Na Saleh
Ally
ALIYEWAHI
kuwa mdhamini mkuu wa Coastal Union, Nassor Bin Slum, ametangaza kurejea tena
na kuungana na viongozi wa klabu hiyo baada ya kukaa nje kwa miezi kadhaa.
Bin Slum
alikaa nje ya klabu hiyo baada ya kutoelewana na viongozi wa klabu hiyo, hali
iliyoanzisha mashambulizi kwenye vyombo vya habari, kila upande ukiulaumu
mwingine.
Kurejea kwa
Bin Slum kwa mara nyingine kumezua gumzo kubwa, wengine wakisema uongozi
umekwama, ndiyo maana umeamua kumrejesha maana kikosi hicho kilikuwa kinateremka
daraja.
Yeye
anasema ameamua kurejea katika klabu hiyo kutokana na mapenzi yake na si kwamba
sasa ni mdhamini tena. Katika mahojiano maalum na Championi Ijumaa, Bin anafunguka:
Kipi kimekufanya urejee Coastal, uliacha kitu labda?
Bin Slum:
Kwanza nifafanue, nimerudi Coastal kama shabiki na mwanachama, si kama mdhamini
kama ilivyokuwa awali. Nimekuwa nikiifuatilia timu, kipigo dhidi ya Prisons
nyumbani, nikagundua inateremka daraja, maana naijua Coastal.
Unaweza kufafanua unaijuaje?
Bin Slum:
Msimu uliopita, mechi tano za mwisho tulivurunda. Bahati nzuri tulikuwa
tumefanya vizuri mwanzoni, ikatusaidia.
Kabla ya kurejea, ulifanya tathmini na kujua tatizo ni
nini?
Bin Slum:
Mchawi wa haya wanajua wachezaji na viongozi, ila viongozi wana tatizo zaidi
pia. Wanakuwa wamejiwekea malengo ya kufanya vizuri, wanapofeli, huanza
kutafuta mchawi na mzigo ni kwa wachezaji.
Nilirudi
katika mechi dhidi ya Yanga. Msisitizo wangu ulikuwa ni kurudishwa kwa
wachezaji. Niliomba warejeshwe ili kupambana na Yanga, lengo tusahau
yaliyopita.
Coastal
ilikuwa haina wachezaji wengi kama Mbwana Hamis ‘Kibacha’, Joseph Mahundi,
Tumba Sued na Selemani Kibuta. Utasikia Julio alisema tumeshitukizwa, lakini
ukweli waliocheza siku hiyo walikuwa vijana wengi, ni rahisi kupoteza dhidi ya
Yanga iliyo sawa.
Viongozi
hawakulisikiliza hilo, tukafungwa nane. Ukawa wakati mzuri wa kuwakumbusha,
nashukuru sana wakakubali kuwarudisha wachezaji wazoefu na kweli wakasaidia
mechi iliyofuata dhidi ya JKT, tukashinda kwa mabao 2-0 kule Chamazi.
Unafikiri malengo ni tatizo pia?
Bin Slum:
Malengo ni kitu kizuri, lakini viongozi wanakuwa na hofu ya kufeli. Hata mwaka
huu, Coastal ilijiwekea malengo ya kuwa bingwa, mwisho mambo yamekwenda
tofauti. Badala ya kulumbana, vema kukaa na kutathmini kwa pamoja.
Unakumbuka
hata msimu walipofukuzwa akina Juma Nyosso na Crispine Odulla, Haruna Moshi ‘Boban’
akajitoa. Baada ya hapo, timu ikaanza kuyumba. Nafikiri kuliko kulaumiana,
kurekebishana ni jambo bora zaidi.
Msimu huu,
kipa mzoefu kama Shabani Kado pia hakuwa akipangwa. Kuna mambo mengi, lakini
binadamu mnapokuwa pamoja lazima mkubali kuvumiliana, kurekebisha na kwenda
pamoja.
Umerudi Coastal sababu ya mapenzi, ulikaa kando kwa
sababu ya chuki?
Bin Slum:
Sina chuki na Coastal, ila nina chuki na wale wanaofanya ifeli. Sina kinyongo
nao, ndiyo maana wanapokosea ninasema bila ya woga. Mimi ni mwanachama wa
Coastal, nina haki, niliamua kukaa kando kwa kuwa sipendi malumbano.
Uchaguzi unakaribia, unafikiri nini bora cha kufanya
ili kutengeneza Coastal imara?
Bin Slum:
Swali zuri sana, kwanza lazima viongozi wa makundi yote yanayokubaliana na
yanayopingana wakutane pamoja. Wanaweza kumualika hata mkuu wa mkoa kama mlezi
au mtu muhimu, wakazungumza na kukubaliana.
Wasahau
yaliyopita, wapeane mikono na baada ya hapo wapendekeze viongozi wanaoamini
wakigombea na kushinda wataisaidia timu na klabu kwa ujumla.
Vipi wewe kuhusu nafasi yoyote ya uongozi ili uisaidie
timu na klabu?
Bin Slum:
Sina mpango wa kugombea, wala sina mtu ninayemuunga mkono kwa maslahi binafsi.
Nitawaunga mkono wote wenye lengo la kusaidia klabu. Tunahitaji viongozi imara
kwa manufaa ya klabu yetu, hiyo ndiyo furaha ya kila mwana Coastal.
Coastal ikishinda mechi dhidi ya Stand United,
itajiweka katika mazingira ya kukwepa kushuka. Wewe ni shabiki wa Coastal na
mdhamini wa Stand, hapo vipi?
Bin Slum:
(Tabasamu) Kweli mimi shabiki na mwanachama wa Coastal lakini Stand
inadhaminiwa na Bin Slum Tyres Ltd kupitia bidhaa za Double Star. Hii ndiyo
tofauti, ni vitu viwili tofauti kabisa.
Wana Kimanumanu African Sports wamepanda, nyie Coastal
mmejiandaa kweli?
Bin Slum:
Ndiyo maana tunapambana Coastal ibaki ili tuone Tanga derby ambayo
hatujaishuhudia kwa miaka 23 sasa. Kumbuka familia ya Bin Slum ilipambana kuona
Sports inarejea ligi kuu.
Lengo ni
kurejesha ushindani na changamoto katika soka la Tanga. Ndiyo maana
nilikuambia, utaipandisha Sports halafu uiache Coastal iteremke? Haiwezekani
hata kidogo!










0 COMMENTS:
Post a Comment