KIKOSI HIKI CHA TOTO AFRICAN KINA VIJANA SITA KUTOKA SIMBA B, MMOJA AKIWA ALIWAHI KUCHEZA SIMBA KUBWA. |
Na Saleh Ally
SIMBA ni moja ya timu inayojitahidi sana
katika suala la ukuzaji wa wachezaji vijana. Ndiyo maana timu yake ya vijana
ilikuwa maarufu sana.
Simba B ilikuwa ikifanya vema katika
michuano mingi miaka mitatu iliyopita na ikaendelea kuwa gumzo kubwa baada ya
kufanikiwa kutwaa ubingwa wa Kombe la Banc ABC.
Michuano hiyo, Simba pekee iliamua
kupeleka timu ya vijana huku timu nyingine kama Azam FC na Mtibwa Sugar zikiwa
na vikosi vikubwa lakini vikaambulia vipigo, Simba B ikawa bingwa.
Unaweza kushangazwa na namna ambavyo
Simba imekuwa ikisumbuka kipindi hiki kusajili wachezaji kama Pape N’daw kutoka
Senegal ambaye badala ya kucheza soka, amechukua umaarufu katika masuala ya
ushirikina.
N’daw hadi sasa hajapiga hata shuti moja
kali kwenye lango la timu pinzani lakini Simba imetoa lundo la fedha, zaidi ya
Sh milioni 50 hadi kukamilisha kila kitu cha N’daw.
Timu ya watoto ya Simba, pia imepoteza
mwelekeo na ajabu zaidi, utaona wachezaji wengi wa Simba ambao walikuwa katika
timu yake ya vijana ndiyo wanaofanya vizuri katika timu nyingine za Ligi Kuu
Bara.
Achana na kwamba Simba imekuwa ikiwaacha
wachezaji wanaonekana wazuri, kila wanapotoka Simba wanafanya vizuri sana.
Wachezaji wawili, Amissi Tambwe aliyekwenda Yanga na Elius Maguli ambaye sasa
anakipiga Stand United na ndiye anaongoza kwa kufunga mabao.
Simba imekuwa na mwanzo mzuri kwa timu
zake za vijana lakini mwendelezo ni hovyo kwa kuwa viongozi wanaonekana kuwa ni
wenye papara sana.
Ndiyo maana wachezaji wengi ambao huenda
wangekuwa msaada mkubwa kwa Simba, wanakwenda katika timu nyingine na huenda
hapo baadaye Simba italazimika kuwanunua kwa fedha nyingi kuwarudisha nyumbani.
Kuna wachezaji wachache ambao Simba
ilifanikiwa kuwabakiza, mfano Jonas Mkude, Said Ndemla na Ramadhan Singano
‘Messi’ ambaye aliamua kuhamia Azam na kuachana na Simba.
Bado Simba ingeweza kuwakuza zaidi
wachezaji waliokuwa katika kizazi cha Ndemla ambao nina uhakika misimu miwili
ijayo, Simba italazimika kuwatafuta na kuwanunua kwa fedha nyingi.
Ukienda Majimaji utakuta zaidi ya vijana
wanne, wengine wapo kwenye kikosi cha Toto Africans kilichofungwa na Yanga kwa
mabao 4-1 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, kilionyesha soka safi
sana na kuwapa Yanga wakati mgumu.
Tatizo kubwa likaonyesha wachezaji wake
hawakuwa na uzoefu. Kikosi chake cha kwanza kilikuwa na wachezaji sita kutoka
Simba B ambao msimu uliopita waliamua kuondoka baada ya kuona Simba B
haieleweki au hakukuwa na mpango wa kuwapa nafasi ya kupanda.
Wachezaji hao Japhet Makaray
‘Balotelli’, Carlos Protus, Miraji Madenge ‘Sheva Go’, Abdallah Seseme, Hassan
Khatibu na Edward Christopher ‘Edo’ walionekana kuwa msaada mkubwa kwa Toto
ambao wako katika nafasi ya 10, utaona safu yake ya ulinzi inaongozwa na Protus
na imefungwa mabao saba, mshambuliaji Sheva Go, pia ni tishio na uliona
alivyokuwa akiwahangaisha akina Kelvin Yondani na Vincent Bossou.
Kiungo Seseme ambaye ndiye alikuwa
anashika nafasi ya pili kupiga pasi ndefu baada ya Athumani Iddi ‘Chuji’ pia
alikuwa moto kwa Yanga.
Si rahisi timu imtumie kila mchezaji
iliyemkuza lakini Simba inatumia asilimia 9 tu ya wachezaji inaowakuza na
mwisho hawaifaidishi kwa lolote kwa kuwa hakuna mipango ya muda mrefu ya
mwendelezo wa wachezaji hao.
Hata kama watakuwa wanaondoka, suala la
Simba imefaidika vipi lina maswali mengi. Inaonekana wazi haiwezekani kabisa
kwani wanaondoka zao tu wanavyotaka au wasivyotaka kutokana na kuona mambo
hayaendi vizuri, lakini Simba haifaidiki.
Simba ni timu inayojitahidi kuwa na timu
ya vijana, lakini suala la timu hiyo linaonekana si mpango wenye malengo ya
mwendelezo wa kibiashara na kupata faida. Ndiyo maana inaweza kuwaacha
wachezaji waende na baadaye kuwanunua.
Angalia mshambuliaji kama Madenge ‘Sheva
Go’, Simba ilihitaji kuwa naye kwa maana ya kumpa uzoefu. Baadaye awe tegemeo,
lakini kesho utasikia ametua Yanga au Azam halafu anakwenda kuwa tishio Simba
ambayo iliona hana lolote jambo ambalo uongozi unapaswa kulitupia macho ya
kitaalamu na si kufanya mambo kama ni sehemu ya kujifurahisha tu.
0 COMMENTS:
Post a Comment