BIN KLEB (KULIA) AKIWA NA TENGA (KATIKATI) NA BIN SLUM. |
Na Saleh Ally
WAKATI Yanga inaanza
kujivunia kuwa na moja ya vikosi bora chini ya uongozi wa Yusuf Mehbuub Manji,
kuna watu hawawezi kusahaulika.
Wanaweza kuwa wengi lakini
mmojawao ni Abdallah Bin Kleb ambaye aliwahi kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Usajili ya Yanga.
Kati ya wachezaji
aliopambana kuwasajili ni pamoja na Haruna Niyonzima, Kelvin Yondani, Mbuyu
Twite, Juma Kaseja, Ally Mustapha ‘Barthez’, Deogratius Munishi ‘Dida’,
Emmanuel Okwi na wengine wengi.
Bin Kleb akishirikiana na
Seif Ahmed ‘Magari’ pamoja na wajumbe wengine, waliongoza mapinduzi kwa mara ya
kwanza Yanga kuwa na timu kali ya usajili, yenye kuweza fitna.
Awali, suala la fitna za
soka, wachezaji wazuri wengi walichukuliwa na Simba na hasa kama ukizungumzia
lile Kundi la Friends of Simba (Fos) ambalo lilikuwa likimtaka mchezaji au
kocha, hachukui muda wala hawezi kukwepa.
Kipindi cha kamati ya
usajili ya Bin Kleb, mambo yakawa tofauti na sasa ikaonekana hata Fos nao
waliingia hofu, kwani mara kadhaa walijikuta wakiangushwa kwenye usajili wa
wachezaji waliowataka na Yanga ikafanikiwa kuwanasa.
Chini ya uongozi wa Manji
na kikosi cha Bin Kleb, Yanga ilianza kujijenga zaidi na kuifanya kuwa imara
hadi sasa ni tishio.
Ilionekana kazi iliyowashinda ni moja tu, kuwafunga Simba.
Wakati Wanayanga
wakionekana kuwa na furaha, ghafla Bin Kleb na Seif ‘Magari’ wakapotea na
taarifa zikawa zinaeleza kwamba wamebanwa na majukumu ya kifamilia pamoja na
biashara zao.
Ilielezwa wawili hao,
mpirani tu ni nadra kwenda na unakumbuka wakati fulani Bin Kleb aliwahi
kumuomba Manji asimteue kwenye kamati yoyote kutokana na kubanwa kwake na
majukumu.
Huenda Wanayanga wangependa
kujua kiongozi wao huyo aliyekuwa mchapakazi yuko wapi na tatizo lake nini
akaitupa kando klabu yake ambayo sasa inaonekana kwenda na mwendo mzuri.
SALEHJEMBE: Inaonekana kama
umeikimbia Yanga. Je, kuna tatizo lolote?
Bin Kleb: Hapana, hakuna
tatizo ni kutokana na kubanwa na majukumu tu ya kikazi pia familia.
SALEHJEMBE: Lakini yote hayo
yalikuwepo wakati ule, vipi sasa?
Bin Kleb: Kweli, lakini
siku zinapishana ndugu yangu. Wakati mwingine majukumu yanazidi zaidi. Hivyo
nimeona ni wakati mzuri kuyatekeleza.
SALEHJEMBE: Iwapo Yanga watakuja
na kuomba ushirikiano wa jambo fulani, uko tayari?
Bin Kleb: Siyo wakija, hata
sasa nimekuwa nikishirikiana nao katika mambo kadhaa. Ni jambo la kawaida
kabisa, inategemea na nafasi yangu. Maana sasa mara nyingi nakuwa nje ya nchi kikazi,
lakini nikiwa hapa, tunashirikiana vizuri kabisa.
SALEHJEMBE: Labda mwenendo
wa Yanga kwa kipindi hiki unakuridhisha?
Bin Kleb: Hakika Yanga
inakwenda vizuri kabisa. Uongozi ni imara, kikosi ni kizuri na ina kocha bora.
SALEHJEMBE: Kwa sifa hizo,
unaona inaweza kuendelea kufanya vizuri kwa msimu huu mpya au ndiyo zamu ya
Simba?
Bin Kleb: Yanga ina nafasi
kubwa ya kufanya vizuri. Utaona tangu timu tuliyoisajili, mabadiliko ni kidogo
sana. Maana yake ina wachezaji waliozoeana na kocha ni bora, pia muunganiko
wake na msaidizi wake (Charles Boniface Mkwasa) umekubali na unafanya kazi
vizuri.
SALEHJEMBE: Hauoni kuwa huu
unaweza kuwa ni msimu wa Simba ambao wanaonekana kujipanga zaidi?
Bin Kleb: Sidhani, Simba
hawawezi kufanya vizuri labda baada ya miaka mingine mitatu. Mpinzani mkubwa wa
Yanga ataendelea kuwa Azam.
SALEHJEMBE: Simba
hawajashika hata nafasi ya pili kwa misimu mitatu sasa, unafikiri watakubali?
Bin Kleb: Hawana ujanja,
utaona Yanga na Azam wana timu zilezile na zimeboreshwa tu na hilo ndiyo jambo
zuri. Tofauti na Simba, makocha wapya, wachezaji wapya. Ingawa kweli mpira
unaweza kubadilika lakini sidhani kama wataweza kuwapita Yanga na Azam na kuwa
mabingwa.
SALEHJEMBE: Timu nzuri
ndiyo, lakini uongozi ukiwa bora hauoni unaweza kusaidia kuleta mabadiliko na
kuisaidia timu kufanya vizuri hata kama haikutegemewa?
Bin Kleb: Kweli, hilo
linawezekana. Lakini uongozi wa Yanga ni imara pia. Tena Yanga wana bahati,
hawana watu wengi lakini wanaweza kufanya kazi zao kwa ufasaha, maana
wanasikilizana.
SALEHJEMBE: Unaamini Simba
hawasikilizani au kuna tatizo?
Bin Kleb: Raha ya Simba
wana watu wengi sana kwenye uongozi, unaweza kusema wanajua mpira, si kama
Yanga. Lakini wana tatizo la kila mmoja kuwa anajua kuliko mwingine, hilo nalo
linawaangusha pia.
SALEHJEMBE: Ukiachana na
hilo, Yanga haionekani kama inatoa nafasi ya kukuza viongozi makinda ambao
wataisaidia baadaye. Nini maoni yako katika hili?
Bin Kleb: Hilo naungana na
wewe, Yanga haina watu wengi kwa kuwa hapo awali hakukuwa na utaratibu huo.
Lakini sasa angalau utaona wapo vijana na baadaye watakuwa msaada kwa klabu
baada ya miaka kadhaa.
SALEHJEMBE: Pamoja na yote
mazuri au mwendo mzuri, unafikiri nini hasa tatizo la Yanga imeshindwa kuifunga
Simba?
Bin Kleb: Unajua Yanga
imekuwa na wachezaji walewale kwa kipindi kirefu. Baadhi wamo wale waliofungwa
mabao 5-0 na Simba. Hivyo bado wameathirika kisaikolojia na hofu inawatafuna.
SALEHJEMBE: Nini sasa
kifanyike?
Bin Kleb: Nafikiri Yanga
waendelee kuimarisha ubora wao wa kazi. Iko siku wataipatia Simba, kuanzia hapo
mambo yatabadilika.
SALEHJEMBE: Labda lini
unatarajia kurejea tena na kuungana na Yanga kama zamani?
Bin Kleb: Niko na Yanga
kila ninapopata nafasi. Ikiwa nitapata nafasi zaidi, basi nitaongeza muda zaidi
wa kuwa na wenzangu, tushirikiane kusukuma gurudumu la Yanga.
0 COMMENTS:
Post a Comment