Katakata hovyo ya umeme ambao upo chini ya Shirika la
Umeme Tanzania (Tanesco) kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar, juzi Jumatano
kulisababisha hali ya mvurugano mara baada ya mechi ya Yanga dhidi ya Tanzania
Prisons.
Mvurugano huo ulitokea baada ya mechi hiyo ambapo
kiza kilitawala katika vyumba vya kubadilishia nguo, hali iliyosababisha
wachezaji wa Yanga na wale wa Prisons ambao walikuwa wametoka kucheza, kupata
wakati mgumu katika kubadili nguo na kubeba vitu vyao kwenye vyumba hivyo.
Timu hizo zilikutana katika mchezo wa Ligi Kuu
Bara ambapo wachezaji wa timu zote walilazimika kutumia mwanga wa simu zao
kuonana.
SALEHJEMBE ilishuhudia hadi viongozi wa timu zote
nao wakipata wakati mgumu kuonana na kufanya shughuli zao.
Alipoulizwa meneja wa uwanja huo, Rish Urio juu
ya tatizo hilo alisema “Tatizo ni Tanesco, najaribu kulishughulikia, acha
kwanza nimalizie kwa sababu yakitokea matatizo huko nje, Tanesco pia hawawezi
kuzuia ila tunazo ‘phase’ mbili zinafanya kazi badala ya tatu ambazo kwa
kawaida ndizo zinatumika, nadhani baada ya muda mfupi utarejea.”
0 COMMENTS:
Post a Comment