Inawezekana ikawashtua mashabiki na wadau wa
Simba lakini habari ni kuwa, kocha mkuu wa timu hiyo, Dylan Kerr, amewataja
washambuliaji wa TP Mazembe, Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu kuwa ni aina ya
wachezaji ambao anawahitaji kikosini kwake.
Kerr amesema kama ikitokea wachezaji hao
wakamaliza mikataba yao kwenye klabu yao ya sasa, basi anatamani kuona wanatua
Simba na ikiwa hivyo basi mambo yatakuwa bambam kwake katika idara ya
ushambuliaji.
Kauli hiyo inaweza kushangaza wengi kwa kuwa
inajulikana wachezaji hao kwa sasa mipango yao ni kwenda nje ya Afrika kucheza
soka la kulipwa na siyo kurejea Tanzania kucheza katika ngazi ya klabu.
Kerr alitamka hivyo juzi mara baada ya kuwaona
Samatta na Ulimwengu wakiiongoza Taifa Stars kuibuka na ushindi wa mabao 2-0
dhidi ya Malawi, kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Kerr alisema
amevutiwa na viwango vilivyoonyeshwa na washambuliaji hao aliowapa sifa ya
upambanaji licha ya kudai pia walipoteza nafasi nyingi za kufunga.
“Kwenye mechi ya Stars nimefurahishwa na viwango
vya wachezaji wote, lakini sana ni wale washambuliaji wawili, yule aliyevaa
jezi namba 10 (Samatta), namba 11 (Ulimwengu) na Ndemla (Said).
“Hao ni aina ya wachezaji ninaowahitaji kwenye
kikosi changu kutokana na uwezo wa kupambana na kuwasumbua mabeki.
“Ninaamini kama nikiwapata kwenye kikosi changu,
basi nitafurahi nikiamini kuwa tatizo la umaliziaji litakuwa limemalizika
kutokana na uwezo wa washambuliaji hao,” alisema Kerr.
Hata kabla ya msimu kuanza, Simba ilikuwa bize
ikitafuta mshambuliaji mwenye uwezo wa kufunga mabao mengi, licha ya Kerr
kuletewa wachezaji kadhaa, bado ilionekana hakuna ambaye amekidhi vigezo, ndipo
hatua ya mwisho wakasajiliwa Msenegal, Pape Nd’aw, Mussa Mgosi na Mganda, Hamis
Kiiza.
0 COMMENTS:
Post a Comment