NAAMINI utakuwa unakumbuka nilipoandika makala iliyokuwa
inahusiana na suala la nani anapata nini kuhusiana na mapato ya mechi ya
kirafiki ya Nani Mtani Jembe.
Mechi hiyo inayowakutanisha watani, Yanga na Simba
inajulikana kwa kuingiza fedha nyingi na pale ukubwa wa mechi si jina Nani
Mtani Jembe, badala yake timu hizo mbili.
Nikahoji timu hizo zinafaidika na nini hasa baada ya
mechi hiyo huku nikipiga hesabu ya fedha zinazotolewa na wadhamini Kampuni ya
Bia ya Kilimanjaro ambazo mimi niliamini ni kidogo na si sahihi.
Wadhamini hawawezi kuchukua mapato ya mlangoni,
wadhamini wanaopoingia kwenye klabu kwa ajili ya kuidhamini, lengo lao linakuwa
ni kujitangaza.
Hakuna ubishi, Kilimanjaro kama ni kujitangaza, ukianzia
mbele ya watu zaidi ya 65,000 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, kweli
walijitangaza na wamefaidika.
Sasa nikawa ninahoji, vipi tena wachote na mapato ya
mlangoni, kwani Kilimanjaro ambayo iko chini ya Kampuni ya Bia Tanzania (TBL)
inafanya kazi ya kuuza bia au kuandaa mechi?
Hili ni swali ambalo sijajibiwa hadi sasa pia
nisisitize, hata kama katika fedha hizo TBL itakuwa imechukua Sh milioni moja,
bado ninahoji kwamba ni sahihi mdhamini kuingia kuchukua mapato?
Leo nina hoja tofauti kabisa, nayo ni kuhusiana na suala
la mapato yaliyopatikana katika mechi hiyo iliyojaza watu pomoni.
Kuna watu kadhaa walinipigia simu na kunifafanulia
kuhusiana na mgawo. Najua wana nia njema na ninawaamini lakini sijadhibitisha
hadi hapo itakapotolewa ‘official’ kuhusiana na mapato na mgawo wenyewe.
Kama Yanga na Simba zikicheza kwenye Ligi Kuu Bara,
kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) inatangaza suala la mapato na mgawo
ulivyokuwa mara baada ya mchezo.
Sasa kama huo ndiyo utaratibu sahihi, vipi mechi hiyo
ambayo inaandaliwa na wadhamini mapato hayatangazwi. Tunajua Simba na Yanga ni
klabu za wananchi, vizuri wajue kilichopatikana ni kiasi gani.
Sitaki kujua walioingia uwanjani ni wangapi wanakunywa
kinywaji cha Kilimanjaro, lakini najua wengi walioingia ni waliotoa kiingilio.
Je, kiasi gani kimepatikana, Simba na Yanga kila upande wameingiza kiasi gani?
Vizuri pia jamii ingejua kama wadhamini hao kuna kiasi
wanachochukua, basi wamechukua kiasi gani na kwa sababu zipi? Pia kama
hawajachukua, vizuri tukaelezwa halafu tuendelee kuhoji kama ni hivyo, fedha
hizo zimekwenda wapi na kwa nini?
Huu ndiyo wakati wa uwazi zaidi, ukimya au uficho wa
mambo unaashiria kuna tatizo au kuna mambo ya konakona. Kama hakuna tatizo,
lazima kunakuwa hakuna sababu ya kuficha mambo.
Nitaendelea kuhoji, kama wadhamini watakuwa wanachukua
fedha. Je, wanazipeleka kwenye biashara yao au wanazirudisha kwenye mpira? Haya
ndiyo mambo ambayo ninataka yafanyiwe ufafanuzi.
Leo ninauliza maswali mengi kwa kuwa tu hakukuwa na taarifa
ya kiasi kilichopatikana kwenye mechi hiyo ya watani lakini mgawo pia ulikwenda
kwa nani na yupi na kwa nini pia.
Lazima fedha za mpira zirudi kwenye mpira na kusaidia.
Hata kama serikali itakuwa imechukua nyingi kupitia kodi, bado nako nitahoji
kwa kuwa ninaamini lazima zisaidie mpira.
Yeyote anaweza kutofautiana nami, lakini fedha za
viingilio uwanjani zinatolewa na wapenda mpira, hivyo wana haki ya kuona
zinaleta maendeleo kwenye sekta wanayoifurahia.
Je, wadhamini wakichukua ni sahihi, huu ni utaratibu wa
hapa Tanzania pekee au duniani kote?
Hakika hamjachelewa, hata keshokutwa inawezekana. Ndiyo
maana nasisitiza ili kuepusha maswali mengi ninayouliza, tuelezwe mapato
yalikuwa kiasi gani? Nani na yupi alichukua, kwa nini? Nitarudi.
0 COMMENTS:
Post a Comment