October 9, 2015


Na Saleh Ally
WAKATI timu ya soka ya taifa, Taifa Stars inapambana kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, hakukuwa na idadi kubwa sana ya watu.


Mechi hiyo imepigwa juzi kwenye Uwanja wa Taifa na Stars ikaibuka kwa ushindi wa mabao 2-0 na kufanikiwa kuamsha matumaini ya kufanya vizuri katika mechi hizo za awali za kuwania kucheza Kombe la Dunia.

Idadi ya watu kuwa chache niliichukulia kama sehemu ya matatizo na mawili niliyapa kipaumbela kabla ya kulisikia la tatu ambalo ndiyo limeamsha mjadala wa leo.

Tatizo la kwanza, niliona watu wengi walishindwa kufika pale uwanjani kwa kuwa ilikuwa ni siku ya kazi. Wengi walikuwa kazini, hivyo hawakuwa na namna zaidi ya kubaki wakiendelea na majukumu ya kujiingizia kipato, iwe waajiriwa au wamejiajiri.

Tatizo la pili, lilikuwa ni foleni ambayo ilisababisha watu wengi waone uvivu kwenda uwanjani na kuamua kumaliza hamu yao ya kuangalia soka katika runinga baada ya kusikia kupitia ving’amuzi vya Azam TV mechi hiyo ilikuwa inaonyesha, hali kadhalika DSTV.

Yote mawili hayakuwa na ujanja kwa kuwa ni ratiba inayopangwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), hakuna njia ya kubadilisha hata kidogo.

Tatizo la tatu, kidogo likanishangaza. Nilikutana na watu waliokuwa wakilalama kwamba kiingilio kilikuwa ni kikubwa sana ndiyo maana hawakwenda uwanjani.

Niliwakumbusha Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), lilichukua uamuzi wa kupunguza viingilio kutoka Sh 7,000 kwa kiingilio cha chini kabisa wakati wa mechi dhidi ya Nigeria hadi Sh 5,000 kwa kiingilio cha chini katika mechi dhidi ya Malawi.

Lakini watu wakapungua zaidi na hicho ni moja ya chanzo wao kutokwenda uwanjani. Hili la mwisho sikukubaliana nalo hata kidogo na mwisho nikaanza kupata hisia heshima ya soka inashushwa kupindukia kwa kuwa watu wanaweza kuzungumza lolote.

Lazima tukubali kwamba maisha ni magumu, fedha pia ni ngumu. Lakini katika maisha ya kawaida, kamwe hauwezi kuishi kwa kula, kulala na kuvaa pekee. Badala yake unalazimika kupoza kichwa kwa kupata vitu ambavyo vinaburudisha kichwa chako.

Kila binadamu anatakiwa ku-relax na hii ni bora kwa afya. Kinachokufanya ufikie huko ni kile ambacho kinapoza moyo wako na aunachoweza kukiita burudani. Hata kama hutakubali, nakukumbusha “Starehe gharama”.

Basi kama unapenda, lazima ujue nao utakuwa gharama. Kwa nini tunataka kuushusha mpira hadhi kiasi hicho kwa kisingizio cha kukosa kabisa fedha au kiingilio kikubwa?

Soka itaendelea kushushwa thamani kila siku kwa madai watu wamekosa wakati watu haohao wanaingia kwenye bendi mbalimbali wakilipa Sh 10,000 kuwaona wasanii kama Christian Bella, Nyoshi El Saadat na wengine huku wakiona nusu ya hiyo kuwaona nyota wanaotamba Afrika kama Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu au wanasoka nyota wa nyumbani kama Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Ndemla, Himid Mao na wengine eti ni ghali.

Kwa mnaopenda soka, hata kama tutakuwa tunatetea mambo, wakati mwingine lazima tuangalie. Kama kweli Mtanzania anashindwa kupata Sh 5,000 ya kuiona timu yake ya taifa inacheza.

Hapa kuna suala la uzalendo, lakini bado ukiingia uwanjani unapata burudani inayotolewa na wanasoka wa timu unayoiunga mkono na wapianzani wao. Sasa kweli unaona si sahihi kulipa?

Nilifikiri ifikie tuwe wakweli, tuonyeshe heshima kwa mpira ambao tunataka uwe mkubwa. England ambako tunaangalia na kuufurahia, mechi moja wanalipa zaidi ya 100,000 na ndiyo kima cha chini katika baadhi ya mechi.
Hakika tuonyeshe mapenzi na tusitake kuufanya mpira hauna thamani kabisa, kama tunataka huku tunaushusha hadhi, ni sawa na kupigana vita kwenye kiza.





1 COMMENTS:

  1. Nadhani tatizo ni TFF, ipo wazi kuwa Jumatano ni siku ya kazi na ndio maana ulaya wanazipiga mechi usiku. Ofisi nyingi za kibongo zinafungwa saa 11 jioni kwenda mbele sasa mpaka atoke mtu na mafoleni ya kibongo atafika taifa saa moja usiku mpira ushaisha zamanii. Kwann wasijaribu kucheza usiku siku za week days waone response ya wananchi?

    ReplyDelete

TwitterFacebookGoogle PlusLinkedInRSS FeedEmail

GONGA HAPA KWENDA AZAM TV

B2.jpg
Image and video hosting by TinyPic