangalia mpira kitaalamu badala ya kufanya mambo kwa
kubabaisha.
Jambo moja ambalo ninalipiga ni Ukawa
kufanyiwa vurugu. Sidhani kama ni jambo zuri kwa kuwa wale wanaendelea kubaki
kama Wanasimba. Kama watakuwa na hisia tofauti, haiwezi kuwageuza na kuondoka
kwenye klabu hiyo.
Hivyo kama ni wakati wa kurudisha umoja,
sasa inawezekana na litakuwa jambo jema kama Ukawa ndiyo watautafuta uongozi
halafu wazungumze na kushirikiana na kuijenga Simba moja ambayo kama kuna jambo
limetokea basi linaweza kurekebishwa pamoja.
0 COMMENTS:
Post a Comment