Mshambuliaji mkongwe wa zamani wa Simba, Mussa
Mgosi, amekifumua kikosi cha timu hiyo kwa kutoa mapendekezo ya kusajili
wachezaji watatu.
Mgosi ametoa kauli hiyo baada ya Simba
kushindwa kutwaa taji la Ligi Kuu Bara kwa mwaka wa tatu sasa.
Mgosi ambaye sasa anakipiga Mtibwa Sugar,
aliiwezesha Simba kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara mwaka 2010 huku akiibuka
mfungaji bora kwa kufunga mabao 18, lakini baadaye aliiacha timu hiyo na
kutimkia DC Motema Pembe ya DR Congo kabla ya kurudi Bongo.
Mgosi alisema kuwa kati ya nafasi ambazo Simba
wanatakiwa kuziboresha ni safu ya ulinzi ya kati, kiungo na ushambuliaji.
Mgosi ambaye aliwafunga Simba katika mchezo wa
mzunguko wa kwanza Morogoro, walipokutana msimu uliopita wa ligi kuu, alisema
safu ya ulinzi ni butu inayohitajika kuimarishwa ili kuhakikisha hawaruhusu
mabao.
Aliongeza kuwa, pia timu hiyo inatakiwa
kusajili mshambuliaji mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao baada ya
kumuacha kimakosa Mrundi, Amissi Tambwe.
“Ni ukweli ulio wazi kabisa, viongozi wa Simba
walikosea kumuacha Tambwe ambaye msimu uliopita alikuwa mfungaji bora na
kumsajili Sserunkuma (Danny).
“Hapo ndipo Simba walipokosea hesabu zao za
ubingwa msimu huu uliomalizika, hivyo wanatakiwa kusajili mshambuliaji mwingine
mwenye uwezo mkubwa wa kufunga mabao.
“Pia wasajili kiungo mmoja atakayemchezesha
mshambuliaji huyo mpya watakayemsajili, pia wanatakiwa kusajili mabeki wawili
wa kati wenye uwezo mkubwa,” alisema Mgosi.
0 COMMENTS:
Post a Comment