Na Saleh Ally
KAMA ulishuhudia mechi kati
ya Liverpool dhidi ya Besiktas ya Uturuki unaweza kujifunza mambo mengi sana
kuhusiana na mshambuliaji Mario Balotelli.
Balotelli raia wa Italia
mwenye asili ya Ghana, huenda ndiye binadamu ‘asiyejali’ zaidi kuliko wote
duniani.
Muitaliano huyo, pia
anaweza kuingia kwenye kundi la watu wanaosahau matatizo au kero haraka kuliko
mwingine yeyote.
Balotelli amefanya kituko
cha aina yake katika mechi hiyo ya Michuano ya Europa baada ya kumpokonya mpira
nahodha wa timu hiyo, Jordan Herdeson na kwenda kupiga penalti.
Wakati anampokonya mpira
huo, mshambuliaji mwingine tegemeo, Danny Sturridge alikuwa akitamani apige
yeye, akamsisitiza nahodha wake ampokonye mpira Balotelli, haikuwezekana.
Akionekana kujiamini,
alitembea na mpira mkononi ikiwa dakika ya 84. Akauweka eneo maalum la kupiga
na kuupiga kwa ufundi mkubwa. Mwisho Liverpool ikashinda kwa bao 1-0 dhidi ya
Waturuki hao.
Ukiliangalia suala la
Balotelli lina sura mbili, kwanza ni utukutu kama ilivyozoeleka na hata amekuwa
akionekana kama ni kituko.
Balotelli hajali, akiamua
kufanya jambo bila hata kuangalia madhara yatakuwa nini, basi yeye anafanya na
hajali kama inawezekana au la.
Kwa kuwa ni majeruhi,
nahodha wa Liverpool, Steven Gerrard alikuwa jukwaani akifanya kazi ya
uchambuzi kupitia runinga ya ITV.
Gerrard alimsifia Balotelli
kufunga, lakini akasisitiza suala la kugombea mkwaju wa penalti kwamba halikuwa
jema na si picha nzuri. Hilo kweli.
Kujiamini:
Utukutu wa Balotelli ni
sehemu ya kuonyesha yeye ni kiburudisho kweli, maana anaamini anachokifanya
hata kama si sahihi.
Lakini kujiamini kwake ni
kwa hali ya juu sana. Huenda wachezaji saba kati ya 10 walio uwanjani ukitoa
kipa, wangeweza kukimbia kupiga mkwaju katika dakika ya 85 wakijua ni lawama
kama wangekosa.
Kwa Balotelli lawama si
jambo kubwa sana kwake. Alijiamini na kuchukua ule mpira, akijua wazi kama
angekosa, basi angekuwa katika matatizo makubwa.
Kwani tangu ametua England,
amefunga katika mechi moja tu ya Ligi Kuu England. Amekuwa na presha kubwa hadi
alipofunga bao hilo, sasa jiulize angeipoteza penalti hiyo ingekuwaje?
Lakini kwa kuwa Balotellia
anajiamini, hakuona shida. Akagombea mpira, akapiga na kufunga. Mwisho yeye
ndiye shujaa hata kama itaonekana amekosea, alichokosea kinafutika.
Maisha ya Balotelli ni
zaidi ya hadithi, amezaliwa katika familia ya Kiafrika ya Barwuah na kulelewa
na familia ya Kizungu ya Balotelli. Huenda hilo ni tatizo kwake pia kwa kuwa
haelewani kabisa na baba yake mzazi lakini amekuwa akiendelea kutoa huduma
katika familia yake.
Kelele kubwa ya vyombo vya
habari vya England ni Balotelli kutokuwa msaada kwa Liverpool kutokana na
kutofunga mabao, anaonekana ni hasara.
Safari hii amegeuza
uelekeo, kwanza amefunga bao la ushindi katika Ligi Kuu England wakati
Liverpool ilipoishinda Tottenham Hotspurs kwa mabao 3-2. Sasa amefunga bao lake
muhimu na kuibeba Liverpool.
Mabao mawili yaliyopeleka
pointi tatu na nafasi nzuri ya kusaidia kusonga mbele katika Ligi ya Europa.
Unawezaje kumkosoa Balotelli kwa kusema hajui? Hakika itakuwa vigumu.
Kujiamini kupindukia:
Karibu kila mmoja anajua
Balotelli anaathirika kwa kujiamini kupindukia. Si mwoga na asiyejipima alipo
ni sehemu sahihi ya kufanya anachotaka au la.
Akiwa Man City alizichapa
na Jerome Boateng, akazozana na Yaya Toure, Micah Richard na Kocha Roberto
Mancini. Liverpool tayari ameishazua mzozo na Sturridge.
Kuna mengi ya kujifunza kwa
Balotelli. Kwanza kabisa si kumhukumu kwa makosa yake, iko haja ya kuangalia
pia ubora wake kama ambavyo leo Wazungu wamekuwa wakiangalia ubora wa
Balotelli.
Kama ingekuwa ni kuangalia
ubora tu, hakuna atakayetaka kuendelea kufanya naye kazi leo hii. Lakini kwa
wachezaji, pia wakati mwingine wajifunze, kujiamini ni sehemu bora hasa kama
unachokifanya unaamini ni bora ingawa kukubali ushauri kama unaona ni sahihi
pia ni bora zaidi.
Kweli Balotelli ni mtukutu,
lakini angekuwa hajiamini ingekuwa rahisi kuyumbishwa na huenda leo angekuwa
anakipiga katika timu ya daraja la pili.









0 COMMENTS:
Post a Comment