WIKI iliyopita niliandika kuelezea suala la
wachezaji wanaokwenda kupumzika baada ya Ligi Kuu Tanzania Bara kusimama kwa
muda.
Ligi itaanza mwishoni mwa Desemba, lakini
wachezaji watakuwa wamerejea katika maandalizi mapema kidogo hasa wale wa Yanga
na Simba kwa kuwa wana mechi ya kirafiki ya Nani Mtani Jembe.
Wengine kama Azam FC na Yanga pia, watakuwa
wanajiandaa na michuano ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho. Hivyo maandalizi
yao yatakuwa tofauti kidogo na timu nyingine zitakazosubiri ligi kuanza.
Maana yake idadi kubwa ya wachezaji kutoka
katika timu 11 za ligi watakuwa kwenye mapumziko marefu ukilinganisha na wale
wa timu tatu za Yanga, Simba na Azam FC.
Nilieleza namna ambavyo wachezaji wanaweza
kupumzika lakini wakajitunza, wakatambua kwamba watakaporejea kwenye ligi
ushindani utakuwa ni mkubwa zaidi ukilinganisha na mechi saba walizokuwa
wameishacheza.
Leo nakumbushia zaidi, kwa wale waliopata
nafasi ya kuiona video ya kiungo Andrey Coutinho akijifua kwao nchini Brazil,
sasa watakubaliana nami kuwa kuna jambo ambalo wachezaji wa hapa nyumbani
wanatakiwa kufanya.
Katika video hiyo iliyovuja sehemu mbalimbali,
Coutinho anayekipiga Yanga, yuko ‘bize’ akipambana kwa mazoezi makali chini ya
kocha ambaye jina lake halikutambulika mara moja.
Coutinho anafanya mazoezi makali ya aina
tofauti akiwa katika usimamizi huo wa uhakika kutoka kwa kocha huyo. Kuonyesha
kweli kiungo huyo amepania, anafuata kila kitu kwa umakini mkubwa huku akiwa na
juhudi ya juu.
Coutinho amejifanyia tathmini baada ya kuuvaa
mziki wa Ligi Kuu Bara, amegundua kasoro zake, aliporejea kwao Brazil,
alichokifanya ni kuanza kuyafanyia kazi matatizo yake.
Moja ya matatizo hayo ni nguvu, kwani
alionyesha uwezo mzuri lakini akashindwa kupambana vilivyo. Mazoezi
anayoyafanya akiwa gym chini ya kocha huyo maalum ni sehemu ya kujitambua. Anayafanyia
kazi makosa aliyoyaona baada ya kucheza mechi za mwanzo za ligi kuu.
Kutokana na uwezo alionao, Coutinho anaamini
kama atazifanyia kazi kasoro zake, basi ana uhakika wa kuwa na kiwango cha juu
zaidi, awe tishio, aisaidie Yanga na ikiwezekana alipwe juu zaidi au auzwe
kokote kule, ghali zaidi.
Wachezaji wangapi wa Yanga wanafanya kama
Coutinho? Wachezaji wangapi wazalendo kutoka Simba, Azam FC, Mtibwa Sugar,
Polisi Moro, Stand United, Mbeya City na kwingine wanafanya kama anavyofanya
Mbrazil huyo?
Kweli ni muda wa mapumziko, lakini yeye
ameamua kuutumia vizuri kufanya marekebisho kwa ajili ya kutafuta ubora.
Inawezekana wengi wa wachezaji wazalendo wamerejea vijijini au mikoani
walikozaliwa au kukulia kwenda kuwatembelea wazazi na hawafanyi lolote kujiweka
fiti.
Achana na kufanya mazoezi kujiweka fiti,
lakini inawezekana kabisa hakuna anayefanya jitihada ya alichokosa wakati wa
mechi saba za ligi zilizopita, badala yake wanaamini wamerogwa na huenda wako ‘bize’
na waganga wa kienyeji.
Tumeficha sana kuhusiana na masuala ya
ushirikina, huu sasa ndiyo wakati mzuri wa kuweka mambo hadharani kwamba hii
imezidi. Uchawi wa mpira ni mazoezi, mipango na juhudi. Si kwenda kwa waganga.
Huwezi ukasema Brazil hakuna waganga wa
kienyeji, lakini Coutinho ameamua kuingia gym kwa kuwa anajua umuhimu wake.
Achaneni na mambo ya hisia, badala yake vitendo na jitihada ziwe dira ya
kuwapeleka kwenye mafanikio.
Coutinho hajafikisha hata nusu msimu, ameanza
kurekebisha aliyoona amekosea. Wa kwetu hapa mnafanya nini? Hata kama
itawaudhi, tafadhali mnaweza kuangalia mazuri na kuyafanyia kazi.
0 COMMENTS:
Post a Comment