SHIRIKISHO la Soka Afrika (Caf) limetoa makundi na
ratiba ya kuwania kucheza Kombe la Mataifa Afrika mwaka 2017.
Katika ratiba ya makundi iliyotolewa na Caf, Tanzania
imetupwa Kundi G, ikiwa na vigogo wawili wa Afrika, Nigeria na Misri. Timu ni
nyingine ni Chad.
Kitendo cha Tanzania, Taifa Stars kupangwa na Nigeria na
Misri, tayari hofu imetawala miongoni mwa Watanzania wengi.
Katika mijadala niliyoisikia kuanzia katika mitandao,
makundi ya wadau wa soka na michezo mingine na wale niliojadiliana nao
wanafikiriaje, wengi wanaona hadithi ya Tanzania kuendelea kuiona michuano ya Afcon
kwenye ‘kideo’ itaendelea kama kawaida!
Wengi wanaamini hilo halina mjadala, wakiamini ni ndoto
Tanzania kuzipindua Misri na Nigeria na kuchukua nafasi ya kucheza Kombe la
Mataifa Afrika. Msisitizo wao, hadithi ya “kichwa cha mwendawazimu” inaonekana
kukosa mwisho.
Hofu hiyo inaonyesha dhahiri Watanzania hawaiamini Taifa
Stars inayoongozwa na Kocha Mholanzi, Mart Nooij. Kwa nini hawaiamini? Jibu
mwendo wake hata katika mechi za kirafiki umekuwa ni wa kusuasua sana.
Pamoja na mwendo kuwa wa kusuasua, bado Stars imekuwa ni
ileile, isiyokuwa na mabadiliko huku Nooij mwenyewe akionyesha kufurahia tu.
Tangu ameichukua timu hiyo kwangu nimekuwa sioni tofauti
ya Mholanzi huyo na Mdenishi Kim Poulsen ambaye angalau alionyesha imani kwa
wachezaji vijana ambao leo wamekuwa tegemeo katika ngazi za klabu na hata timu
ya taifa.
Unakumbuka alichokifanya kwa akina Simon Msuva na Frank
Domayo. Unakumbuka alivyowaamini akina Ramadhani Singano na hata Jonas Mkude.
Sasa ni tegemeo katika klabu mbalimbali na Stars pia.
Nooij amekuwa na mfumo wa “watu wazima” tena katika
mechi za kirafiki na bado timu yake imekuwa haina matokeo mazuri kwamba unaweza
kusema alimchagua Amri Kiemba badala ya Ibrahim Ajibu kwa kuwa alisaidia sana
timu ishinde mabao mengi kujiweka vizuri katika msimamo wa Fifa.
Bora ya sare ndani ukiwa na Ajibu kuliko Kiemba, bora
kupoteza ndani ukiwa unamtumia Salim Mbonde kuliko Aggrey Morris. Hawa
watakwenda baada ya muda kwa kuwa umri nao unawalazimisha.
Tanzania sasa inawahitaji vijana waje kufanya mabadiliko.
Uwezo wanao na wanahitaji kuanza kutumika sasa si kipindi tunaingia katika
mashindano dhidi ya Misri, Nigeria ndiyo wanapewa nafasi katika kikosi cha timu
ya taifa, haiwezi kuwa sawa.
Hofu kubwa inayowakuta wengi ni kwa kuwa hawaoni kama
kuna maandalizi kwa ajili ya kikosi cha baadaye au vijana wachache wenye mwanga
wa kusaidia hata baada ya akina Kiemba, Cannavaro na wengine kuondoka.
Tanzania itaendelea kuzihofia timu nyingine hadi lini?
Cape Verde, Rwanda na timu nyingine zimewahi kufuzu licha ya kuwa katika kundi
moja na timu ngumu kama Cameroon na nyinginezo.
Unapokuwa na jeshi bora, hakika hauwezi kuhofia vita.
Sisi tumekuwa waoga kwa kuwa tunaliona jeshi letu kwamba si imara namna ile na
hata ujengwaji wake umekuwa na walakini wa juu. Vipi watu watakuwa wana imani
ya kuona linakwenda vitani kupambana wasiwe na hofu?
Hofu isipotutoka Watanzania maana yake hatuwezi kushinda
kwa kuwa hatuwezi kuwa na uhakika wa asilimia mia kuzikwepa timu za Afrika
Magharibi na Kaskazini katika makundi.
Kufanikiwa ni lazima kukubali lazima tukutane nazo na
baada ya hapo ni kujiandaa vema, kujipanga sahihi ili kushinda dhidi yao.
Ukitaja timu bora kabisa za Afrika, hauwezi kuiacha
Algeria lakini usisahau kikosi cha Stars chini ya Kim Poulsen kiliionyesha kazi
ya kuitwanga kwa mabao 3-1 pale Taifa jijini Dar tena kikiwa na vijana
walioonekana kama wasingeweza.
Hata Cameroon, Misri, Nigeria wakikutana na Algeria
wanajua si kazi rahisi. Stars iliitungua. Hiyo ni picha kuonyesha kuwa
inawezekana lakini kwa maandalizi yanayoendelea sasa inatia shaka.
0 COMMENTS:
Post a Comment