INAWEZEKANA leo itakuwa ni zaidi ya mara
tatu naandika kuhusiana na usalama kuwa hovyo, uliozorota na hatari kwa
wanamichezo ndani ya Uwanja wa Mkwakwani mjini Tanga.
Katika misimu mitatu, nilifanikiwa
kuhudhuria mechi mbili katika uwanja huo na kushangazwa na mambo mengi sana
huenda si lahisi kuyaona katika viwanja vingi vya soka au michezo hapa nchini.
Kwanza ni mashabiki wake kupenda ugomvi
kupindukia, tena ugomvi usiokuwa na sababu za msingi. Yaani ni sehemu ambayo
mashabiki wao wanaamini ubabe ndiyo ujanja, ugomvi usiokuwa na sababu.
Mwaka juzi wakati Yanga ikipambana na
Coastal Union iliyokuwa chini ya Jamhuti KIhwelo ‘Julio’ na kuishinda kwa bao
1-0 lililofungwa na Mganda Hamis Kiiza.
Mashabiki walifanya vurugu za
kupindukia hadi kwa waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti mchezo huo.
Mashabiki hao walianza kuwashambulia
waandishi wakati wakimshutumu mwamuzi aliipendelea Yanga.
Chupa za maji na
matusi yakaanza kuwaangukia waandishi waliokuwa wametulia tuli wakiripoti.
Binafsi nilishangazwa kushuhudia sura nyingi za ninaoweza kuwaita watu wazima
au wakuu wa familia wakifanya upuuzi huo. Nilifanya juhudi kuu kuwapiga picha
ili niwaanike, wakajificha.
Kujificha kwao kulinifanya niamini kuwa
walichafua hali ya amani kwa makusudi huku wakijua waziwazi walichokifanya
hakikuwa kitu cha kiungwana na si cha kistaarabu. Sasa vipi wanafanya hivyo!
Tokea hapo nimekuwa nikiendelea kushuhudia
vurugu karibu kila mechi ya Yanga au Simba zinapocheza kwenye uwanja huo.
Wakati mwingine hata timu hizo za Coastal Union na Mgambo zinapokutana. Hawa
watu wa Tanga vipi, wanajua sana ngumi? Sasa kwa nini wengi wao wasicheze judo
au Kung Fu wakaachana na soka ambayo haitaki “Yan kibadachi!”
Juzi umeona tena, mara tu baada ya mechi
kati ya Mgambo dhidi ya Yanga kumalizika, mashabiki hao waliruka uzio na
kuvamia uwanjani na kuanza kuwabeba wachezaji wa Yanga, hasa Simon Msuva.
Hawa walikuwa mashabiki wa Yanga, jiulize
vipi wamekuwa na tabia hizo za kizamani ambazo sasa ni nadra kuona zinajitokeza
katika mechi za Ligi Kuu Bara katika viwanja mbalimbali. Bado ninaamini ni
mashabiki wa Yanga wa mkoani Tanga ambao wamezoea kutofuata utaratibu.
Kama wangekuwa Yanga wa Dar es Salaam, mbona
hawafanyi hivyo kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar. Msisitizo kama ni wa Dar es Salaam
walifanya hivyo, basi hata Polisi wanaosimamia ulinzi Mkwakwani nao watakuwa ni
wazembe na wanastahili kubadilika.
Vipi mashabiki wavuke uwanja na kuingia
ndani mara tu baada ya mechi. Waliokuwa wamembeba Msuva, tuna uhakika vipi wote
wanampenda. Wangemchoma kisu, tena tunajua siku chache zilizopita, mashabiki wa
Yanga wamekuwa wakimtafuta na kutaka kumpiga!
Msimu ujao, mji wa Tanga utakuwa na timu
tatu zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ambazo ni Coastal Union na Mgambo ambazo
hazina ugeni tena wa ligi hiyo.
Usisahau wakongwe wengine African Sports nao
wamerejea baada ya kushika nafasi ya pili wka ubora baada ya Mwadui FC ya
Shinyanga.
Upinzani wa African Sports dhidi ya Coastal
Union unajulikana kwa kuwa ni kati ya timu kongwe kabisa za soka nchini. Lazima
kutakuwa na vurugu katika kila mechi inayozihusisha hata kabla hazijakutana
zenyewe.
Pia kutakuwa na vurugu katika kila mechi
inayokutanisha Coastal na Simba Yanga au African Sports dhidi ya Yanga au
Simba. Unaweza kusema wigo wa vurugu na upana wa matatizo utaongezeka katika
uwanja huo wa Mkwakwani. Swali, walinzi wa uwanja huo wanaoonekana kutokuwa
tayari katika misimu mitatu au zaidi sasa, watakuwa tayari kudhibiti hali hiyo
ya hovyo msimu ujao?








0 COMMENTS:
Post a Comment