RUTAYUGA (KULIA) AKIFAFANUA JAMBO MBELE YA NOOIJ, SALUM MADADI NA BOSI WAO KATIBU MKUU WA TFF, MWESIGWA SELESTINE. |
SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) limefikia uamuzi wa kumfuta kazi
Kocha Mart Ignatus Maria Nooij pamoja na kuvunja benchi lote la ufundi.
Kamati ya utendaji ya shirikisho hilo limefikia uamuzi huo ikiwa
imechelewa mara tu baada ya Taifa Stars kuendelea kufungwa hovyo.
Hiyo ilikuwa ni baada ya kupokea kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa
Uganda ikiwa ni harakati za kuwania kucheza Michuano Kombe la Afrika kwa
Wachezaji wa Ndani (Chan).
Stars ilikuwa nyumbani kwenye Uwanja wa Amaan mjini Zanzibar
ilipokutana na kipigo hicho. Hii ni aibu.
Wakati TFF wanafikia uamuzi wa kumuondoa Nooij pia kufuta benchi la
ufundi, mimi naona kama wanampigia mbuzi gitaa bila ya kujua.
Wanamuondoa Nooij ambaye alionekana ni tatizo, hakika alikuwa ni
tatizo, kocha asiyekuwa na mipango dhabiti kuhakikisha Stars inafanya vema,
zaidi ya kujisifia mara kadhaa kuhusiana na umahiri wake katika kunywa bia.
Nooij na benchi lake la ufundi wanaondoka, vipi hiyo Kamati ya
Utendaji ya TFF au rais wake, Jamal Malinzi anajisahau kuwa Pelegrinus Rutayuga
amesahaulika na yeye kama ataendelea kubaki basi atakuwa ni tatizo.
Ingawa cheo hicho hakikuwepo, baada ya kuingia kwa uongozi mpya,
kikaanzishwa na Rutayuga sasa ni Mshauri wa Ufundi wa Rais wa TFF, Malinzi.
Ukitaka kujua anamshauri lipi, labda umtafute.
Rutayuga hakuwahi kucheza soka katika kiwango cha juu, hajawahi kuwa
kocha wa timu kubwa ndani au nje ya nchi!
Huyo Rutayuga, hajawahi kusomea ukocha kwa kiwango cha chini, kati
au juu. Sasa huwa anamshauri nini Rais wa TFF? Inawezekana kabisa kusema haya
madudu yanayotokea ndiyo sehemu ya ushauri wake.
Kama ni hivyo, hasa ukizingatia amekuwa kati ya watu wa karibu wa
timu, kila kitu kimefeli. Kocha na benchi lake la ufundi wanaondolewa. Vipi
yeye anabaki?
Ndiyo maana nimeamua kuweka msisitizo kwamba, kama Rutayuga anabaki,
TFF itakuwa inampigia mbuzi gitaa. Mwisho, kuliondoa benchi lote la ufundi
itakuwa ni kazi bure.
Lazima tukubali, kama Rutayuga ni mshauri wa Rais wa TFF, kila kitu
kimefeli, maana yake ushauri wake haukuwa na tija ndiyo maana mambo yamekwenda
mrama.
Tena utaona, Rutayuga alikuwa pia ni tatizo kwa kuwa alishindwa
kumshauri vizuri Malinzi baada ya Stars kuboronga kule Afrika Kusini katika
michuano ya Kombe la Cosafa.
Ule ulikuwa ndiyo wakati mwafaka wa kumuondoa. Badala yake akabaki
na sasa ameiondoa Tanzania katika michuano yote ya Caf kwa kuwa sasa hakuna
matumaini tena ya kufuzu Afcon wala Chan.
Kama angekuwa ni mzuri au mwenye mambo ya uhakika, Nooij angeondoka
mapema na huenda 3-0 dhidi ya Misri na 3-0 dhidi ya Uganda zingeweza kuepukika.
Nilimsikia Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi ya TFF, Wilfred Kidau
akimtetea Rutayuga, nikashangazwa sana na kuamini kweli Taifa Stars si utaifa
kwa wengine. Ajabu, Kidau huyohuyo, nikasikia akisisitiza Nooij aliipeleka timu
ya taifa ya vijana ya taifa fulani la Afrika Kombe la Dunia, aliipeleka
Msumbiji Afcon.
Sijui alikuwa ana maana gani, tena akizungumza huku anatokwa povu
utafikiri anazungumza jambo la maana. Sasa sisi tufungwe tatu-tatu, halafu
tuendelee kujipoza na kufuzu kwa timu nyingine kucheza Kombe la Dunia la vijana
na Afcon? Hivi hawa wanajitambua kweli?
Sasa Kidau ainue mdomo wake tena kumsifia Rutayuga na Nooij kama
alivyofanya. Naamini kabisa, wengi waliomzunguka Malinzi ni tatizo na kuna kila
sababu ya yeye kulitazama hili.
Kama ilikuwa ni “kulipana” kwa kuwa walimsaidia katika uchaguzi,
sasa imetosha kwa kuwa wanamuangusha, wanaliangusha taifa pia na ile timu si
yao binafsi, ni ya Watanzania.
Hivyo, vizuri TFF ya Malinzi, baada ya Nooij na benchi la ufundi.
Basi, afuatie Rutayuga ambaye ananikumbusha kipindi kile alipokuwa meneja wa
timu, Serengeti Boys ikaondolewa mashindanoni kwa kumchezesha Nurdin Bakari.
NAJUA SALEH UNAOGOPA KUTUMIWA CHATU NDIO MAANA UNAOMBA HUYO RUTA NAYE AONDOLEWE,HAWA WATU WA ZIWA MAGHARIBI MIMI NAWAOGOPA SANA KWA FITNA ZA KIMAZINGARA!
ReplyDelete