Na Saleh Ally
BEKI wa Simba, Hassan Kessy, amekuwa shujaa katika macho
na masikio ya mashabiki wa soka nchini kutokana na uamuzi wake wa kususia
kuichezea Simba.
Kessy ameamua kuchukua uamuzi wa kujiondoa kambini na
kurejea kwao Morogoro kwa kuwa viongozi wa Simba wameshindwa kutimiza ahadi yao
ya kummalizia fedha zake.
Kessy alitakiwa kulipwa Sh milioni tano iliyobakia baada
ya kuwa amepokea Sh milioni 15 za awali katika fedha za usajili.
Sifa kwenda kwa Kessy ni nyingi, kwamba amechukua uamuzi
mzuri na sahihi huku wengi wakiwatupia lawama viongozi wa Simba kama
wababaishaji kwa kuwa wameshindwa kutekeleza ahadi.
Kessy amelalama kutolipwa fedha, lakini hakutafutiwa
hata nyumba aliyoahidiwa, hali iliyomfanya aishi kwa kutangatanga jijini Dar
kwa kuwa hakuwa na makazi!
Hilo pia ni kati ya mambo ambayo wadau wengi wa soka
wamekuwa wakiyapigia kelele, kwamba halikuwa sahihi na beki huyo ni shujaa kwa
kuamua kujiondoa.
Nilipoamua kuanza kufuatilia mkasa mzima, niligundua
meneja wa beki huyo, Athumani Shaaban ‘Tippo’ ndiye anatupiwa lawama kubwa na
viongozi wa Simba, kwamba anahusika kumshawishi Kessy.
Kwanza nianze na viongozi hao, kwamba hawapaswi kumlaumu
sana Tippo, kama meneja lazima awe upande wa Kessy kwa kuwa ni mchezaji wake.
Angeonekana ni mwendawazimu kama angelalia upande wa Simba na kumuacha Kessy.
Hivyo, kama Kessy ataamua “ujinga” au “sahihi”, Tippo
atabaki kuwa upande wa mchezaji wake na hawezi kuwa upande wa Simba.
Katika hili la kutimiza ahadi, bado naamini viongozi wa
Simba wamebabaisha na ilikuwa haina ujanja kwao zaidi ya kupambana na kutimiza
ahadi yao ya kumlipa kama walivyokuwa wameahidi. Inawezekana walichelewa, basi
ilikuwa ni vizuri kuzungumza naye kila mara kumueleza kuhusiana na mambo kwenda
vigumu.
Hakuna ubishi, kama wamechelewa, hawakusema lolote na
hawakuonyesha kujutia hilo, basi wamebabaisha mambo na wanapaswa kujifunza kwa
kuwa watu wanawaamini, basi waonyeshe wanapaswa kuaminiwa na wanaowaamini
hawajakosea hata kidogo.
Nikirudi kwa Kessy, nataka kupishana na wengi sana
wanaomuona beki huyo ni shujaa, kuwa amefichua uozo. Naona Kessy ndiye
aliyebabaisha zaidi.
Fedha alizotakiwa kulipwa ni haki yake, lakini kwangu,
naamini wakati mwingine kuna njia sahihi ya kudai kuliko kutanguliza mgomo
ambao hujenga picha tofauti kwa mtu yeyote, mfano “unaabudu fedha”, “una tamaa”,
“huna mapenzi hata kidogo na klabu” na mengine mengi.
Picha hiyo inayojengwa inaweza isiwe sahihi hata kidogo,
lakini namna unavyodai pia inaweza kuwa tatizo kwa kuwa lazima tukubali Simba
ni taasisi ambayo ina madeni kwa maana kwamba inadaiwa na kudai.
Jiulize, wachezaji wangapi wa Simba wanadai na
wanaendelea kucheza na katika mechi dhidi ya Kagera Sugar waliyocheza na
kushinda waliendelea kubaki na kuitumikia kwa moyo mmoja na nguvu zote hadi
ikashinda kwa mabao 2-1?
Kessy amejiunga na Simba katika dirisha dogo,
hajafikisha hata mwaka tangu ajiunge na Simba. Fedha anazodai ni za usajili kwa
mkataba wa miaka miwili. Hadi sasa hajatumikia hata nusu mwaka lakini
ameshalipwa asilimia zaidi ya 70 ya fedha zake za usajili.
Bado angeweza kumaliza hata msimu halafu baada ya hapo,
angeweka msimamo kwamba asingeweza kutokea kwenye kikosi utakapoanza msimu hadi
amaliziwe fedha zake kwanza lakini si sasa, yeye hajatumikia hata nusu msimu,
anagoma.
Sasa Simba inapambana bila yeye, wakati huu ndiyo ilimhitaji
na angeweza kuonyesha angalau kidogo anaweza kuipigania hata katika wakati
mgumu. Kuna ubaya?
Bado narudi kwake, ile ishu kwamba alikosa hata pa kuishi
kwa kuwa hakupewa nyumba! Viongozi wa Simba walikosea, hili lazima wakubali na
waachane na ahadi za hisia au hewa, badala yake watekeleze yaliyo katika
mkataba.
Lakini kwa Kessy inanishangaza! Alipokuwa Mtibwa Sugar,
mshahara haukuzidi Sh 350,000. Sasa Simba analipwa Sh milioni 1.5, kweli
anashindwa kutoa angalau Sh 300,000 akapanga chumba na sebule?
Sasa kwa mshahara huo, vipi anakubali kuishi maisha ya
kutangatanga wakati inaonekana mshahara wake umeongezeka mara tano?
Bado nashangazwa naye kutoona umuhimu wa kuendelea
kuishi kwa kujilipia wakati akisubiri Simba wamtafutie nyumba. Tena
ingewezekana kufanya nao majadiliano.
Kabla ya kufikia uamuzi wa kugoma, alizungumza na
viongozi wangapi wanaohusika na Simba na kuwaeleza hali yake ya kutokuwa na
furaha kuhusiana na mshahara wake?
Kweli tunamuona Kessy shujaa kwa kugoma, lakini shujaa
wa namna gani aliyeishi kwa kutangatanga huku akiwa na mshahara wa Sh milioni
1.5 kwa mwezi?
Wewe muajiriwa kama mimi, haujawahi kucheleweshewa
malipo hata mara moja? Wewe unayefanya biashara, haujawahi kucheleweshewa
malipo hata mara moja na wale wateja wako? Nikuulize, ulisusa hata mara moja?
Mbona bado unaendelea hadi sasa na maisha yanakwenda!
Matatizo kokote yataendelea kumkuta Kessy kwa kuwa hata
kule alikokuwa akilipwa Sh 300,000 pia waliwahi kumcheleweshea na alicheza hadi
mambo yalipotulia.
Leo anasusa yeye. Swali, kama akishalipwa na siku
akatokewa na tatizo, kweli Simba hawawezi kumsaidia nje ya mkataba wake kama
binadamu?
Tukumbuke kuna ambao Kessy amewakuta wanaichezea Simba, hadi
leo wanaendelea kuidai na wanaitumikia. Hivyo kazi kwa kuwa inahusisha binadamu,
haiwezi kuukimbia ubinadamu. Iko haja wakati mwingine kuangalia njia sahihi ili
kutatua matatizo yetu!
Maisha hayafanani na hakuna mtu mjinga kama anayefanya kwa kuiga!! Si sahihi Kessy kuendelea kuteseka kisa wenzake wanadai!! Kudai ni kudai tu na ukidai chako lazima utaonekana mbaya!! Kama Kessy ameona hiyo ndo njia sahihi basi asipangiwe jinsi ya kudai, hii ni kazi na hata wewe hapo Championi haufanyi kwa mkopo!! Kwanini wasimkope Okwi au Serrunkuma!!? Kwa sbb kessy ni mbongo!!?
ReplyDeleteKweli kaka umenena maana huyu Saleh Simba basi kwake ni kuandika habari za kuipamba timu yake na viongozi wake bila kujali upande wa pili.Yeye huyu Saleh ndiye aliyekuwa anashabikia Okwi kwenda msimbazi eti kwavile Yanga hawajamaliza deni lake,pia alishabikia kwa dhati na mwenzake Ngumbaru kwa Banda kusaini simba kwavile coastal haijatimiza masharti ya mkataba,sasa leo anakuwa kigeugeu kwa Kessy kisa timu ya mahaba yake Lunyasi ndiyo itakayoingia matatizoni.
Deleteyaani hawa washika kalamu ni matatizo mtupu,ndio maana bwana Yesu alisema enyi waamdishi na mafarisayo angalieni kalamu zenu zisiiteketeze dunia!Kalamu za waandishi zimepoteza watu wengi saana.
Sio suala la kusema hajamaliza mwaka. Kwani mkataba unasemaje? Bila ya wachezaji kama Kessy, uswahili wa viongozi wa timu zetu utaendelea milele. Inabidi wapatikane akina Kessy kama 10 kwa kila timu ndio watatia akili.
ReplyDeleteNi upuuzi kusema ajilipie nyumba kwa kuwa anapata 1.5m na kule Mtibwa alikuwa anapata 350,000 kwa mwezi. Akijilipia kodi ya nyumba kinyume na mkataba maana yake mshahara wake sio 1.5m tena.
Wakati mwingine viongozi wanasajili wachezaji wasio wahitaji ili mradi kukomouna na timu nyingine tu. Hivi Okwi asipotimiziwa atakubali? Kwa nini kwa mtanzania anayejitambua iwe nongwa?
mwandishi wewe ndio mbabaishaji mkuu, habari yako imelalia upande mmoja nafikiri kwa kiasi kikubwa nyie mnamchango wa kushusha mpira wetu, kwa kukusaidia tu hapo unaongelia kuhusu sharia za kazi kwa hiyo nivizuri ungefanya research yako kwanza kabla ya kuandika hisia zako, ule wakati wa kucheza mpira kwa mapenzi umekwisha ni ajira kama zilivyo nyingine hivyo mikataba inatakiwa kuheshimiwa. eti kwa kua mshahara wake umepanda basi ajilipie nyumba, waliweka kipengele cha kumlipia nyumba cha nini then?
ReplyDelete