Straika mpya wa Yanga Mrundi, Amissi
Tambwe, amemuangalia straika Mliberia, Akpah Sherman na kutamka kuwa atafurahi
kama akianzishwa naye kwenye kikosi cha Yanga.
Mastraika hao wote, walijiunga na timu hiyo
hivi karibuni kwenye dirisha dogo la usajili, Tambwe yeye amesaini mkataba wa
mwaka mmoja na Mliberia miaka miwili kwa ajili ya kuichezea Yanga inayojiandaa
na Kombe la Shirikisho Afrika na Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
Washambuliaji hao, tayari wameshaanza kufanya
mazoezi pamoja ya kujiandaa na Ligi Kuu Bara inayotarajiwa kuendelea kutimua
vumbi Desemba 26, mwaka huu.
Tambwe alisema
alimuona mshambuliaji huyo kwa mara kwanza kwenye mchezo wa Nani Mtani Jembe 2,
yeye akiwa anaichezea Simba ambayo ilimalizika kwa Yanga kufungwa mabao 2-0 na
kuukubali uwezo wake.
Tambwe alisema, mshambuliaji huyo ana uwezo
mkubwa wa kufunga mabao na msumbufu kwa mabeki wa timu pinzani, hivyo anaamini
akicheza naye pamoja atafunga mabao mengi.
“Sherman ni mchezaji mzuri mwenye uwezo mkubwa
wa kucheza soka, tena katika nafasi anayocheza ya ushambuliaji, ni mshambuliaji
anayetishia mabeki wa timu pinzani.
“Natamani kucheza naye katika kikosi cha
kwanza, ninaamini nikipangwa naye pamoja, basi nitafunga mabao mengi sana.
“Kwa sababu licha ya uwezo wake wa kufunga
mabao, lakini ana uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga ni mchezaji
ninayetamani kucheza naye pamoja, lakini ninaomba muda zaidi wa kuzoeana naye
katika kipindi hiki ambacho tupo kwenye maandalizi,” alisema Tambwe.
0 COMMENTS:
Post a Comment