Na Saleh Ally
REKODI ya Kocha Mart Ignatus Maria Nooij raia wa Uholanzi inaonyesha
ameifundisha Taifa Stars na kuiongoza kucheza mechi 18 tu kabla ya kutimuliwa.
Nooij alitua nchini Agosti 28, 2014 na kuanza kazi. Katika mechi
hizo 18, kashinda tatu! Sare 6 na kapoteza 9.
Kimahesabu utagundua ameshinda mechi chache kuliko vipigo, ana sare
chache kuliko vipigo. Maana yake ameshinda mechi chache zaidi na alistahili
kutimuliwa ikiwezekana mara tu baada ya michuano ya Cosafa nchini Afrika
Kusini.
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limefikia uamuzi wa kumuondoa
Nooij baada ya kuchapwa mabao 3-0 dhidi ya Misri na wiki mbili baadaye yaani
juzi akachapwa mabao 3-0 na Uganda.
Mechi dhidi ya Misri ilikuwa ni kuwania kucheza michuano ya Afcon
ambako timu nyingine ni Nigeria na Chad.
Mechi ya pili ya Uganda ilikuwa kuwania kucheza Chan, kwa mabao hayo
matatu, maana yake nafasi ni finyu na kinachotakiwa ni kuepusha aibu kubwa.
Hatuwezi kudanganyana kwa kikosi tulichonacho sasa twende tukashinde
nne. Kama tunapambana kushinda tatu na kutafuta kwenda kwenye mikwaju ya
penalti hapo sawa.
Lakini kupoteza tatu nyumbani, tumejiweka kwenye zaidi ya wakati
mgumu na nafasi ya Tanzania kusonga mbele Chan sasa ni asilimia 15 hata kama
mpira unadunda. Sidhani kama Uganda watakuwa “wa kulala” kama sisi, watupe
nafasi hiyo.
Pia makocha watakaopewa timu, hawatakuwa na nafasi ya kutosha na
hakutakuwa na sababu ya kuwalaumu.
Ukiangalia nafasi ya Chan, ndiyo imekwenda hiyo, lakini hata ile ya
Afcon unaweza kusema hatunayo tayari. Kawaida ni mechi sita na tayari ya kwanza
tumepoteza kwa mabao 3-0.
Tunajiamini kuifunga Misri hapa nyumbani? Kweli tumejiandaa vya
kutosha katika mechi mbili dhidi ya Nigeria na uhakika upi tulionao wa
kuishinda Chad!
Tunaingia kwenye mashindano na kocha na benchi jipya la ufundi.
Lazima tukubali Nooij alipaswa kuondoka mara moja baada ya michuano ya Cosafa.
Anaondoka sasa, anaondoka na Afcon na Chan na sasa Tanzania
italazimika kusubiri zaidi ya miaka mingine mitatu kuanza kuwania kucheza tena
katika michuano hiyo.
Nguvu kubwa ihamie kwenye Kombe la Dunia lakini bado kama umepoteza
Chan na Afcon, jiulize nafasi yako Kombe la Dunia inakuwaje?
Suala la Nooij linatufunza
mambo mawili na lazima tukubali kwamba wakati mwingine urafiki na Woga si mambo
mema linapofikia suala la utaifa.
Wako wenye urafiki na Nooij ndani ya TFF, huenda walikuwa
wakifaidika kimaslahi kutokana na kuwepo kwake au ulikuwa ni urafiki wa kawaida.
Linapokuja suala la utaifa, walipaswa kuwa wakweli.
Pili ni woga. Kwamba akiondoka itakuwaje na nani ataweza! Si sahihi,
kama angetolewa mara tu baada ya Cosafa, huenda ingesaidia kupandisha morali
upya kwa wachezaji kupitia kocha mpya kwa kuwa kila anayecheza angetaka
kumuonyesha anastahili kuwepo Stars.
Woga ndiyo umefanya Nooij abaki hadi kututia katika tope na sasa
inaonekana wazi Chan na Afcon ni ndoto.
Wachezaji:
Waingereza wanasema, “No victory without sacrifice”. Kweli, hakuna
ushindi bila ya kujitolea. Sasa hapa ni mawili, watuambie hawakujitolea vizuri
au ndiyo uwezo wao mdogo.
Hakika tumeona matatizo kwa kocha, ndiyo maana rekodi yake ni mbovu
tangu ametua Tanzania na sasa ameondoka.
Katika soka, kuna uwezo binafsi ambao pia ni msaada. Vipi wachezaji
hata kama wanaona kocha wao hana lolote wanashindwa nao kuonyesha uwezo binafsi
ili kulisaidia taifa lao?
Kwa nilivyowaona, niliona hawajiamini, hawakuwa tayari kwa lolote na
walicheza utafikiri wanaitumikia klabu ambayo wanajua wakitaka wanahamia
nyingine.
Timu ya taifa haina usajili, timu ya taifa ni moyo na utaifa ndiyo
utambulisho wa utu wako. Wakati mwingine nafikiri vizuri hata kuanza upya pia
na kikosi hicho cha timu ya taifa.
Kuna kila sababu ya wachezaji wa Stars kutambua umuhimu wa jezi ya
timu ya taifa. Ni sawa na askari anayelipigania taifa lake, acheni ubishoo.
Rutayuga:
Mshauri wa ufundi wa Rais wa TFF, Pelegrinus Rutayuga yeye amebaki.
Hili ni kosa jingine na kwa utaratibu yeye alikuwa anashughulikia mambo mengi
ya timu na kiufundi.
Kama atakuwa hashiriki, basi lazima anajua upatikanaji wa Nooij,
uteuzi wa benchi la ufundi na vinginevyo kwa kuwa yeye ndiye anamshauri Malinzi
katika masuala ya ufundi.
Kufeli kwa Nooij na benchi lake la ufundi, maana yake hata yeye
amefeli. Kumbakiza ni kujidanganya kwa kuwa ni sawa na kupalilia magugu, halafu
ukaliacha lile gugu mzazi. Litazaa tu tena.
Ili kuanza upya tena bila ya kuhofia kuonekana kuwa ni kuanza
mwanzo, lazima Rutayuga aondoke ili kama ni mshauri, basi aje mwingine.
Kumbakiza yeye na kuingiza benchi jipya la ufundi, tena kwa ushauri
wake yeye, hakika ni kufeli kwa mara nyingine.
Huu ndiyo wakati wa Malinzi kuonyesha ujasiri halafu afanye kazi kwa
ajili ya taifa. Asihofie kuwa atamkasirisha Rutayuga huku akiwa anawaudhi
Watanzania zaidi ya milioni 25 wanaopenda mchezo wa soka.
SOURCE:
CHAMPIONI
0 COMMENTS:
Post a Comment