Na
Saleh Ally
TAIFA
Stars imeamsha matumaini upya kwa Watanzania kwa kuitandika Malawi mabao 2-0
katika mechi ya kuwania kucheza Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka 2018.
Moja
ya mambo ambayo yamekuwa magumu katika timu yetu ya taifa kwa miaka nenda rudi
ni kucheza michuano miwili mikubwa, Afcon na Kombe la Dunia.
Kila
Mtanzania mpenda soka au michezo kwa ujumla atakuwa anatamani kuiona hiyo hali
tukiifikia. Kwamba Taifa Stars inakwenda kushiriki Afcon au ikiwezekana Kombe
la Dunia, dah! Acha ifike.
Hata
hivyo siku hiyo, haiwezi kufika kwa ndoto tukiwa tumelala. Lazima kupambana na
kuwa na mipango endelevu ambayo inaangalia mbele angalau kwa uchache wa miaka
10 mbele yetu.
Miaka
10 mbele, haiwezi kuwa mipango yenye wigo finyu ambayo unaangalia vitu
vichache. Lazima watu wafungue vichwa vyao kweli na kujua kipi wanakitaka na
kukisimamia kwa miaka yote tena kukiwa na mipango na maendeleo.
Mipango
inaanzia kwa vijana kwenda mbele. Lazima watu waachane na mambo ya kuripua,
wakiamini ushindi wa leo ndiyo kila kitu.
Tumekaa
kando muda mwingi sana, huu ndiyo wakati wa vitendo na baada ya Taifa Stars
kuitwanga Malawi kwa mabao 2-0 angalau kunainuka matumaini upya kwamba kuna
uwezekano wa kufanya jambo Fulani.
Hiyo
ni habari njema au dalili ya kuonyesha tunaanza kwenda ingawa Watanzania lazima
waweke vichwani mwao kwamba kwa kuwa Stars inashiriki mechi za soka, kupoteza
siku yoyote inawezekana pia ni jambo la kawaida na wasianze kelele kwa kupoteza
mechi moja.
Katika soka kuna kuteleza na kuinuka na uwezekano wa kufanya hivyo
kabla ya kuanguka upo.
Lakini
lazima tukubali, Stars haikucheza vema kama ilivyokuwa katika mechi dhidi ya
Nigeria. Hii ni changamoto pia inayoonyesha bado safari ni ndefu na hakuna haja
ya kuridhika.
Wakati
nikishuhudia mechi ya Stars dhidi ya Malawi ambayo mabao mawili ya mechi ya
yalifungwa na Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu, nilianza kufikiri kuhusiana
na washambuliaji hao wawili wa TP Mazembe.
Samatta
na Ulimwengu sasa ni lulu ambayo Watanzania ambao wanajivunia. Swali likawa
hivi, hivi bila ya hawa wapiganaji wawili? Tunakwenda vip?
Nakumbuka
mechi zote ambazo wanakosekana, mara nyingi John Bocco amekuwa mkombozi. Lakini
kweli tuna watu ambao tunaamini kweli ndiyo sahihi wanaweza kushika mikoba ya
Samatta na Ulimwengu?
Lazima
tukubali wao ni binadamu, wanaweza kuwa wanaumwa au majeruhi na Tanzania ina
mechi muhimu sana ambayo inatakiwa kushinda. Ndani ya 11 hayumo Samatta na
Ulimwengu, kweli tunaweza kuwa na kikosi kitakachopambana mwanzo mwisho na kusababisha
ufungaji wa mabao.
Achana
na hawa wawili, nguvu ya kule mbele kwa Taifa Stars pia inaongezwa na Mrishi
Ngassa. Watakaokuwa wanamsahau basi wanafanya makosa sana, ana msaada mkubwa
ingawa namba yake ya pembeni angalau utasema kuna watu mbadala kama Simon Msuva
au Farid Mussa.
Lakini
kwa Ulimwengu na Samatta ambao ni washambuliaji wenye uwezo wa mengi wasiyoweza
wengi. Mfano kuingia na mpira wakiwa wamezongwa na mabeki hadi watatu, kutoa
pasi zinazozaa mabao au kufunga kwa uwezo binafsi. Nani mwingine wa hapa
nyumbani?
Ninaweza
nikawa nawauliza mashabiki, lakini kwa wachezaji wenyewe wakiwa na timu zao
chini ya klabu, wanaona kazi ya kina Ulimwengu na Samatta na kweli wanajifunza
kwamba wako tayari kuwa washindani?
Inawezekana
kabisa mchezaji akawa anacheza nyumbani na kuonekana ni mshindani wa yule
anayecheza nje ya nyumbani. Mfano mzuri Ahemd Musa wa Nigeria, alianza kupata
namba akiwa anacheza nyumbani licha ya Super Eagles kuwa na nyota wengi
wanaocheza nje ya Afrika. Sasa yuko CSKA Moscow na tegemeo la nchi yake.
Nani
anathubutu kuwa mpinzani wa Samatta na Ulimwengu hapa nyumbani. Ikiwezekana
siku moja apate timu nje lakini hata kama bado, ndiye aonekane mbadala wa
wawili hao na siku moja wakija wakae benchi huku yeye akiisaidia Stars kupata
ushindi.
Hili
ni jambo ambalo hata Kocha wa Taifa Stars, Charles Boniface Mkwasa na msaidizi
wake, Hemed Morocco wanapaswa kuliangalia kwa maana ya kuwa na kikosi kipana
zaidi chenye kulenga kupambana kwa muda mrefu.
0 COMMENTS:
Post a Comment