KATIKA
soka la wenzetu, ndani na nje ya Bara la Afrika, chimbuko kubwa la wachezaji
mastaa ni shule za kukuza na kuendeleza vipaji, maarufu kama akademi.
Mifano
ni mingi sana kwa orodha ya wachezaji wanaofanya vizuri katika ngazi ya
kimataifa ambao chimbuko lao ni kwenye akademi.
Lakini
kwa Tanzania, kidogo kuna utofauti. Ishu za akademi zimebaki kwenye makaratasi,
kiutendaji ni ziro! Labda kwa kizazi cha sasa. Zaidi ya 80% ya nyota wa
kipindi hiki wametokea katika soka la mchangani, maarufu kama ndondo!
Unajua
michuano ya mchangani inavyoandaliwa? Viingilio vyake ni vya chini lakini
inavuta watu wengi na nyota wanaocheza katika timu kubwa nao hulipwa ili kwenda
kushiriki.
Katika
chimbuachimbua ya Championi Jumamosi, imebainika kuwa, wachezaji wa klabu kubwa
za Yanga, Simba na Mtibwa ndiyo wanaoongoza kucheza katika ndondo licha ya
kulipwa angalau vizuri.
Uchunguzi
unaonyesha wapo wanaofuata fedha kutokana na dau kubwa wanalopewa au wengine
wanalazimika kufanya hivyo kwa kuwa wanazichezea timu za mtaani kwao.
Mechi
za mchangani hazina msimu, kamwe haziishi, ikiisha michuano ya mbuzi, inafuata
ya jezi, ng’ombe na kadhalika. Hivyo kuwafanya wachezaji kuwa ‘busy’ wakati
wote wa msimu.
Nyota
wengi wanaingiza fedha nyingi, wakati mwingine hata kuliko wanazolipwa katika
klabu zao ili mradi ni kulingana na mechi wanazocheza kwa maana ya idadi na
eneo gani.
Kwa
mujibu wa utafiti wa gazeti hili, wafuatao ni nyota wa ligi kuu waliojiandikia
majina makubwa kwenye ndondo na huwa ni nadra sana kukosekana katika michuano
ya ndondo.
Uchunguzi
unaonyesha nyota hawa hukodiwa kwa gharama tofauti na vigezo tofauti. Kwanza ni
kulingana na kiwango cha mchezaji mwenyewe na pili ni kulingana na hatua ya
michuano yenyewe.
Kima
cha chini cha kumshawishi mchezaji wa Ligi Kuu Bara, hususan kwa timu kubwa
hadi aweze kucheza, huanzia 50,000 na hupanda kadiri ya hatua za michuano
ilivyo. Hatua ya fainali kwa 90% wachezaji hawa hulipwa kuanzia 80,000 hadi
laki moja!
Baadhi
yao ni Mussa Hassan ‘Mgosi’ (Mtibwa Sugar), Hussein Sued (Coastal Union), Salum
Aboubakary ‘Sure Boy’ (Azam), Said Ndemla (Simba), Ibrahim Ajibu (Simba), Jerry
Tegete (Yanga), Salum Machaku (Polisi Moro), Issa Rashid ‘Baba Ubaya’ (Simba),
Omega Seme (Yanga) na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ wa Simba.
Wengine
ni Juma Nyosso (Mbeya City), Rashid Mandawa (Kagera Sugar), David Luhende
(Mtibwa Sugar), Nizar Khalfan (Yanga), Hamad Kibopile (Mbeya City), Salum
Telela (Yanga), Abdallah Seseme (Simba), Gideon Brown (Ndanda), Said Morad
(Azam) na Mussa Nampaka wa Mtibwa.
Pia
wamo Abasirim Chidiebere (Stand United) na Nassor Masoud ‘Chollo’ (Simba),
Godfrey Wambura (Coastal Union), Juma Seif ‘Kijiko’ (Ruvu Shooting), Kessy
Mapande (JKT Ruvu) na wengine wengi wa timu za ligi kuu.
Kimahesabu
supastaa anayeweza kukodiwa kuanzia hatua ya makundi mpaka fainali, katika
michuano yenye hatua tano, yaani hatua ya makundi, 16 bora, robo fainali, nusu
fainali na fainali, ana uwezo wa kukunja si chini ya laki nne.
Iwapo
fedha hizo ataingiza ndani ya mwezi mmoja, maana yake anakuwa amechukua nusu ya
mshahara wake kama anacheza Yanga, Simba au Azam FC. Lakini anaweza kubeba
zaidi ya mshahara wake kama anacheza timu ndogo kama za JKT Ruvu, Stand United,
Ndanda FC na nyinginezo.
Inaonekana
Jerry Tegete na Mussa Hassan Mgosi ni kati ya wachezaji ghali kwa kukodiwa
mchangani kwani huanzia Sh 60,000 kwenye hatua ya makundi. Mastraika hao
huchukua hadi Sh 100,000 au zaidi ili wacheze mechi ya fainali.
Kiwango
kama hicho ndiyo cha mastaa kama Luhende, Nyosso, Morad, Sure Boy na Hussein
Sued ambaye anatajwa wakati mwingine hugombaniwa kutokana na umahiri wa kucheka
na nyavu huko mchangani. Aliwahi kuwa mfungaji bora mara mbili.
Timu
vinara wa kukodi mastaa:
Kuna
timu za mchangani vinara kumwaga mamilioni kwa mastaa wa Ligi Kuu Bara, baadhi
ni hizi hapa; Vegetable, Morning Stars, Daladala Camp, Saigon FC, Tabata FC,
Muheza FC, Segerea United, Yakuza FC na Burudani FC.
Viwanja
maarufu mchangani:
Utafiti
umebaini kuwa, mastaa hawa hupiga madili yao katika viwanja mbalimbali, lakini
maarufu zaidi ni; Toto Tundu (Segerea), Mwananyamala B (Mwananyamala), Tabata
Shule (Tabata), Shule ya Benjamin Mkapa (Kariakoo), Sigara (Temeke), Beira
(Kigogo), Bandari (Tandika), Kinyerezi na Vinyago uliopo Mwenge.
0 COMMENTS:
Post a Comment