Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic,
amewataka wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kutulia na kuendelea kumuunga mkono
katika kipindi hiki anachoendelea kukisuka kikosi chake ili kiweze kuendana na
hadhi ya klabu hiyo ambayo ilianzishwa mwaka 1936.
Kocha huyo raia wa Serbia
ambaye amejiunga na klabu hiyo hivi karibuni akichukua mikoba ya Mzambia,
Patrick Phiri, ameyasema hayo juzi Jumamosi alipoiongoza Simba kuibuka na
ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya JKT Ruvu katika mchezo wa Ligi Kuu Bara kwenye
Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mbali na mechi hiyo, pia
Kopunovic ameshaiongoza Simba katika mechi nyingene saba na kushinda sita na
kupoteza moja tangu alipoanza kuifundisha timu hiyo Janura 2 mwaka huu.
Kopunovic alisema kuwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo waendelee
kuwa watulivu na wavumilivu huku wakimuunga mkono katika harakati zake za
kuhakikisha kikosi chake hicho kinakuwa sawa.
“Bado naendelea kukisuka
kikosi changu, hivyo mashabiki wetu wawe watulivu na waendelee kutuunga mkono
ili tuweze kufikia malengo yetu tuliyojiwekea.
“Tangu nianze kuifundisha
timu hii ndiyo kwanza kesho Jumatatu (leo) natimiza mwezi mmoja, hivyo ni muda
mchache sana lakini nimekuwa nikijitahidi kuhakikisha tunakuwa vizuri,” alisema
Kopunovic.
Hata hivyo, uongozi wa
Simba kupitia kwa rais wa klabu hiyo, Evans Aveva, umesema kuwa hauna wasiwasi
na kocha huyo na unaridhishwa vilivyo na utendaji wake wa kazi.
“Hatuna wasiwasi na kocha,
tunalidhika na utendaji wake wa kazi, kwani kwa muda mfupi tu aliochukua timu,
ameweza kufanya mambo makubwa, hivyo tunawaomba Wanasimba tushirikiane naye
vizuri ili aweze kutufikisha kule tunakotaka kufika,” alisema Aveva.
0 COMMENTS:
Post a Comment