Na Saleh Ally
MWAKA
2003, Denis Oliech akiwa na umri wa miaka 17 tu, aliingia katika kipindi cha
pili katika mechi dhidi ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ na kuisaidia Kenya
‘Harambee Stars’ kubeba ubingwa wa Kombe la Cecafa kwa kuishinda Kilimanjaro
Stars.
Kocha
Mkuu wa Tanzania, James Siang’a ambaye ni raia wa Kenya, alijua kabisa
kwamba kuna hatari ya Oliech. Lakini aliwaamini mabeki wake wa kati, Boniface
Pawasa na Lubigisa Lubigisa ambao walikimbizwa na Oliech kuanzia katikati ya
uwanja pale CCM Kirumba kabla hajamchambua Juma Kaseja na kuandika bao la tatu
na kuifanya Kenya iibuke na ushindi wa mabao 3-2.
Kipindi
hicho, Kenya ilikuwa chini ya kocha kijana, huyu ni Jacob ‘Ghost’ Mulee ambaye
anajulikana kwa kazi nzuri.
Ushindi
ule, uliwafanya Watanzania waliojazana kwa wingi Kirumba waanze kutoka
taratibu. Habari ikaisha, kila mmoja wetu, waandishi na mashabiki wa kawaida,
tulikubali iko siku Oliech atacheza soka Ulaya. Kweli, sasa anakipiga nchini
Ufaransa.
Michuano
ya Kombe la Kagame inaendelea katika jiji la Dar es Salaam na gumzo kubwa sasa
ni mshambuliaji Michael Olunga wa Gor Mahia ambao ni mabingwa wa Kenya.
Olunga
raia wa Kenya pia, sasa ana umri wa miaka 21 na ameonyesha uwezo mkubwa ingawa
haujawa wa kutosha kupita kiasi.
Lakini
kwa kuwa Tanzania haina mshambuliaji hata mmoja katika timu zake tatu ambaye
ameonyesha ni hatari kweli au zaidi ya Olunga, maana yake lazima yeye awe gumzo
na mjadala mkuu.
Olunga
amecheza mechi mbili, moja dhidi ya Yanga na nyingine dhidi ya KMKM ya
Zanzibar. Katika mechi hizo amefanikiwa kupachika mabao matatu.
Nakukumbusha
katika mechi hizo mbili alizofunga mabao matatu ni dhidi ya ngome za timu za
Tanzania yaani Yanga aliyoifunga bao moja na KMKM mabao mawili.
Amezinyanyasa
timu mbili za Tanzania, kupitia safu mbili za ulinzi zinazoongozwa na
Watanzania kwa asilimia 90. Ndiyo maana Olunga kawa gumzo na vyombo vya habari
vya Tanzania na nchi jirani, viko ‘busy’ kuhusiana naye.
Vyombo
vya habari vimekuwa ‘busy’ naye kwa kuwa Watanzania wengi wanataka kujua
kuhusiana naye. Sasa ni gumzo, kwamba atakwenda Yanga au Simba, maana Azam FC
nao imeelezwa kwamba wanammezea mate.
Stori
yake ndiyo ile ya Oliech ambaye kipindi kile ilielezwa angesajiliwa na Simba,
hata hivyo ikashindikana kwa kuwa ilikuwa na watu kama kina Athumani Machuppa
na Oliech mwenyewe alionyesha msimamo kwa kuwa ndoto yake ilikuwa ni kucheza
Ulaya.
Olunga
ambaye ni mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ufundi nchini Kenya, tayari amesema yu
tayari kucheza kokote lakini anachoangalia ni maslahi, ingawa zaidi angependa
kucheza Ulaya.
| KIKOSI CHA GOR MAHIA, OLUNGA WA PILI KUTOKA KUSHOTO WALIOSIMAMA. |
Tayari
aliwahi kukataa kujiunga na Super Sport United ya Afrika Kusini kwa sababu moja
tu. Ilishindwa kumpatia nafasi ya kujiendeleza kimasomo kwa kuwa alitaka
kucheza soka huku akisoma.
Tangu
Kenya walipompeleka Oliech Ulaya baada ya kuwa ameibukia hapa nyumbani kwetu
kwa kuipa nchi yake Kombe la Cecafa. Leo ni miaka 13, Tanzania haina mchezaji
yeyote anayecheza Ulaya hasa katika ligi tano kubwa za England, Hispania,
Ujerumani, Italia na Ufaransa.
Katika
miaka hiyo 13, Tanzania imeendelea kuendeleza maneno, yaani fitna, watu
wasiopendana katika mpira hadi tumeibukia kwa Olunga na sasa amekuwa gumzo,
hakuna ubishi kama ataendelea hivyo, basi iko siku atacheza Ulaya.
Mulee
ambaye sasa ni mchambulizi katika runinga ya SuperSport, kipindi hicho alikuwa
kocha na mlezi wa Oliech kisoka. Sasa Mulee ndiye mlezi wa Olunga na hawezi
kwenda timu yoyote bila ya kuhusishwa kwa kuwa alianza kuchipukia kisoka katika
kituo chake cha malezi ya wanasoka vijana, pia ile michuano ya Airtel Rising
Stars ambayo mara moja ameibuka kuwa mchezaji bora.
Tokea
kwa Oliech hadi kwa Olunga, hapa nyumbani kuna nini ambacho kinaweza kuelezwa
ni sehemu ya mpira kupiga hatua?
Kumezea
mate si jambo baya, lakini katika soka kuendeleza watu wako ni jambo jema.
Simba, Yanga na Azam zinazommezea mate mshambuliaji huyo zimefanya nini kwa
vijana wa Tanzania?
Huu
ndiyo msimu wa kwanza kwa Olunga kutamba kwenye Ligi Kuu Kenya. Kama umaarufu
zaidi, atakuwa ameupata kwenye Kagame, michuano inayofanyika Dar es Salaam.
Inafanyika
katika ardhi yenye waoga wengi, wasiopendana wengi na wenye uwezo mkubwa wa
kutamani na kusifia vya wenzao huku wakijivunia maendeleo ya wenzao.
Sioni
kama kuna ubaya kumpa Olunga sifa zake kwa kuwa anafanya vizuri. Lakini kama ni
sahihi kuendelea kuwa washangiliaji, wasindikizaji na watoa fursa kwa wageni
kung’ara na kuigeuza nchi ya Tanzania sehemu ya watu kupitia kwenda kwenye
mafanikio makubwa. Zindukeni, furahieni vya wenzenu lakini nafsi ziwaume, mtengeneze
na vyenu na wanaotengenezwa nao wajitume. Mwe!







0 COMMENTS:
Post a Comment