Na Saleh Ally
INAWEZEKANA kabisa katika mechi zote za
Yanga dhidi ya Simba ambazo umewahi kushuhudia iwe uwanjani au ukiwa umekaa
pembeni ya runinga, hii ya leo ndiyo utatakiwa kuangalia kwa umakini zaidi.
Mechi ya leo ya Bonanza la Nani Mtani Jembe
ndiyo itakuwa na maswali mengi ambayo kila dakika 90 zinavyosonga mbele majibu
yatakuwa yanapatikana.
Mechi hiyo inaweza ikatengeneza maswali
mengi, kwa kuwa inawezekana kabisa ikashindwa kutoa majibu kwa asilimia mia.
Maswali ni yale yanahohusiana na wachezaji
wapya wa kila upande, lakini wale waliokuwepo tokea awali.
Kikubwa ni suala la namna gani wanacheza kwa
wachezaji wa zamani, lakini kwa wachezaji wapya, viongozi kupitia kamati zao za
usajili, wamefanya kazi yao kwa ufasaha au kubahatisha.
Wachezaji watatu wa kuwatupia macho kwa
Yanga kwa upande wa wapya ni Danny Mrwanda, Emerson Roque na Kpah Sherman.
Mrwanda:
Ni Mtanzania, anajulikana kwa uwezo wake wa
kufunga. Lakini hii ni mara yake ya kwanza kuichezea Yanga, tena anaanza katika
mechi dhidi ya Simba ambayo inajulikana ndiyo ilimpa umaarufu mkubwa na
‘anaipenda’.
Je, ataweza kuonyesha uwezo, atawafurahisha
mashabiki wa Yanga kwamba wamefanya kazi sahihi kuiwahi Simba na kumchukua?
Emerson:
Baadhi ya mashabiki wamefanikiwa kuona kazi
yake kwenye video akiwa katika mechi mbalimbali, anaonekana ni jembe. Je,
ataonyesha hayo akiwa kazini leo dhidi ya Simba?
Itakuwa ni mechi yake ya kwanza, hana sababu
ya kusingizia presha kubwa kwa kuwa ni professional kutoka Brazil,
kinachotakiwa ni kazi.
Sherman:
Alicheza mechi ya Ligi Kuu Cyprus, wiki
iliyopita. Alipofika mazoezini Yanga, akakimbia raundi kumi, hakuna ubishi,
yuko fiti.
Umbo lake linavutia kwa mshambuliaji, sasa
kinachotakiwa ni kazi. Picha za video zinaonyesha asipofunga, anatoa pasi. Je,
leo atafanya hivyo?
Wenyeji:
Kwa upande wa Yanga, wenyeji wapo ambao
wanatakiwa kuonyesha mabadiliko au mundelezo mzuri. Simon Msuva, amekuwa chachu
ya ushindi ya Yanga. Leo ataendeleza, halafu Mrisho Ngassa ambaye anaonekana
mvuto wake umeshuka, atapiga kiki na kuurudisha leo?
Kwa upande wa Simba halikadhalika kuna mambo
sawa na yale ya Yanga kwani kuna wachezaji watatu watakuwa wanaichezea Simba
kwa mara ya kwanza.
Danny Sserunkuma:
Kiuwezo hakua maswali, lakini anaweza
kuupasua ukuta mgumu uliojengwa na Kelvin Yondani, Nadir Haroub pamoja na
nyongeza na Mbrazil, Emerson.
Si kazi lahisi, kuonyesha umahiri wake ni
lazima afunge au kutoa pasi za mabao, mwisho aipe Simba ushindi.
Juuko Murushid:
Ni beki mpya, timu anayochezea Uganda si
kubwa. Hata kama yuko kwenye timu ya taifa, ataiweza presha ya mechi ya watani.
Ni beki, kwelia taweza kupambana na mikiki
ya ‘jitu’ kama Sherman, ufundi wa Mrwanda na kasi ya Msuva na Ngassa. Si kazi
ndogo na kama kweli Simba wamemtema Peirre Kwizera na kumpa yeye nafasi, basi
acha tumuone.
Simon Sserunkuma:
Ni bwa’mdogo wa Danny Sserunkuma. Alikuwa
anakipiga Express na akawa Simba shidaaaa wakati walipocheza mechi ya kirafiki
iliyoisha kwa sare ya suluhu.
Tatizo la Amissi Tambwe msimu huu
limeonekana ni mabao, anachotakiwa ni kuonyesha amekuja kumaliza tatizo hilo.
Kama amepewa nafasi ya Mrundi huyo, Mganda huyu lazima aonyesha Simba
wamepatia.
Wenyeji:
Shabani Kisiga na Ramadhani Singano ‘Messi’
wana deni, hawakumaliza vizuri mechi saba za mwanzo. Lazima waonyesha
mabadiliko na kwamba wao msaada maana Simba inacheza mechi yao ikiwa ina
mabadiliko ya kikosi chake kwa asilimia 55, maana haitakuwa na Amri Pierre
Kwizera, Amissi Tambwe (kama Simba imeachana nao), Kiemba, Haruna Chanongo,
Miraji Adam ambao walianza katika mechi ya kwanza ya ligi dhidi ya Coastal
Union.
Ukuta vs fowadi:
Ukiachana na wachezaji hali halisi
inaonyesha Yanga ina safu ngumu ya ulinzi, inajumuisha wazoefu na watu wa kazi.
Angalia ikiwa hivi, mbili, Mbuyu Twite, tatu-Oscar Joshua, nne-Yondani,
tano-Cannavaro na sita-
Emerson:
Kweli ni ukuta wa chuma, lakini Simba pia
wana fowadi kamwe hutakiwi kuidharau. Angalia hawa Waganda watatu, Sserunkuma
wawili na Emmanuel Okwi. Pia katika mechi kama hiyo huwezi kudharau uzoefu wa
Shabani Kisiga na ukali wa Ramadhani Singano ‘Messi’.
Ukitaka kufaidi, hata kama uwanjani, punguza
kelele na maneno mengi. Angalia kazi, nani ataifanya, kiungo yupi au kiungo cha
timu gani kitapiga chakula kinono.
Ukizungumza sana, dakika 90 za mechi
zitamalizika, halafu utatoka uwanjani na maswali kibao.
0 COMMENTS:
Post a Comment