December 2, 2014


WAKATI Ligi Kuu Bara ikiendelea, kulizuka mgogoro kati ya uongozi dhidi ya wachezaji wake watatu, Amri Kiemba, Shabani Kisinga na Haruna Chanongo.


Wachezaji hao walisimamishwa kwa madai ya aina mbili, kwanza ni utovu wa nidhamu na pili, kucheza chini ya kiwango.
Hakukuwa na ufafanuzi mkubwa wa kutosha lakini Simba walionekana wanajua mambo mengi zaidi ambayo hawakupenda yatajwe, tukawaachia wao.

Mwisho wakaanza taratibu kulimaliza tatizo hilo wakianza na lile la Kisiga ambaye alisamehewa na kurejea kundini. Pili wakamruhusu Kiemba kwenda Azam FC, limebaki suala la Chanongo.

Suala hilo limekuwa likishughulikiwa kwa ukimya wa juu lakini tayari kumekuwa na maneno kadhaa, kwamba Simba ina mpango wa kumrejesha Chanongo katika kikosi B.
Lakini Meneja wa mchezaji huyo, Jamal Kisongo ameoamba aachiwe ili aende Mtibwa Sugar ambao wameleeza hawana fedha za kumnunua lakini wako tayari kumpokea.

Kisongo aliasa kwamba halitakuwa jambo zuri kumshusha kikosi B mchezaji anayecheza katika kikosi cha timu ya taifa. Kweli, naungana naye haitakuwa sahihi.

Lakini nilikutana na mdau mwingine wa Simba, akanieleza kwamba Chanongo alionyesha utovu wa nidhamu wa hali ya juu alipokutana na viongozi wa Simba akiwemo Rais, Evans Aveva.

Alinieleza, licha ya kwamba Chanongo hakutokea mara ya kwanza, alipokwenda mara ya pili, alikuwa amevaa kofia na kuishusha hadi usoni na hata alipoombwa kuivua, alifanya hivyo kwa unyonge wa hali ya juu kama hakukubaliana na jambo hilo.

Mimi nimehadithiwa tu, sina nia ya kumshutumu Chanongo, lakini namuasa mapema kama kweli alifanya vile basi ana kila sababu ya kubadilika kwa kuwa kila atakapokwenda, ataishi na watu wazima.

Kijana kama yeye ambaye Simba wamemkuza, wamempa nafasi ya kucheza na leo anaonekana, anapaswa kuwathamini. Hata kama watakuwa wamekosea, basi iko haja ya kuzungumza nao vizuri.

Hauwezi kujua, maisha ya kawaida kama yalivyo maisha ya mpira, mambo ni kama duara. Uko huku na kule lakini siku moja unajikuta uko palepale tena, hivyo ni vizuri hata kama unaachaa na watu, basi usiwajengee vinyongo kwa kuwaonyesha dharau.

Kwa upande wa Simba, viongozi wote ni watu wazima kuliko Chanongo. Inawezekana akawa amewaudhi kweli, labda hajitambui au alipata mwongozo mbaya hadi kufikia kufanya vile.

Tunaweza kuamini yote, kwamba ni hasira labda aliona ameonewa, au kuna mtu ambaye amemshika kiushawishi alimuongoza vibaya nay eye akashindwa kujitambua.

Lakini kwa rekodi, Simba kamwe hawawezi kubadili historia kama ilivyo kwa Chanongo kwamba sura yake ilianza kujulikana akiwa Msimbazi. Sasa kwa nini kuwe na uadui kwa ajili ya jambo moja! Kwani Simba na Chanongo wamefanya mambo mangapi makubwa?

Ndiyo maana ninasisitiza sula la busara kwa pande hizo mbili. Kila mmoja akubaliane na mwenzake alipokosea na mwisho iwe ni kuangalia uamuzi gani utakuwa ni bora kama kubaki pamoja iwe kwa makubaliano mazuri na ikiwa kuachana, hali kadhalika iwe kwa uzuri.

Chanongo akiondoka Simba haiwezi kufa wala kuyumba, lakini haina maana atakwama kimaisha kama atakuwa nje ya Msimbazi. Hivyo kila mmoja anaweza kuishi kwa njia yake nzuri na yenye amani anapokuwa mbali na mwenzake.

Ndiyo maana nasisitiza sana suala la kumaliza suaka hilo kiungwana, bila ya kutanguliza kukomoana au mtu fulani kutaka mwingine afeli. Wanaopambana na maisha ni wale wenye malengo na hauwezi kufanikiwa kwa kuwakomoa wengine.

Hata iwe vipi, Chanongo aende Mtibwa Sugar au aende Yanga, hataweza kuindoa Simba kwenye historia ya maisha yake. Viongozi wa Simba pia hawawezi kumfuta kijana huyo kwenye rekodi za klabu hiyo. Watabaki kuwa familia hata kama ni kwa hadithi, hivyo kumbukeni mlikopita na busara iwe ndiyo muongozo katika kulimaliza jambo hili.




2 COMMENTS:

  1. Ninachokiona hapa ni tafsiri tu, hivi kuvaa kofia hadi usoni ni kosa!? 'alivua kiunyonge' hii ni tafsiri potofu, kama angekataa kuvua sawa lakini amevua bado mnasema ni kiunyonge!!!!!! Akutukanaye akuchagulii tusi.......!!

    ReplyDelete
  2. Thank you because you have been willing to share information with us. we will always appreciate all you have done here because I know you are very concerned with our. metodo fanart 2.0

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic