Na Saleh Ally
YANGA imepangiwa kuanza kampeni yake ya
michuano ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Botswana Diffence Force (BDF).
Yanga itaanzia nyumbani kati ya Februari 12, 14
na 15, halafu itasafiri hadi Gaborone, Botswana kwa marudiano kati ya Februari
27, hadi Machi Mosi, mwakani.
Timu hiyo ya Jeshi la Ulinzi la Botswana ni
maarufu sana kama BDF XI na ndiyo imekuwa moja ya timu chache ziliyoshiriki
michuano ya kimataifa mara nyingi zikitokea nchini humo.
Kwa kuangalia soka la Botswana, hakuna ubishi
tena kwamba linakua kwa kasi kubwa na kumekuwa na mabadiliko makubwa pia.
Muonekano wa tangu Shirikisho la Soka Afrika
(Caf) lilipotangaza kwamba Yanga imepangiwa BDF, ilionekana kama wao wana kazi
rahisi sana ukilinganisha na Azam FC ambao katika Ligi ya Mabingwa Afrika
watakipiga dhidi ya El Merreikh ya Sudan.
Kweli Azam FC wana kazi ngumu, lakini hakuna
linaloshindikana wakijiandaa vilivyo. Yanga pia wanapaswa kuamini wana kazi
ngumu, wakitanguliza dhaharau, imekula kwao.
Kuna mambo kadhaa ya kuangalia katika kikosi
hicho cha BDF ambavyo vinaweza kuifanya Yanga ijue haitakuwa inakutana na timu
nyanya tu kama inavyotaka kuonyeshwa.
Hadi sasa, BDF iko katika nafasi ya nne kwenye
msimamo wa Ligi Kuu ya Botswana.
Baada ya mechi 15, tayari ina pointi 28, sawa
na BMC inashika nafasi ya nne. Vinara ni Township Rollers wenye pointi 37,
wakifuatiwa na Centre Chiefs wenye 33.
Hii inaonyesha si timu ya kubeza kwa kuwa hata
Yanga hapa nyumbani, iko katika nafasi ya pili baada ya mechi saba.
Ushindi:
Katika mechi 15, BDF imeshinda tisa, imetoka
sare moja na kupoteza tano. Bado ni timu inayoweza kushinda kutokana na idadi
ya mechi ilizoibuka na ushindi.
Hivyo lazima Yanga waamini wanakutana na timu
iliyowahi kushinda na lazima wajue wachezaji wake wana morali ya ushindi.
Ushambuliaji:
Ukiipima safu yake ya ushambuliaji, katika
mechi 15, BDF XI imetikisa nyavu mara 23. Hapa pia utaona ina washambuliaji
ambao wana uwezo wa kufunga kama wataachiwa nafasi ya kufanya hivyo.
Kama timu imefikisha mabao 23 katika mechi 15,
hauwezi kusema ina wastani mbaya au haiwezi kufunga. Hii ni kengele ya usifanye
kosa.
Ulinzi:
Katika safu ya ulinzi, Yanga wanaweza kujifunza
kwa kuitumia, kwamba inapitika na inafungika. Katika mechi 15, timu hiyo
imeruhusu mabao 17 ikiwa na wastani wa kufungwa bao moja katika kila mchezo.
Maana yake, kama Yanga wakikutana nao, lazima
wahakikishe wanawafunga maana safu yao inapitika na inakubali kufungika.
Mechi 5:
Katika mechi tano zilizopita za Ligi Kuu Botswana,
matokeo ya BDF XI yanaonekana kuwa na wastani wa saizi ya kati.
Kwamba ni inayoweza kubadilika na kuwa hatari
au ikiwezekana ikafungika kirahisi. Kawaida ili ifungike kirahisi lazima
uilazimishe.
Katika mechi hizo tano za mwisho, BDF XI
imeshinda mbili, sare moja na imepoteza mbili pia.
Maana yake katika mechi tano za mwisho, BDF XI
imekusanya pointi saba na kupoteza nane. Ni wastani wa kati ambao hauwezi
kuusifia.
Kitaalamu, unapoona timu inapoteza nyumbani,
lazima ujiulize kama nguvu zao nyingi wamezielekeza kwenye michuano ya
kimataifa? Hivyo si sahihi kubweteka na rekodi zao nyumbani.
Pia katika msimamo huo, unaonekana kuna
mabadiliko, kwani ndani ya wiki mbili, BDF XI imepanda kutoka nafasi ya saba
hadi ya nne.
Hivyo ni timu inayojitutumua kutoka katika hali
duni hadi nafuu na huenda ikasonga zaidi kwa kuwa pointi zake ni sawa na aliye
katika nafasi ya tatu.
Nidhamu:
Ni timu ya jeshi, hakuna ubishi suala la nidhamu
linakuwa juu. Jeshi la Ulinzi la Botswana linasifika kwa kufanya michezo
mbalimbali kwa ufanisi.
Ufiti:
Wanaweza wasiwe wazuri kisoka, lakini kwa kuwa
ni timu ya jeshi, suala la kuwa fiti zaidi halina mjadala.
Yanga lazima waingie uwanjani wakijua wanakutana
na timu iliyo fiti. Kikubwa lazima washinde kwa idadi nzuri kwa kuwa mechi ya
kwanza ni nyumbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
0 COMMENTS:
Post a Comment