Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zakaria Hans Poppe, ameibuka na kusema kipa namba moja wa Gor Mahia ya Kenya, Boniface Oluoch, ni mzuri ila wanatakiwa kumuona kwenye mechi nyingine huku mwenyewe akisema anataka kuichezea timu hiyo.
Kipa huyo amesema ana mambo matatu yanayomfanya kukubali kuichezea Simba kama watakubaliana kila kitu kwa kuwa ameelezwa ndiyo timu inayomfaa.
Simba kwa sasa inahaha kutafuta kipa ambaye atakuwa akisaidiana na Ivo Mapunda baada ya kocha wa makipa Abdul Salim kusema kuwa aliyekuwa kipa msaidizi wa timu hiyo, Peter Manyika, bado anatakiwa kuwa na uzoefu.
Oluoch alionyesha uwezo mkubwa katika mchezo dhidi ya Yanga huku akiokoa penalti ya beki wa Yanga Nadir Haroub ‘Cannavaro’ kwenye mchezo wa kwanza wa Kombe la Kagame.
Hans Poppe amesema wamevutiwa na kipa huyo kwani alionyesha uwezo mzuri kwenye mechi dhidi ya Yanga lakini hawawezi kumjaji kwa mechi moja au mbili.
“Kipa wa Gor Mahia ni mzuri lakini hatuwezi kumsajili kwa mechi moja au mbili, bado tunazidi kumuangalia kwa kuwa tunataka kipa mwenye rekodi na uwezo wa kuisaidia timu yetu,” alisema Hans Poppe.
Taarifa zimekuwa zikisema kuwa Simba imeshaanza mazungumzo na timu hiyo na kuna uwezekano ikamsajili kipa huyo mara baada ya kumalizika kwa Kagame.
Alipotafutwa kipa huyo ambaye anaichezea timu ya taifa ya Kenya, alisema yupo tayari kucheza Tanzania na timu anayoona inamfaa ni Simba pekee.
“Nipo tayari kucheza soka Tanzania na timu nitakayopenda kujiunga nayo ni Simba.
Kuna vitu ambavyo vinanipelekea kupenda kucheza hapa, moja ni mfumo mzuri wa kuajiri Wakenya kuliko timu yoyote hapa nchini.
“Kitu kingine kinachonifanya nikubali kujiunga na Simba ni kwamba ndugu yangu Jerry Santo, aliyewahi kuichezea klabu hii aliniambia hapa kuna maisha mazuri kuliko sehemu nyingine, pia napenda kufanya kazi na kocha, Salim ambaye ni mzuri kwa kuwafundisha makipa,” alisema Oluoch ambaye amebakiza mkataba wa mwaka mmoja na miezi minne katika kikosi cha Gor Mahia.







0 COMMENTS:
Post a Comment