August 3, 2015

KAMUSOKO
Siku chache baada ya kikosi cha Yanga kutupwa nje ya michuano ya Kombe la Kagame, iliyofikia tamati jana Jumapili huku benchi la ufundi la timu hiyo likigundua kilichoimaliza, sasa limeutaka uongozi wa klabu hiyo kuhakikisha unamsajili kiungo mkabaji wa FC Platinum ya Zimbabwe, Thabani Kamusoko.


Benchi hilo la ufundi la Yanga linaloongozwa na Mholanzi, Hans van Der Pluijm, linadaiwa kufikia uamuzi huo hivi karibuni baada ya kukaa pamoja na uongozi wa klabu hiyo na kujadili majina matatu ya viungo wakabaji waliokuwa wamependekezwa.

Majina mengine yaliokuwa yamependekezwa na benchi hilo la ufundi la Yanga ni pamoja na Khalid Aucho wa Gor Mahia ya Kenya pamoja na Mkenya Anthon Akumu ambaye anaitumikia Al Khartoum ya Sudan.

Hata hivyo, miongoni mwa wachezaji hao, Kamusoko ndiye anadaiwa kupewa nafasi kubwa ya kujiunga na timu hiyo kutokana na kupigiwa upatu na viongozi wengi wa klabu hiyo, wakiwemo pia baadhi ya wachezeji waandamizi wa kikosi hicho cha Yanga.

Habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga zimedai kuwa, tayari uongozi umeshaanza harakati za kuhakikisha unainasa saini ya kiungo huyo maarufu kwa jina la Rasta ambaye alikuwa ni miongoni wa wachezaji wa FC Platinum waliowasumbua vilivyo wachezaji wa timu hiyo yenye makao makuu Jangwani jijini Dar, zilipokutana katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika.

“Endapo itashindikana kumsajili mchezaji huyo, ndipo tutakapowageukia hao wengine lakini kwa sasa Rasta huyo ndiye chaguo letu la kwanza.

“Kila mtu anaujua uwezo wake kwani alitusumbua sana tulipocheza na FC Platinum, hivyo baada ya benchi letu la ufundi kugundua upungufu katika michuano ya Kombe la Kagame kwenye nafasi ya kiungo mkabaji, likapendekeza asajiliwe kwa sababu ana uwezo mkubwa wa kuiunganisha timu, hivyo tukimpata ni matumaini yetu kuwa atasaidiana vizuri na Makapu (Said Makapu),” kilisema chanzo cha habari.


Alipotafutwa Katibu Mkuu wa Yanga, Dk Jonas Tiboroha ili aweze kuthibitisha juu ya taarifa hizo, hakuweza kupatikana hadi tunakwenda mitamboni, kufuatia simu yake ya mkononi kuita bila kupokelewa, hata hivyo kwa upande wake, mkuu wa kitengo cha habari cha klabu hiyo, Jerry Muro, alipoulizwa kuhusiana na mpango huo, alisema: “Habari hizo ni ngeni kwangu, hivyo siwezi kuzizungumzia, hivyo kama zipo basi tutawajulisha.”

0 COMMENTS:

Post a Comment

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic