March 23, 2015


Na Saleh Ally
INAWEZEKANA isiwe ajabu kama utasikia uongozi wa Simba umeanza harakati za kuhakikisha unamnasa mshambuliaji Amissi Tambwe wa Yanga ili kuongeza nguvu ya kikosi chake katika ufungaji!


Tambwe tayari ana mabao matano katika Ligi Kuu Bara, moja amefunga akiwa Simba na mengine manne baada ya kuhamia Yanga wakati wa usajili wa dirisha dogo.

Si vibaya kukumbushana namna makosa yamekuwa yakifanyika katika timu nyingi za soka nchini na hasa klabu za Yanga na Simba ambazo viongozi wengi wamekuwa wakiziendesha kwa kujali uzoefu bila kujali kujiendeleza au kujifunza jambo fulani.

Viongozi wengi wenye nafasi angalau ya kupaza sauti katika klabu hizo, si wale wanaokubali kwamba mambo yanabadilika katika soka, lakini wanauamini uzoefu wao kuwa hauyumbi wala kushindwa, kitu ambacho ni kosa kubwa.

Mfano mzuri ni suala la mshambuliaji Tambwe raia wa Burundi ambaye kila kitu kipo wazi sasa kuwa anahitajika katika kikosi hicho.


Simba inatengeneza nafasi nyingi lakini hakuna mtu anayeweza kusimama na kuzimalizia. Kwa kawaida, unaweza kusema Simba ina mshambuliaji mmoja tu, Elias Maguri ambaye anajifunza.

Maguri si mzoefu, ndiye anaanza kuchipukia kuingia kwenye kundi la wafungaji mahiri, tena kama ataendelea kujitahidi. Utamuona ni mpambanaji hasa, lakini nani mmaliziaji mzuri na anajifunza kwa nani?

Tambwe alikuwa jibu sahihi na utaona kazi anayoifanya Yanga sasa inakosea mengi yaliyosemwa na viongozi wa Simba wakati wakipambana kuhakikisha anaondoka.

Kukaba:
Wengi walisema hakabi, kilikuwa kichekesho kwa kuwa hawakuwa na ushahidi wa kutosha na huenda hawakukumbuka angalau mechi nne tano alizocheza.

Tambwe ni kati ya wachezaji wanaokaba tena kwa kero kubwa, anayewapa presha kubwa kila mabeki anaokutana nao. Mmoja alisema, wengine wakamuamini na uzushi ukasambaa na kupata nguvu.

Anavizia tu:
Huenda hiki ndiyo kilikuwa kichekesho bora zaidi, kwamba Tambwe anavizia pekee na mabao yake mengi ni penalti tu. Aliyofunga Yanga kwa sasa, hakuna hata moja la penalti, amefunga mengi ya vichwa ambayo yanaaminika kuwa mabao magumu zaidi kwa kuwa yanahitaji ufundi zaidi.

Ile hadithi kuwa hana uwezo wa kuwatoka mabeki wawili, pia imezimika kwa kuwa anaonekana anavyopambana na mshambuliaji si lazima kukimbia mbio kama winga.

Kpah Sherman wa Yanga ana uwezo wa kuwatoka hata mabeki sita, lakini hajafunga hadi leo. Tambwe asiyeweza kuwatoka, anazidi kufunga. Ana mabao manne katika Ligi Kuu Bara na matatu katika michuano ya Kombe la Shirikisho.

Mapenzi:
Tabia ya kuamini mapenzi yao kwa viongozi ni tatizo kubwa. Wanaziangusha timu kwa kuwa kumuondoa Tambwe katika kikosi cha Simba, ilikuwa ni furaha iliyoanzia kwa mtu mmoja, akaamini kilicho katika ubongo wake, akawasambazia wengine, nao wakalibeba.

Mshambuliaji aliyekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu ya Burundi na Kombe la Afrika Mashariki na Kati kwa klabu maarufu kama Kagame kabla ya kutua Simba.

Alipotua nako akaibuka mfungaji bora kwa kufunga mabao 19 katika mechi 23 tu alizocheza, anaachwa eti haendani na mfumo wa kocha. Wakati huo, Patrick Phiri ndiye alikuwa kocha mkuu wa Simba, akapinga vikali hilo, kwamba kamwe asingeweza kumuacha mfungaji bora wa msimu uliopita, jibu unalo mwenyewe.

Mashabiki:
Lazima kukubali, viongozi wengi wa soka ni mashabiki kwa kuwa si wataalamu wa soka. Mambo yao wanayapeleka kishabiki na wakati mwingine wanaongozwa na hisia za mashabiki wao, hili ni somo.


Mfano mzuri ni Simon Msuva, amechipukia akiwa na tatizo kubwa la umaliziaji. Mwishoni mwa msimu uliopita alionekana kubadilika na kuanza kufunga mfululizo, mashabiki wakampenda na kumshangilia mno.

Mechi nne mfululizo aliposhindwa kufunga huku akipoteza nafasi wakamchukia, wakataka kumpiga mara baada ya mechi dhidi ya Simba!

Ajabu, juzi kaifungia Yanga dhidi ya Mgambo, mwisho wa mchezo, wamembeba! Utajua hao ni watu wa aina gani, sifa zao zikoje na inabidi uishi nao vipi.

Viongozi nao ni mashabiki kwa kuwa tabia zao hazipishani na hizo. Simba waliwahi kumuondoa Donald Musoti, wakamsajili Pierre Kwizera, siku chache baadaye wakataka kumrudisha wakiona wamekosea. Kisa cha kumuondoa, alifanya vibaya mchezo mmoja tu.

Mkikaa pamoja watu wengi mnaojua sana, mara nyingi mambo huharibika kwa kuwa kila mmoja hujibandika utaalamu na kutaka akubaliwe au kuheshimiwa kwa kile anachoamini.

Simba walikuwa wakali kuambiwa si sahihi kumuacha Tambwe. Waliamini wako sahihi, lakini walisema hawezi kufunga ameisha, sasa anaonyesha tofauti kabisa, unaweza kusema anawapiga msasa taratiiibuuu, wakiwa tayari kujifunza, watabadilika.

Mabao zaidi ya saba akiwa na Yanga katika michuano yote tangu ajiunge katika dirisha dogo, inaonyesha walibahatisha na lazima wajifunze si kumuangushia mzigo Phiri.


Kumsaidia kocha si jambo baya, lakini kushinikiza ili kufurahisha nafsi za wachache na kusahau maslahi ya klabu ni tatizo jingine kubwa.

Sura inajionyesha Yanga wana jicho sahihi kwa kuwa waliona Simba wakipotea njia kumuacha Tambwe, wakamuwahi njia, wakampa mshahara mara mbili ya ule aliokuwa akilipwa Simba na kumpangishia nyumba nzuri Sinza. Leo anawafanyia kazi vizuri na hata asipofunga, kazi yake imekuwa ikionekana kwamba alisaidiaje kikosi.

Sifa nyingine ya Tambwe ni mchezaji mwenye nidhamu ya hali ya juu, Simba wanalijua hilo na hawawezi kumlinganisha na wengine ambao sasa wanawasumbua kila siku mara wagonjwa, mara walitaka kurogwa, mara wamesusa hawajapangwa. Wajifunze, watafakari na kubadilika.


Mabao manne aliyoyafunga Tambwe katika Ligi Kuu Bara akiwa Yanga ni dhidi ya timu ambazo Simba haijashinda katika ligi. Amezifunga Azam FC wakatoka sare, halafu akaongoza ushindi wa Yanga dhidi Mbeya City, Kagera Sugar na Mgambo.

Enzi za kubahatisha, enzi za mmoja kutaka kujifurahisha bila kufanya tathmini za kitaalamu wakati wa usajili zimekwisha. Hakuna ubishi tena, hata kama itakuwa ndiyo mwisho wake kufunga juzi, lakini Tambwe anajua kufunga kuliko mastraika wa Simba na Simba walistahili kumbakiza si kukurupuka kama walivyofanya, jifunzeni.


1 COMMENTS:

  1. Nimesoma makala yako na nimeona niweke na mimi hoja zangu angalau na upande wa pili nao usikike. Kwanza ningependa nisema wazi kuwa mpira hauna fomula kama vile hesabu kwamba 2 jumlisha mbili dunia nzima jibu lake ni 4. Hii ina maana kuwa sio kweli kuwa mchezaji Fulani akiwa mzuri na timu moja basi atakuwa mzuri kwenye timu nyingine au kila timu atakayochezea. Mpira huchezwa na timu nzima na sio mtu mmoja na pale kila mmoja atakapotimiza wajibu wake utapata team work na matokeo bora.
    Mchezaji anaweza akawa mzuri kwa sababu ya ushirikiano mzuri wa wachezaji wenzake ambapo anaweza akahamia timu nyingine na asifanye vizuri kwa sababu haendani na wachezaji anaowakuta au ikawa kinyume chake kwamba alikotoka hakufanya vizuri na akafanya vizuri alikoenda. Mifano ya namna hii iko mingi sana na watu wa mpira wanaijua. Ndio maana narudia kusema hakuna formula katika mchezo huu.
    Sielewi kwa nini katika suala la Tambwe kuwe kuna lawama kwa Simba kwa kumuacha na sifa kwa Yanga kwa kumchukua kwa sababu Simba walimuacha kwa kuwa kweli alikuwa hafungi magoli na hata alipokwenda Yanga hakufunga magoli pia katika mechi nyingi tu. Siku zote mfungaji hupimwa kwa nafasi ngapi kapata na katumia ngapi na sio magoli mangapi katika mechi ngapi kwa sababu mara nyingi nafasi hutengenezwa na wachezaji wengine na sio mfungaji. Kama katika nafasi 10 anatumia moja binafsi siwezi kumuweka katika wafungaji wazuri ila kama katika nafasi 3 atatumia moja basi huyo ni mzuri.
    Unapenda sana kumtumia Phiri katika maelezo yake lakini ujue kuwa yule ni mtu ambaye hapendi lawama hata siku moja lakini siku zote maneno ya mtu huthibitshwa na vitendo vyake. Sasa kama ni kweli Phiri alikuwa anamuona Tambwe ni striker mzuri ungemuuliza basi ni kwa nini alikuwa akimtumia mwanzoni lakini taratibu akaanza kumweka pembeni kama substitute na baadaye akawa anampa dakika tano za mwisho. Huu si mwenendo wa kumtumia mchezaji mahiri bali ni wa kumweka kando mchezaji mzigo lakini naona wewe umeyapa uzito maneno yake zaidi ya matendo yake. Ilipofikia hatua hiyo ulitegemea uongozi ufanye nini zaidi ya kumuachia mchezaji akatafute riziki yake kwingine kuliko kumbakiza huku mkiona mchezaji aliyekuwa mzuri akiishia.
    Nilitegemea kuwa kwa kutambua hivyo mngeusifia uongozi wa Simba lakini badala yake mnawalaumu na kuwakejeli ati sasa wanammezea mate kama vile umewaona wakifanya vile. Sio kweli kuwa haukuwa sahihi uamuzi ule kwa kipindi kile na kama hali ingewezekana kujirudia basi uamuzi bado ungekuwa vile vile.
    Pengine pia ingefaa uangalie huko alikoenda ameanza kufunga lini na katika mfumo gani maana kacheza muda mrefu tu bila kufunga pengine hata wao na nyie mlianza kukubali kuwa labda ni kweli kapungua kiwango. Sasa hivi mfumo wa uchezaji Yanga umebadilika na wanatumia viungo watatu badala ya kutumia mashambulizi ya pembeni na ni mabadiliko hayo ambayo Tambwe ameweza kupata nafasi. Kuna msemo wa kiingereza unasema no situation is permanent na maamuzi mengi hufanywa na uongozi wakizingatia hali halisi ya wakati huo. Mara nyingi naona unapenda kuzungumza na Phiri na ukifanya hivyo tena si vibaya ukamuuliza ni kwa nini alifikia kumpa Tambwe dakika tano za mwisho na umahiri wake wote na pia si vibaya ukimuuliza pia ni kwa nini hakukubali kuwatumia Ndemla na Banda ambao sasa ndio tegemeo la Simba. Kama nilivyosema mwanzoni hakuna formula na zuri la leo ndio baya la kesho. Wakatabahu

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic