Na
Saleh Ally
WAKATI
anamfunga kipa Juma Kaseja wa Yanga katika mechi ya kwanza ya Nani Mtani Jembe,
kiungo wa Simba, Awadhi Juma alikuwa anacheza namba 10.
Kocha
Zdravko Logarusic alimuamini Juma kucheza namba 10, lakini aliwahi kumpa nafasi
ya kucheza namba sita au nane.
Raia
huyo wa Croatia alijulikana kwa ukorofi, lakini hakutaka mchezo kazini. Wakati
fulani aliwahi kusikika akisema, kama atafukuza wachezaji wote kikosini, basi angebaki
na Awadhi.
Wakati
anamfunga kipa Deogratius Munishi ‘Dida’ wa Yanga katika mechi ya pili ya Nani
Mtani Jembe, Jumamosi iliyopita, Awadhi alikuwa anacheza kiungo mchezeshaji,
yaani namba nane.
Baada
ya ujio wa Patrick Phiri kutokea Zambia, wapo waliodhani nafasi ya Awadhi isingekuwepo
tena lakini kiungo huyo anayetokea Tanzania Visiwani amezidi kuonyesha ni
mchezaji wa aina yake.
Wakati
akiwa Mtibwa Sugar, zaidi walimtegemea kucheza kama kiungo mkabaji, pia wakati
mwingine kama namba saba au kiungo mchezeshaji.
Ameendelea
kuonyesha kuwa ndiye kiraka bora zaidi katika kipindi hiki kwa maana ya kuvuka
wigo wa namba ipi acheze kwani akiwa Simba amewahi kucheza kama beki wa kulia,
namba saba.
Hadi
sasa, rekodi zinaonyesha Juma ndiye mchezaji pekee aliyecheza vizuri zaidi
katika mechi mbili za Nani Mtani Jembe.
Ndiye
mchezaji pekee wa Simba na hata Yanga aliyefunga mabao katika mechi zote mbili
za kirafiki za bonanza la Nani Mtani Jembe.
Katika
timu kumekuwa na wachezaji ambao nyota zao si kali sana hata kama wanafanya
mambo makubwa, mfano mzuri kwa Yanga ni mshambuliaji Justin Mtekere (marehemu).
Alikuwa akifunga karibu kila mechi, lakini hakuwa maarufu sana kama wasiofunga.
Awadhi
si maarufu kama wachezaji wengine wa Simba ambao huenda wana uwezo wa kucheza
nafasi moja tu uwanjani.
Kiungo
huyo ana uwezo wa kucheza zaidi ya namba tano uwanjani, iwe ni kwa ajili ya
ulinzi au kushambulia.
Hilo
halina ubishi kwa kuwa katika kipindi ambacho ameanza kuichezea Simba, tayari
makocha kutoka nchi tatu tofauti wameonyesha imani ya juu kwake.
Alianza
kuaminiwa na kocha mkongwe nchini, Abdallah Kibadeni ‘King Mputa’, akaaminiwa
na Logarusic wa Croatia na sasa Phiri kutoka Zambia.
Ndiyo
maana Simba imekuwa na jeuri ya kumuacha Pierre Kwizera kwa kuwa kama Jonas
Mkude hatakuwa fiti wakati fulani, wana jeuri Awadhi yupo.
Namba
tatu muhimu kwenye ulinzi na ushambulizi, sita, nane na kumi, zote amecheza kwa
ufanisi mkubwa na hii inaonyesha ni mmoja wa wachezaji wa kiwango kizuri au cha
juu lakini hawana ‘sura’ ya kupendwa na mashabiki.
Nenda
mazoezini Simba uone tofauti ya Awadhi na wachezaji wengi wengine. Juhudi
anayoonyesha inathibitisha kuwa, amelenga kupata mafanikio, ingawa anajua haonekani.
Wachezaji
kama Awadhi, bila ya kuzunguka ni wale wanaotakiwa kupata nafasi katika kikosi
cha Taifa Stars, Mart Nooij amtupie jicho.
Wachezaji
kama Awadhi ni kati ya wale wanaopaswa kupewa heshima na kuthaminiwa na klabu
yake kwa kuwa ni mchapakazi, asiye na maneno, si msumbufu na huenda ana ubora
kuzidi hata wachezaji wengi wa kigeni.
Lengo
si kumvimbisha kichwa lakini kuonyesha anachokifanya kinaonekana, anaweza
kuongeza zaidi ya hapo, akafika mbali na kuwashangaza wengi licha ya kwamba kwa
sasa, wengi hawamuoni.
0 COMMENTS:
Post a Comment