MAJIMAJI |
Siku chache baada ya kocha wa Majimaji ya
Songea iliyopanda Ligi Kuu Bara msimu huu, Raia wa Finland, Mike Lonnstrom,
kuwasili nchini, ameweka wazi baadhi ya mikakati yake ndani ya timu hiyo ikiwemo
kufanya usajili wa nguvu ili kujenga timu iwapo ataona kuna upungufu.
Kocha huyo raia wa Finland, alisema ana
mikakati mizito ya kuifanya timu hiyo kuwa na uwezo wa kupambana na timu kubwa
za hapa nchini, zikiwemo Azam, Simba na Yanga, hivyo atakaa na wachezaji wake
na kuwaangalia, hasa safu ya ushambuliaji na kama hataridhika nao, basi
atamtafuta mshambuliaji ambaye hana mbwembwe nyingi uwanjani, bali kazi yake ni
kufunga tu.
Kocha huyo mwenye leseni A ya ukocha ya
Shirikisho la Soka Ulaya (Uefa), alisema kuwa licha ya wengi kuamini kuwa
mshambuliaji mzuri ni lazima awe mrefu, yeye hataangalia suala la urefu, bali
atakachokiangalia ni uwezo wa kufunga tu.
“Kama nitakuta kuna tatizo la ushambuliaji,
basi sitaenda mbali, nataangalia wa kumsajili kutoka hapahapa nchini, ila
kawaida yangu siangalii umbo wala mbwembwe za mchezaji, bali kigezo kikubwa
ninachokiangalia sana ni uwezo wake wa kufunga mabao, huyo ndiye nitapigania
kumchukua,” alisema Lonnstrom.
0 COMMENTS:
Post a Comment