February 20, 2015


Na Saleh Ally
KUNA wachezaji wengi sana waliokuwa wakionekana hawafai kabisa katika vikosi vya Yanga au Simba, halafu walipoondoka, wakawa lulu.

Kuna rundo la wachezaji ambao wamekuwa wakionekana wanafaa wakiwa katika timu nyingine ambazo si Yanga au Simba. Wanapoondoka na kujiunga na timu nyingine, makali yao huanza kuonekana haraka sana.

Shabani Kisiga aliyekuwa ameamua kukaa kando na soka, alirejea na kujiunga na Mtibwa Sugar, akawa tishio hata kwa timu hizo kongwe. Msimu uliofuatia, akajiunga na Simba, hakuchukua raundi, kaanza kuonekana hana lolote na mwisho sasa ni ‘mtu’ wa benchi na yuko nje ya timu!

Said Bahanuzi alikuwa shujaa wa Yanga miaka mitatu iliyopita, alifunga mabao muhimu na kuipa Yanga ubingwa wa Kombe la Kagame yeye akiibuka mfungaji bora.

Nusura Bahanuzi awe shujaa tena wa Yanga baada ya kupewa penalti ya mwisho aimalize Al Ahly katika Uwanja wa Jeshi jijini Alexandria, lakini akashindwa kufunga na mwisho Yanga ikatolea.

Utafikiri mkosi, kuanzia hapo akaanza ‘kuchezea’ benchi hatua kwa hatua, hadi alipoonekana kuwa hafai kabisa akapelekwa kwa mkopo katika kikosi cha Polisi Moro.

Mwezi mmoja na nusu tu baada ya kuichezea Polisi Moro, Bahanuzi amefanikiwa kuibuka mchezaji bora wa Januari, 2015 akiwapiku wengine wakiwemo nyota wote wa Yanga.

Tayari akiwa ameichezea Polisi mechi nane, Bahanuzi amepachika mabao mawili. Awali ilielezwa ni matatu lakini ikathibitika kwamba bao moja lilifungwa na Selemani Kassim ‘Selembe’.

Bahanuzi si mchezaji wa kwanza kuondoka Yanga au Simba halafu akapata mafanikio akiwa nje ya kikosi hicho.

Lazima tukubaliane kwamba Yanga na Simba pamoja na ukubwa wao, kumekuwa na matatizo mengi sana yanayowakuta wachezaji ambayo huenda hawawezi kabisa kuyasema, lakini ni tatizo katika maendeleo ya soka.

Wanachama, hasa wale maarufu kama Makomandoo, wamekuwa wakisababisha presha kubwa. Wapo wenye nguvu hadi ya kuwavamia wachezaji na kuwatukana au kuwalaumu kwa madai wameshindwa kucheza.

Wapo Makomandoo ambao wanaamini wachezaji hawajui na wao wanaujua mpira hata kuliko wao, hivyo wanakuwa ni watu wa kwanza kuwapa presha kubwa wachezaji hao.

Ukiachana na hao Makomandoo, viongozi wengi wanaoongoza soka na hasa Yanga na Simba, hawajui mpira na hawajajifunza mengi kuhusu mpira lakini kwa kuwa ni viongozi waliopigiwa kura au ni wale ambao wamekuwa wakisaidia kifedha katika klabu na timu, basi wanajiona wanajua sana.

Kuna skendo inaendelea Simba ya kiongozi kubainika kwamba alikuwa akimpangia timu mwalimu Goran Kopunovic. Simba wamekuwa kimya katika hilo lakini ukweli ni tatizo kubwa.

Tunajua halijaanza leo au kwa uongozi wa sasa pekee wa Simba. Ukweli ni kwamba kila anayeongoza Yanga au Simba huona anajua sana mpira kuliko wengine na huenda anajua hata kuliko kila kocha anayeajiriwa.

Kichekesho cha Simba, eti kiongozi anampangia mwalimu timu pia anataka kueleza hadi mfumo gani utumike. Tayari kuna ufafanuzi umetoka, kwamba kiongozi alitoa ushauri tu.

Swali linabaki palepale, kuwa kweli kiongozi anaweza akawa anajua mfumo unaotakiwa kutumika au 4-4-2 inatumika vipi linapofikia suala la aina uchezaji?

Hata kama viongozi wa Simba watakuwa wanajaribu kuficha, lakini hilo ni tatizo na ndiyo sehemu ambayo imekuwa ikiwaangusha baadhi ya wachezaji kwa baadhi ya viongozi wa klabu hizo kongwe kuona wanajua sana na kufikia hadi kuwapangia walimu wapange vipi vikosi vyao.


Kuna kila sababu ya viongozi na hao wanachama wanaojiita Makomandoo, wajiulize. Wabadilike kwamba wachezaji wanakwama kwa sababu zao na faida zao na si za klabu na timu zao!

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic