Na Saleh Ally
INAWEZEKANA isiwe ajabu kama utasikia uongozi
wa Simba umeanza harakati za kuhakikisha unamnasa mshambuliaji Amissi Tambwe wa
Yanga ili kuongeza nguvu ya kikosi chake katika ufungaji!
Tambwe tayari ana mabao matano katika Ligi Kuu
Bara, moja amefunga akiwa Simba na mengine manne baada ya kuhamia Yanga wakati
wa usajili wa dirisha dogo.
Si vibaya kukumbushana namna makosa yamekuwa
yakifanyika katika timu nyingi za soka nchini na hasa klabu za Yanga na Simba
ambazo viongozi wengi wamekuwa wakiziendesha kwa kujali uzoefu bila kujali
kujiendeleza au kujifunza jambo fulani.
Viongozi wengi wenye nafasi angalau ya kupaza
sauti katika klabu hizo, si wale wanaokubali kwamba mambo yanabadilika katika
soka, lakini wanauamini uzoefu wao kuwa hauyumbi wala kushindwa, kitu ambacho
ni kosa kubwa.
Mfano mzuri ni suala la mshambuliaji Tambwe
raia wa Burundi ambaye kila kitu kipo wazi sasa kuwa anahitajika katika kikosi
hicho.
Simba inatengeneza nafasi nyingi lakini hakuna
mtu anayeweza kusimama na kuzimalizia. Kwa kawaida, unaweza kusema Simba ina
mshambuliaji mmoja tu, Elias Maguri ambaye anajifunza.
Maguri si mzoefu, ndiye anaanza kuchipukia
kuingia kwenye kundi la wafungaji mahiri, tena kama ataendelea kujitahidi. Utamuona
ni mpambanaji hasa, lakini nani mmaliziaji mzuri na anajifunza kwa nani?
Tambwe alikuwa jibu sahihi na utaona kazi
anayoifanya Yanga sasa inakosea mengi yaliyosemwa na viongozi wa Simba wakati
wakipambana kuhakikisha anaondoka.
Kukaba:
Wengi walisema hakabi, kilikuwa kichekesho kwa
kuwa hawakuwa na ushahidi wa kutosha na huenda hawakukumbuka angalau mechi nne
tano alizocheza.
Tambwe ni kati ya wachezaji wanaokaba tena kwa
kero kubwa, anayewapa presha kubwa kila mabeki anaokutana nao. Mmoja alisema,
wengine wakamuamini na uzushi ukasambaa na kupata nguvu.
Anavizia tu:
Huenda hiki ndiyo kilikuwa kichekesho bora
zaidi, kwamba Tambwe anavizia pekee na mabao yake mengi ni penalti tu.
Aliyofunga Yanga kwa sasa, hakuna hata moja la penalti, amefunga mengi ya
vichwa ambayo yanaaminika kuwa mabao magumu zaidi kwa kuwa yanahitaji ufundi
zaidi.
Ile hadithi kuwa hana uwezo wa kuwatoka mabeki
wawili, pia imezimika kwa kuwa anaonekana anavyopambana na mshambuliaji si
lazima kukimbia mbio kama winga.
Kpah Sherman wa Yanga ana uwezo wa kuwatoka
hata mabeki sita, lakini hajafunga hadi leo. Tambwe asiyeweza kuwatoka, anazidi
kufunga. Ana mabao manne katika Ligi Kuu Bara na matatu katika michuano ya
Kombe la Shirikisho.
Mapenzi:
Tabia ya kuamini mapenzi yao kwa viongozi ni
tatizo kubwa. Wanaziangusha timu kwa kuwa kumuondoa Tambwe katika kikosi cha
Simba, ilikuwa ni furaha iliyoanzia kwa mtu mmoja, akaamini kilicho katika
ubongo wake, akawasambazia wengine, nao wakalibeba.
Mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi
Kuu ya Burundi na Kombe la Afrika Mashariki na Kati kwa klabu maarufu kama
Kagame kabla ya kutua Simba.
Alipotua nako akaibuka mfungaji bora kwa
kufunga mabao 19 katika mechi 23 tu alizocheza, anaachwa eti haendani na mfumo
wa kocha. Wakati huo, Patrick Phiri ndiye alikuwa kocha mkuu wa Simba, akapinga
vikali hilo, kwamba kamwe asingeweza kumuacha mfungaji bora wa msimu uliopita,
jibu unalo mwenyewe.
Mashabiki:
Lazima kukubali, viongozi wengi wa soka ni
mashabiki kwa kuwa si wataalamu wa soka. Mambo yao wanayapeleka kishabiki na
wakati mwingine wanaongozwa na hisia za mashabiki wao, hili ni somo.
Mfano mzuri ni Simon Msuva, amechipukia akiwa
na tatizo kubwa la umaliziaji. Mwishoni mwa msimu uliopita alionekana
kubadilika na kuanza kufunga mfululizo, mashabiki wakampenda na kumshangilia
mno.
Mechi nne mfululizo aliposhindwa kufunga huku
akipoteza nafasi wakamchukia, wakataka kumpiga mara baada ya mechi dhidi ya
Simba!
Ajabu, juzi kaifungia Yanga dhidi ya Mgambo,
mwisho wa mchezo, wamembeba! Utajua hao ni watu wa aina gani, sifa zao zikoje
na inabidi uishi nao vipi.
Viongozi nao ni mashabiki kwa kuwa tabia zao
hazipishani na hizo. Simba waliwahi kumuondoa Donald Musoti, wakamsajili Pierre
Kwizera, siku chache baadaye wakataka kumrudisha wakiona wamekosea. Kisa cha
kumuondoa, alifanya vibaya mchezo mmoja tu.
Mkikaa pamoja watu wengi mnaojua sana, mara
nyingi mambo huharibika kwa kuwa kila mmoja hujibandika utaalamu na kutaka
akubaliwe au kuheshimiwa kwa kile anachoamini.
Simba walikuwa wakali kuambiwa si sahihi
kumuacha Tambwe. Waliamini wako sahihi, lakini walisema hawezi kufunga ameisha,
sasa anaonyesha tofauti kabisa, unaweza kusema anawapiga msasa taratiiibuuu,
wakiwa tayari kujifunza, watabadilika.
Mabao zaidi ya saba akiwa na Yanga katika
michuano yote tangu ajiunge katika dirisha dogo, inaonyesha walibahatisha na
lazima wajifunze si kumuangushia mzigo Phiri.
Kumsaidia kocha si jambo baya, lakini
kushinikiza ili kufurahisha nafsi za wachache na kusahau maslahi ya klabu ni
tatizo jingine kubwa.
Sura inajionyesha Yanga wana jicho sahihi kwa
kuwa waliona Simba wakipotea njia kumuacha Tambwe, wakamuwahi njia, wakampa
mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akilipwa Simba na kumpangishia nyumba nzuri
Sinza. Leo anawafanyia kazi vizuri na hata asipofunga, kazi yake imekuwa
ikionekana kwamba alisaidiaje kikosi.
Sifa nyingine ya Tambwe ni mchezaji mwenye
nidhamu ya hali ya juu, Simba wanalijua hilo na hawawezi kumlinganisha na
wengine ambao sasa wanawasumbua kila siku mara wagonjwa, mara walitaka kurogwa,
mara wamesusa hawajapangwa. Wajifunze, watafakari na kubadilika.
Mabao manne aliyoyafunga Tambwe katika Ligi Kuu
Bara akiwa Yanga ni dhidi ya timu ambazo Simba haijashinda katika ligi.
Amezifunga Azam FC wakatoka sare, halafu akaongoza ushindi wa Yanga dhidi Mbeya
City, Kagera Sugar na Mgambo.
Enzi za kubahatisha, enzi za mmoja kutaka
kujifurahisha bila kufanya tathmini za kitaalamu wakati wa usajili zimekwisha.
Hakuna ubishi tena, hata kama itakuwa ndiyo mwisho wake kufunga juzi, lakini
Tambwe anajua kufunga kuliko mastraika wa Simba na Simba walistahili kumbakiza
si kukurupuka kama walivyofanya, jifunzeni.








Nimesoma makala yako na nimeona niweke na mimi hoja zangu angalau na upande wa pili nao usikike. Kwanza ningependa nisema wazi kuwa mpira hauna fomula kama vile hesabu kwamba 2 jumlisha mbili dunia nzima jibu lake ni 4. Hii ina maana kuwa sio kweli kuwa mchezaji Fulani akiwa mzuri na timu moja basi atakuwa mzuri kwenye timu nyingine au kila timu atakayochezea. Mpira huchezwa na timu nzima na sio mtu mmoja na pale kila mmoja atakapotimiza wajibu wake utapata team work na matokeo bora.
ReplyDeleteMchezaji anaweza akawa mzuri kwa sababu ya ushirikiano mzuri wa wachezaji wenzake ambapo anaweza akahamia timu nyingine na asifanye vizuri kwa sababu haendani na wachezaji anaowakuta au ikawa kinyume chake kwamba alikotoka hakufanya vizuri na akafanya vizuri alikoenda. Mifano ya namna hii iko mingi sana na watu wa mpira wanaijua. Ndio maana narudia kusema hakuna formula katika mchezo huu.
Sielewi kwa nini katika suala la Tambwe kuwe kuna lawama kwa Simba kwa kumuacha na sifa kwa Yanga kwa kumchukua kwa sababu Simba walimuacha kwa kuwa kweli alikuwa hafungi magoli na hata alipokwenda Yanga hakufunga magoli pia katika mechi nyingi tu. Siku zote mfungaji hupimwa kwa nafasi ngapi kapata na katumia ngapi na sio magoli mangapi katika mechi ngapi kwa sababu mara nyingi nafasi hutengenezwa na wachezaji wengine na sio mfungaji. Kama katika nafasi 10 anatumia moja binafsi siwezi kumuweka katika wafungaji wazuri ila kama katika nafasi 3 atatumia moja basi huyo ni mzuri.
Unapenda sana kumtumia Phiri katika maelezo yake lakini ujue kuwa yule ni mtu ambaye hapendi lawama hata siku moja lakini siku zote maneno ya mtu huthibitshwa na vitendo vyake. Sasa kama ni kweli Phiri alikuwa anamuona Tambwe ni striker mzuri ungemuuliza basi ni kwa nini alikuwa akimtumia mwanzoni lakini taratibu akaanza kumweka pembeni kama substitute na baadaye akawa anampa dakika tano za mwisho. Huu si mwenendo wa kumtumia mchezaji mahiri bali ni wa kumweka kando mchezaji mzigo lakini naona wewe umeyapa uzito maneno yake zaidi ya matendo yake. Ilipofikia hatua hiyo ulitegemea uongozi ufanye nini zaidi ya kumuachia mchezaji akatafute riziki yake kwingine kuliko kumbakiza huku mkiona mchezaji aliyekuwa mzuri akiishia.
Nilitegemea kuwa kwa kutambua hivyo mngeusifia uongozi wa Simba lakini badala yake mnawalaumu na kuwakejeli ati sasa wanammezea mate kama vile umewaona wakifanya vile. Sio kweli kuwa haukuwa sahihi uamuzi ule kwa kipindi kile na kama hali ingewezekana kujirudia basi uamuzi bado ungekuwa vile vile.
Pengine pia ingefaa uangalie huko alikoenda ameanza kufunga lini na katika mfumo gani maana kacheza muda mrefu tu bila kufunga pengine hata wao na nyie mlianza kukubali kuwa labda ni kweli kapungua kiwango. Sasa hivi mfumo wa uchezaji Yanga umebadilika na wanatumia viungo watatu badala ya kutumia mashambulizi ya pembeni na ni mabadiliko hayo ambayo Tambwe ameweza kupata nafasi. Kuna msemo wa kiingereza unasema no situation is permanent na maamuzi mengi hufanywa na uongozi wakizingatia hali halisi ya wakati huo. Mara nyingi naona unapenda kuzungumza na Phiri na ukifanya hivyo tena si vibaya ukamuuliza ni kwa nini alifikia kumpa Tambwe dakika tano za mwisho na umahiri wake wote na pia si vibaya ukimuuliza pia ni kwa nini hakukubali kuwatumia Ndemla na Banda ambao sasa ndio tegemeo la Simba. Kama nilivyosema mwanzoni hakuna formula na zuri la leo ndio baya la kesho. Wakatabahu