Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic, ameingizwa mjini baada ya
kuibiwa kiasi cha dola 300 (Sh 510,000) pamoja na fedha za Kitanzania ambazo
hazikufahamika ni kiasi gani akiwa katika hoteli yenye hadhi kubwa mkoani
Morogoro.
Kocha huyo amekumbwa na tukio hilo alipokuwa mkoani humo wakati timu
yake ilipokuwa mkoani humo maalum kwa ajili ya mechi dhidi ya Polisi Morogoro
iliyochezwa, Jumapili iliyopita.
Filamu ya tukio hilo ipo hivi; alipofika mkoani hapo alifikia katika
hoteli (jina kapuni), Jumanne asubuhi kocha huyo alihamishiwa katika hoteli
nyingine kwa sababu za kile kilichoelezwa usalama.
Baada ya hapo, mizigo ya Kopunovic ikatangulizwa kwenye hoteli hiyo
kubwa na kisha michakato yote ikafanyika, baada ya kocha huyo kufika hotelini
hapo na kuingia ndani jioni ya siku hiyo, ndipo alipogundua kuwa kulikuwa na
upungufu wa kiasi hicho cha fedha na kuamua kuripoti suala hilo kwa uongozi wa
hoteli.
Baada ya kocha huyo kuripoti, uongozi wa hoteli ukaitisha kikao cha
dharura na kukubaliana kumlipa fidia ya shilingi 540,000 licha ya kudai kuwa
hoteli hiyo haihusiki katika upotevu huo, lakini umeamua kufanya hivyo ili
kulinda heshima ya wateja wao na hoteli hiyo kwa jumla.
Chanzo kutoka katika hoteli hiyo kilisema kuwa, ulifanyika upekuzi
juu ya yeyote aliyehusika kuingia kwenye chumba cha kocha huyo kupitia kamera
zilizopo hotelini hapo lakini hakukuwa na jibu la uhakika la kilichotokea
kwenye kamera hizo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Simba, Humphrey Nyasio juu ya suala
hilo alikanusha vikali kuwepo kwa taarifa hizo na kusema: “Hakuna kitu kama
hicho, kama kungekuwa na suala kama hilo lazima kocha angeniambia tu.”
Upande wa uongozi wa hoteli hiyo haukuwa tayari kufunguka wakati
Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Simba, Kassim Dewji alikiri kuwepo kwa suala
hilo na akalitolea ufafanuzi.
“Hilo suala la wizi ni kweli limetokea na ni kwamba kocha alitoka
chumbani kwake, aliporejea akakuta fedha zake zimepungua, kulikuwa na dola 600
lakini akakuta zimebaki 300.
“Ni ajali imetokea na sisi kama uongozi tumesikitishwa na
kusononeshwa kwa wizi huo ingawa kocha hakutakiwa kuacha fedha chumbani. Kuhusu
kulipwa taarifa hizo sijazipata ila kama amelipwa tayari au mtu amejitolea
kuzilipa, basi ni suala zuri,” alisema Dewji.
SOURCE: CHAMPIONI







0 COMMENTS:
Post a Comment