Na Saleh Ally
KUMEKUWA na kawaida ya watu wengi sana
hawataki kuona wachezaji wakisifiwa na vyombo vya habari, wanadai ikifanyika
hivyo, basi wachezaji wanavimba vichwa na kuishia njiani.
Kila mtu ana akili zake, huwezi kumlazimisha
zikapanda. Kazi yangu kuandika, mchezaji yake ni kucheza. Akishindwa kuifanya
yake wakati nimefanya yangu, atafeli yeye, mimi nitaendelea.
Leo nimeamua kusifia sana, pia kuasa kwa
kuwa kuna kitu nimekiona. Huenda kuna wengine wamekiona lakini walishindwa
kusema au walipuuzia, lakini mimi nakianika.
Kiungo wa pembeni wa Azam FC, Farid Mussa,
ambaye sasa yuko katika kikosi cha timu ya taifa, Taifa Stars, kwangu ni
mchezaji ambaye naweza nikasema ni zawadi.
Tanzania ina vipaji vingi sana, iwe ni
mchezo wa soka au mingine. Lakini kumekuwa hakuna njia sahihi ya kuvisaka,
kuviendeleza vipaji.
Nchi yetu ina zawadi kubwa ya vipawa vya
kila aina kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Nataka nikuhakikishie, Farid ambaye sasa
ana miaka 19, ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kwake, kwa familia yake.
Nasema ni zawadi kwa Watanzania kwa kuwa
tunahitaji wachezaji wa aina yake, wachezaji wenyewe uwezo mkubwa ambao
unaonekana ni tofauti au una jipya ndani ya mchezo wa soka.
Tanzania inahitaji wachezaji wa kwenda nje
ya mipaka ya nchi hii ili baadaye wawe msaada kwa taifa letu ambalo pamoja na
kutaka timu imara ya taifa, lakini kuna mambo kadhaa ya kufanya kwanza ili
kuingia ili kupata msaada huo.
Mfano, kuwa na wachezaji wengi wanaocheza
nje ya Tanzania kama unavyoona Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wanaocheza TP
Mazembe ya DR Congo walivyo msaada mkubwa kwa sasa.
Utaona wameiwezesha kufika fainali ya Ligi
ya Mabingwa Afrika. Hakika changamoto wanazokutana nazo, wanaporejea kuitumikia
Taifa Stars wanakuwa ni msaada mkubwa sana.
Sisemi wachezaji wanaocheza hapa nyumbani
hawana msaada, lakini lazima tuchanganye ili kuwe na changamoto ya nguvu ya
kutoka ndani na nje.
Utaona hata hao Nigeria, Ghana, Ivory Coast
wamekuwa na mafanikio makubwa kutokana na wachezaji wanaocheza nje ya nchi zao.
Nchi kama Misri imekuwa ikijitutumua kwa kutumia wachezaji wa nyumbani, lakini
sisi bado hatuna ligi imara yenye timu zenye utajiri unaojibeba ili kutuwezesha
kutegemea timu za nyumbani kuwa na kikosi imara cha timu ya taifa.
Nikiwa Uturuki kwenye kambi ya Taifa Stars,
nilipata bahati ya kusoma mambo mengi sana ya Farid ndani na nje ya uwanja.
Niligundua ni mchezaji ambaye ana hamu ya mafanikio ambaye pia anajitambua
sana.
Alinifurahisha kwa kuwa anaonyesha ana
nidhamu na msikivu. Kidogo tu, alikuwa anaonyesha ‘utoto’. Jambo ambalo
niliamini linaweza kuendana na umri wake. Mfano, wakati wenzake wamejipanga
kwenye msitari katikati ya mazoezi, yeye aliendelea kucheza “Bolingo”.
Hilo linaweza kuwa dogo sana, lakini
uwanjani, ana kasi, nguvu, akili ya haraka, krosi za nguvu, nguvu ya kupiga
mashuti na kipimo changu cha kwanza ilikuwa ile mechi mazoezi kati ya Stars
dhidi ya Libya. Farid alitoa pasi kwa Simon Msuva baada ya kuwachambua mabeki
wawili, wakamuangusha na kuwa penalti aliyofunga John Bocco.
Uwezo wa Farid katika miaka 19 unaonyesha
uko juu. Utaona hata Kocha Charles Boniface Mkwasa ameonyesha wazi kweli
anamuamini. Angalia kikosi cha Stars
kilichoivaa Nigeria, alikuwa kati ya wachezaji wanne waliokuwa mbele kusukuma
mashambulizi katikati na pembeni.
Wachezaji hao ni Samatta, Ulimwengu, Mrisho
Ngassa na Farid. Watatu, wote wanacheza nje ya Tanzania, Farid pekee ndiye
alikuwa anatokea ndani ya Tanzania. Hakika alicheza vizuri sana kwa muda wote.
Huyu bwan’mdogo hakika ni zawadi ambayo ni
muhimu sana kwa soka la nchi yetu. Anachotakiwa ni kujitambua halafu
ajiendeleze na si kujitambua halafu aanze maringo na kujisahau.
Lakini kwa upande wa wadau, tunatakiwa kumpa
nafasi, kumkubali na ikiwezekana inapofikia wakati wa Taifa Stars ni kumsaidia.
Angalia leo kwa umri wake, anapata nafasi Stars na wangapi unaowaamini
wameikosa?
Angalia Azam FC, anapata nafasi ya wachezaji
11 wa kwanza, jiulize wangapi hawana. Wengine wachezaji wa kigeni wameachwa kwa
kuwa kocha anaona anaweza.
Ninaamini kabisa, Farid anatakiwa kuondoka
nchini kwenda nje, iwe Ulaya au timu kubwa sehemu nyingine Afrika ili
akajiendeleze. Anaweza kuja kuwa mshambuliaji tishio Afrika na hilo
linawezekana, maana tayari Ulimwengu na Samatta wameweza.
Nimekuelewa mno Saleh
ReplyDeletebinafsi sijapata nafasi ya kumuona mazoezini lakini nimemuona mechi kadhaa za Azam na zile za Taifa hakika neno ZAWADI ni sahihi kulitumia,Mungu alishatupa zawadi nyingi sana hapo kabla hatukuzitumia walau kina Samatta na Ulimwengu wanawaonesha wenzao kuwa inawezekana.
Zawadi nyingine nakushauri uifuatilie ni JOSEPH KIMWAGA aliyekuwa Azam sasa yupo Simba kwa mkopo kisha utatupa majibu.
Kazi njema.