Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe Mkoa wa Njombe, Fredrick Wilfred
Mwakalebela, ameahidi kuifanyia makubwa wilaya hiyo kwa kuanza na kuinua mchezo
wa soka.
Kauli hiyo ameitoa ikiwa ni siku moja tangu Rais wa Jamhuri ya
Muungano ya Tanzania, Dk Jakaya Kikwete kumtangaza kuwa mkuu mpya wa wilaya
hiyo.
Mwakalebela ambaye ni katibu mkuu
wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), alisema wilaya hiyo ni mpya,
hivyo anakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha soka linapiga hatua
wilayani humo.
Mwakalebela alisema wilaya hiyo ina mwamko mdogo katika soka, hivyo
katika kuhakikisha anakuza mchezo huo, amepanga kuuinua kwa kuanza na shule za
msingi na sekondari kwa kuwaanzishia mashindano ya wenyewe kwa wenyewe.
Aliongeza kuwa, pia amepanga kugawa vifaa mbalimbali vya michezo
zikiwemo jezi, mipira, soksi na viatu kwa ajili ya kuchezea soka kwa wanafunzi.
“Kiukweli ninakabiliwa na changamoto kubwa ya kuhakikisha wilaya
yangu inapiga hatua kwenye mchezo wa soka, hiyo ni kutokana na wilaya yenyewe
kuwa mpya ambayo haina mwamko wa michezo.
“Kikubwa nitaandaa mashindano ya wenyewe kwa wenyewe mashuleni kwa
kuanzia shule za msingi na sekondari, pia nitaandaa mashindano mengine mitaani
kama yale ya Mufindi yaliyopewa jina la Muungano kwa kugawa vifaa vya michezo,
ninaamini nitafanikiwa katika hilo kutokana na uzoefu wangu wa kuendesha soka
nikiwa na TFF,” alisema Mwakalebela.







0 COMMENTS:
Post a Comment